Pages

MAALIM SEIF AHITIMISHA ZIARA YAKE NCHINI MAREKANI

Na Mwandishi wetu Washington 

Makamo wa Kwanza Mstaafu wa Rais wa Zanzibar na Katibu mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), maalim Seif Sharif Hamad, jana alimaliza ziara yake nchini Marekani iliyochukua muda wa wiki moja.
Makamo wa Kwanza Mstaafu wa Rais wa Zanzibar na Katibu mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), maalim Seif Sharif Hamad (Picha na http://swahilivilla.blogspot.com/)

Maalim Seif alikhitimisha ziara yake hiyo kwa mkutano wa hadhara ambapo alipata nafasi ya kuongea na Watanzania waishio nchini humu.

Katika Mkutano huo, mwanasiasa huyo gwiji nchini Tanzania alisema kuwa lengo la ziara yake ni kuuelezea ulimwengu kukhusu kile kilichotokea Zanzibar kufuatia uchaguzi wa Oktoba 25 na mwelekeo wa demokrasia nchini Tanzania kwa ujumla.

Aliielezea ziara yake hiyo nchini Marekani kuwa imezaa matrunda. “Sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kuwa tumeeleweka na ziara yetu imezaa matunda” alisema Maalim Seif.
Sehemu ya hadhira wakimsikiliza kwa makini Maalim Seif

Kukhusiana na zoezi la uchaguzi wa mwaka jana Visiwani Zanzibar, Maalim Seif alisema kuwa, uchaguzi huo ulihudhuriwa na waangalizi wa Kimataifa na wa ndani kutoka pande zote za Muungano, Bara na Zanzibar, na wachunguzi wote hao walithibitisha kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki. “Waangalizi wote, wote kabisa, walikiri kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki”, alisisitiza kiongozi huyo na kuongeza kuwa “Ulikuwa uchaguzi bora kabisa kuliko chaguzi zote zilizotangulia Zanzibar”

Aliuulezea mchakato wa uchaguzi kuwa ulikwenda vizuri mpaka kufikia tarehe 27 Oktoba ambapo jumla ya Majimbo 34 ya uchaguzi yalikuwa tayari yameshatangazwa, na mengine 9 yakiwa yameshahakikiwa ikiwa bado kutangwazwa tu. Na kwa upande wa udiwani na Uwakilishi, uchaguzi ulikuwa umeshakamilika na washindi kupewa shada zao za ushindi.

“Kufika hapo vikashuhudiwa vituko vya Tume ya Uchaguzi khususan Mwenyekiti wake”, alisema Maalim Seif, na kufuatiwa na uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Bwana Jecha Salum Jecha kufuta uchaguzi wote kwa ujumla hapo tarehe 28 Oktoba 2015.

Katibu Mkuu huyo wa CUF na ambaye pia alikuwa mgombea urais wa Zanzibar katika uchaguzi huo, alikielezea kitendo cha Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi kuwa hakikuwa cha kisheria, kilichokiuka taratibu za Tume ya Uchaguzi, na kusisitiza “Kwa kitendo hicho, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi aliingiza nchi katika mgogoro wa Kikatiba”.

Kufuatia mgogoro huo wa Kikatiba, Maalim Seif, mwenye uzoefu wa siasa za Zanzibar, alichukua hatua za kujaribu kutatua mgogoro huo, ambapo moja ya hatua hizo muhimu ni kuwasiliana na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohammed Shein ambaye pia alikuwa akiwania kuchaguliwa kwa kipindi cha pili.

“Niliona mgogoro baada ya kufutwa kwa uchaguzi, na kwa hivyo nikachukua juhudi za kuwasiliana na kiongozi mwenzangu ili kuitoa nchi kutoka kwenye mgogoro”, alifafanua Maalim Seif, na kuendelea kuwa walikubaliana kukutana katika vikao vilivyowajumuisha viongiozi wa Serikali ya Zanzibar ya wakati huo, na wale waliopita.

