Pages

MAKAMU WA RAIS AHIMIZA WATOTO KUPEWA ELIMU KATIKA MASHINDANO YA KUHIFADHI QURAN

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) akiwasili kwenye ukmbi wa Diamond Jubilee ambapo kulikuwa na mashindano ya kuhifadhi Quran yalioandaliwa na Taasisi Isiyo ya Kiserikali ya Aisha Sururu.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) akizungumza na Mwenyekiti Mtendaji wa Taasisi ya Aisha Sururu  Bi. Aisha Sururu (kushoto) na Katibu wa Taasisi hiyo Bi. Joha Lemky wakati wa mashishindano ya kuhifadhi Quran yaliofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee.
 Sehemu ya Viongozi waliohidhuria mashindano hayo ya kuhifadhi Quran
 Majaji wa Mashindano ya kuhifadhi Quran yalioandaliwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya  Aisha Sururu kwenye ukumbi wa Diamond.
 Sheikh Muharami Mziwanda akitoa elimu juu ya umuhimu wa kuijua Quran kwenye mashindano ya Kuhifadhi Quran yaliofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee.
 Kijana mwenye ulemavu wa macho Ali Hamisi Mpemba akisoma Juzuu 30 wakati wa mashindano hayo.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akitoa nasaha zake mara baada ya shindano la kuhifadhi Quran lililoandaliwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Aisha Sururu.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidi mshindi wa kwanza kwa upande wa wanawake na mshindi wa jumla wa kuhifadhi quran juzuu 30 ,Ashura Amani (16) mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya Benjamini Mkapa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa kike walioshiriki mashindano ya kuhifadhi quran kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee.


Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi nchini kuhakikisha wanawapa watoto wao elimu tangu wakiwa wadogo ili iwajengee misingi bora katika  maisha yao. Mheshimiwa Samia ameeleza hayo wakati akizungumza kwenye mashindano ya Qur'an yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es salaam. Alisema wazazi wanapaswa kutambua kuwa hakuna zawadi kubwa kwa mtoto kama elimu kwa sababu itamjengea misingi ya kujua afanye nini katika kuendesha maisha yake kwa mafanikio.


"Vile vile, niwaombe wazazi tuwatengenezee watoto wetu fursa wapate muda wa kupata 
elimu. Ukimpa utajiri mtoto na kwa kuwa hana elimu anaweza asiutumie vizuri; 
lakini ukimpa elimu itamfaa katika kuendesha maisha yake," alisema Makamu 
wa Rais. Aidha, aliwataka washindi wote wa kuhifadhi Qur'an wasisite kutafuta elimu zaidi ya dini na ya dunia kama maandiko ya kitabu kitakatifu cha Qur'an yanavyousia ili iweze kuwasaidia ulimwenguni na huko akhera kwenye maisha ya milele. 
Makamu wa Rais alielezea kufarijika kwake kuona kuwa idadi ya washindani inaongezeka kila mwaka bila ya kubagua jinsia zao na washiriki wa mashindano hayo wakiwa na umri mdogo.


"Hii inaonyesha kwamba vijana wanayo fursa nzuri ya kuhifadhi Qur'an Tukufu tena 
juzuu nzima wakiwa wadogo endapo sisi kama wazazi tutalifanyia kazi na kuwahimiza vijana wetu," alidokeza. Mapema Katibu wa Taasisi ya Aisha Sururu Foundation iliyoandaa mashindano hayo Bi Jokha Lemky alimweleza Makamu wa Rais kuwa kwa mwaka huu mashindano hayo yameshirikisha mikoa 24 ya Tanzania Bara na Visiwani yakiwa na washiriki 653 ambapo 66 ndiyo wameingia fainali.

Alisema pamoja na mafanikio hayo lakini Taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto za kukosekana kwa kompyuta, photocopy, usafiri, scholarship na zawadi kwa washindi jambo ambalo Makamu wa Rais alisema atajitahidi kufanya kazi bega kwa bega na Taasisi hiyo katika kutatua changamoto hizo. Katika mashindano hayo ya kuhifadhi Qur'an Makamu wa Rais alikabidhi zawadi kwa washindi waliohifadhi juzuu tatu hadi 30 ambapo aliyehifadhi juzuu 30 alipata shilingi milioni tano.

Mashindano hayo yalihudhuriwa na waumini mbalimbali wa dini ya kiislam wakiwemo Balozi wa Algeria nchini na wawakilishi wa mabalozi wa Misri, Sudan na Iran.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)