Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Juma Assad
|
Soko la Mwanjelwa jijini Mbeya
|
Na JamiiMojaBlog,Mbeya
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesanu za serikali(CAG), anatarajia kuanza kufanya kazi ya ukaguzi maalum katika halmashauri ya Jiji la Mbeya baada ya kudaiwa kuwepo kwa viashiria vya ubadhilifu wa fedha zilizotumika kukamilisha ujenzi wa soko la Mwanjelwa.
Awali, Agosti 9 mwaka huu, Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa akiwa katika ziara yake Mkoani Mbeya, alifanikiwa kutembelea mradi huo wa soko ambao inasemekana umetumia kiasi cha shilingi Bilioni 26, tofauti na matarajio ya serikali.
Serikali, ilikuwa ikiamini mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 16 lakini kutokana na utendaji kazi wa hovyo unaodaiwa kufanywa na baadhi ya watendaji tena kwa maslahi yao binafsi ulisababisha soko hilo kutumia kiasi cha shilingi bilioni 26.
Hatua hiyo ndio iliyomfanya waziri Mkuu, kumuagiza Mkaguzi Mkuu wa Hsabu za serikali kwenda Mbeya na kufanya ukaguzi wa mradi huo ili kuondoa utata uliopo juu ya kiasi sahihi cha fedha kilichotumika kwenye mradi huo.
Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, David Mwashilindi
|
Akizungumzia hilo, Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, David Mwashilindi amesema kuwa baada ya agizo la waziri mkuu kutolewa, halmashauri ilianza mchakato wa kumuita mkaguzi huyo ili kufika kufanya ukaguzi.
Amesema, kinachofanyika sasa ni kamati ya fedha kuketi kwa ajili ya kupitisha matumizi hayo ya fedha na kazi kuanza kufanyika ikiwa na kutekeleza agizo la Waziri Mkuu.
Amesema Kamati ya fedha inataraji kukaa November 22 mwaka huu, na kutoa maamuzi na kupitisha kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kutumika kwa kazi ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ya kufanya ukaguzi wa fedha katika soko la Mwanjelwa.
Aidha, Meya huyo aliwaomba wafanya biashara wote ambao tayari waliingia mikataba na halmashauri ya Jiji, kuanza kuendesha biashara zao kama makubaliano ya mkataba yanavyoelekeza.
Hata hivyo, aliongeza kuwa tayari halmashauri imeingia mkataba na wakala atakayendesha zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara wote ambao wamekiuka makubaliano ya mkataba kwa kushindwa kuendesha biashara kwa kipindi husika.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)