Mazungumzo kati ya viongozi hao yaliendelea na kufikia jumla ya vikao 8 bila kuzaa matumda, ambapo mada kubwa iliyojadiliwa ilikuwa ni iwapo Mwenyekiti wa Tume alikuwa na haki ya kuufuta uchaguzi. “Kubwa tulilolijadili awali ilikuwa ni iwapo Mwenyekiti wa tume ana haki ya kuchukua uamuzi wa kuufuta uchaguzi”, alielezea Maalim Seif, na kuendelea kuwa “Pili ilikuwa ni kurudiwa kwa uchaguzi, jambo ambalo mimi nililipinga”

Hata hivyo, Maalim Seif alidokeza kuwa hatimaye alikubaliana na wazo la kurudiwa kwa uchaguzi lakini kwa sharti la kusimamiwa na Umoja wa Mataifa, wazo ambalo lilikataliwa. “Niliposhauri uchaguzi urudiwe chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, walikataa”, alisema Maalim Seif.

Katibu Mkuu huyo wa CUF, aliamua kujitoa kwenye mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa Zanzibar baada ya kutangazwa uchaguzi wa marudio bila kufikiwa mwafaka kwenye mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea. “Tuliendelea na vikao mpaka walipoamuru Tume kutangaza marudio ya Uchaguzi”, alidokeza.

Chama cha CUF kiliamua kuususia uchaguzi wa Marudio wa Zanzibar uliofanyika tarehe 20 Machi 2016, uchaguzi ambao wataalamu wa mambo ya kisisasa pamoja na wachunguzi waliohudhuria waliuelezea kuwa haukuwa wa haki, khususan ikizingatiwa kiwango kidogo cha watu waliojitokeza kupiga kura ambacho hakikuzidi asilimia 12 ya watu wote wenye haki ya kupiga kura.

Maalim Seif aliyaelezea yale yaliyotokea baada ya Uchaguzi wa mwaka jana kuwa yameirudisha nyuma Zanzibar na Tanzania kidemokrasia, khususan ikizingatiwa kuwa kabla ya hapo palikuwa na serikali ya Umoja wa Kitaifa Visiwani Zanzibar, kufuatia mwafaka kati yake na Rais Mstaafu wa Zanzibar Dkt Amani Abeid Karume ya mwaka 2009.

Alitahadharisha dhidi ya kauli za Wahafidhina wanaodai kuwa Serikali haiwezi kutolewa kwa vikaratasi, na kuonya kuwa hali hiyo inatuma ujumbe mbaya kwa vijana. “Ikiwa utawanyima vijana nafasi ya kuleta mabadiliko kwa njia ya kura, unawaambia nini? Alihoji Maalim Seif na kuonya “Lazima hii isimame.”

“Haki ya Umma na sauti zao lazima zisikilizwe”, alisisitiza.

Mkutano huo wa Maalim Seif Sharif Hamad ulihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tawi la Diaspora Bwana Kalley Pandukizi.

Maalim Seif yupo nchini Marekani kwa mwaliko wa Taasisi ya Mikakati na Tafiti za Kimataifa ambapo Jumatatu iliyopita alihutubia kwenye Taasisi hiyo. Aidha yeye na ujumbe wake wamepata nafasi ya kukutana na viongozi mbali mbali wa serikali ya Marekani.

Katika juhudi hizo za kutafuta uungaji mkono wa Kimataifa kwa madai ya demokrasia Zanzibar, na Tanzania kwa ujumla, Maalim Seif ambaye anafuatana na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa Chama cha CUF Bwana Ismail Jussa, pia alifika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, ambapo aliielezea ziara yake hiyo kuwa ilikuwa ya ufanisi.

Maalim Seif na ujumbe anaofuatana nao unaomjumuisha pia Mkuu wa Watumishi katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CUF, Bwana Issa Kheir Hussein wanatarajiwa kuondoka leo kuelekea nchini Canada.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)