Wafugaji wamwomba Rais Magufuli kuwanusuru ng’ombe wao - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Wafugaji wamwomba Rais Magufuli kuwanusuru ng’ombe wao

1
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Maghembe Makoye akizungumza na waandishi wa habari wakati akifafanua mambo mbalimbali kuhusu wafugaji walionyaganywa mifugo yao na uongozi wa hifadhi ya Pori la akiba Katavi , Kushoto ni mfugaji anayelalamikia kunyang'anywa mifugo yake Mayunga Gamasa na kulia ni mfugaji Charles Mtokambali.
2
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Maghembe Makoyeakionyesha hukumu iliyotolewa na mahakama kuu Kanda ya Sumbawanga ili wafugaji hao warudishiwe mifugo yao kushoto ni Mayunga Gamasa mfugaji na kulia ni mfugaji Charles Mtokambali.

NA MWANDISHI WETU
WAFUGAJI wa mkoa wa Katavi, wamemwomba Rais John Magufuli kuwasaidia kurejeshewa mifugo yao 1,600 ambayo imeshikiliwa na watendaji wa hifadhi ya Katavi.

Wamesema mifugo hiyo aina ya ng’ombe ilikamatwa Machi mwaka huu na kufunguliwa kesi lakini baada ya kesi hiyo walishinda na kuamliwa kurejeshewa ng’ombe zao lakini mpaka sasa amri hiyo haijatekelezwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wamesema, kutokana na unyanyasaji wanaofanyiwa na watendaji hao wa hifadhi, Rais Magufuli ambaye ni mtetezi wa wanyonge atupie jicho suala lao na kulimaliza.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Maghembe Makoye alisema wafugaji waliochukuliwa mifugo yao hivi sasa familia zao zinaishi maisha ya shida kwani hawana njia mbadala wa kupata fedha na ufugaji ndiyo tegemeo lao.

“Tunamwomba Rais Magufuli aingilie kati jambo hili ili Watanzania hawa wanyomge wapate haki yao. Tunanyanyasika katika nchi yetu, huku chini kuna watu wanaendesha serikali zao, hawajui juu kuna Magufuli, tunamwomba sana Rais alione hili,” alisema Makoye

Alisema agizo la Rais la kuwataka wakuu wote wa mikoa kubaini na kutenga maeneo kwa ajili wafugaji nchini limeshindwa kuchukuliwa kwa uzito wake mpaka sasa hivyo umefika wakati wa kulifanyia kazi.

Katibu huyo alisema katika kufanikisha agizo hilo la Rais Magufuli kwa ufanisi, wameomba kushirikishwa ili kumaliza migogoro iliyopo kati ya wafugaji na wakulima.

Naye Mayunga Gamasa alisema kati ya ng’ombe hizo 1600 yeye zake ni 552 ambazo kukamatwa kwake zimemfanya kuwa masikini huku familia yake yenye watu zaidi ya 70 ikiishi kwa shida kwani chanzo cha mapato ndiyo hicho kimeondoka.

“Mimi nina watoto 28, waijukuu 24, wake wane jumla na wasaidizi kama watu 70, sasa ng’ombe hawa ndiyo msaada kwangu, lakini uongozi wa hifadhi ya Katavi haitaki kutupatia licha ya kushinda kesi, tunaomba Rais atusaidie” alisema Gamasa

Naye Charles Mtokambali mwenye ng;ombe zaidi ya 700, alisema kunyimwa kwa ng’ombe hao kumebadili maisha yake kwani kwa sasa familia yake haijui kesho yake, kutokana na watendaji hao wa hifadhi huku akisema ana imani kubwa na Rais kwamba atalishughulikia suala hilo.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages