Afisa wa Masuala Endelevu wa kampuni ya TBL Group Irene Mutiganzi akiwa na cheti cha utambuzi wa mchango wa kupambana na saratani kwa wanawake, baada ya kukipokea kutoka kwa Makamu wa Rais,Mh. Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya kampuni kwenye hafla iliyofanyika jijini Mwanza
Afisa wa Masuala Endelevu wa kampuni ya TBL Irene Mutiganzi akisalimiana na Makamu wa Rais Mh.Samia Suluhu Hassan katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya kupima Saratani mkoani Mwanza.
Makamu wa Rais,Mh. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Mwanza,MEWATA na wadau waliofanikisha kampeni ya uchunguzi wa saratani mkoani Mwanza
Makamu wa Rais,Mh. Samia Suluhu Hassan akiagana na katika baadhi ya viongozi wa mkoa wa Mwanza,MEWATA na wadau waliofanikisha kampeni ya uchunguzi wa saratani mkoani Mwanza katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Furahisha.
Kampuni ya TBL Group imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuunga mkono mapambano ya kutokomeza ugonjwa wa Saratani ya Matiti na mlango wa Kizazi nchini ambapo imeungana na wadau wengine kuchangia kufanikisha operesheni ya Chama Cha Madaktari Wanawake (MEWATA) ya kuwafanyia uchunguzi akina mama katika wilaya zote za mkoa wa Mwanza.
Meneja wa Masuala Endelevu wa TBL,Irene Mutiganzi ameeleza wakati wa uzinduzi wa operesheni hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza kuwa kampuni imeamua kuunga mkono mapambano haya ikiwa ni utekelezaji wa moja ya malengo yake ya kusaidia kupambana na changamoto zilizopo kwenye jamii inapofanyia biashara zake.
“Tumekuwa na Programu mbalimbali ndani ya kampuni za kusaidia jamii katika sekta mbalimbali hususani za afya,elimu,maji , mazingira na Usalama.Hivi sasa tumeanza kuunga mkono mapambano ya ugonjwa wa saratani ambao umekuwa ukiongezeka nchini kwa kasi kubwa na kusababisha vifo vingi”.Alisema.
Mutiganzi alisema ugonjwa wa Saratani ya Matiti kwa hivi sasa ni moja ya magonjwa tishio nchini yanayoendelea kuhatarisha maisha ya Wanawake wengi wanaoishi maeneo ya mijini na vijijini.
Alisema TBL Group itaendelea kuunga mkono jitihada za serikali kutokomeza ugonjwa huu kwa kushirikiana na wadau wengine ili kuweza kupunguza kasi yake ya kuenea kwake “Wataalamu wa afya wanashauri kupima afya mara kwa mara ili ugonjwa ukibainika mapema uweze kutibiwa , bado elimu ya uhamasishaji wa kupima haijawafikia wananchi wengi ambapo wanajitokeza hali za afya zao zikiwa zimeanza kuteteleka na ugonjwa ukiwa tayari umesambaa kwa kiasi kikubwa mwilini”.Alisema.
Pia Mutiganzi amesema kuwa kampuni inatekeleza mpango wa Afya kwa ajili ya wafanyakazi wake ujulikanao kama Afya Kwanza ambapo wafanyakazi hupatiwa mafunzo ya afya,jinsi ya kukabiliana na magonjwa ya muda mrefu,kufanya mazoezi,lishe na umuhimu wa kupima afya zao mara kwa mara.”Hivi karibuni katika kuadhimisha mwezi wa Saratani ya Matiti,wafanyakazi pamoja na familia zao walipata fursa ya kupima ugonjwa huu na kupatiwa elimu ya jinsi unavyoanza na namna ya kutambua dalili zake.
TBL Group imetunikiwa cheti kwa kutambua mchango wake katika kufanikisha operesheni ya upimaji Saratani ya Matiti na Mlango wa kizazi mkoani Mwanza ambayo uzinduzi wake umefanyika katika Viwanja vya Furahisha ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mh.Samia Suluhu Hassan.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)