Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha Chibuku (Darbrew Ltd) wakisoma katiba ya Vicoba
Wafanyakazi wa Kiwanda cha Chibuku (Darbrew Ltd) wakimsikiliza Rais wa Vicoba endelevu Tanzania, Devotha Likokola
Rais wa Vicoba endelevu Tanzania, Devotha Likokola, akitoa mafunzo ya elimu ya vicoba kwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Chibuku (Darbrew Ltd) cha Ubungo jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa Vicoba mkoa wa Dar es Salaam, Amina Mkuwa (kulia) akigawa vipeperushi vya taasisi hiyo wakati wa mafunzo hayo.
Wafanyakazi wa Chibuku (Darbrew Ltd)Ubungo jijini Dar es Salaam, wakiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Vicoba endelevu Devotha Likokola mara baada ya kumalizika kwa mafunzo.
Rais wa VICOBA Devotha Likokola amewaasa wafanyakazi waliopo kwenye ajira hususani wanawake kujiunga na vikundi vya VICOBA ili waweze kujikwamua kimaisha na kuboresha maisha ya familia zao.
Bi.Likokola alitoa wito huu jana wakati wa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake wanaofanya kazi katika kampuni ya DarBrew inayotengeneza kinywaji cha Chibuku iliyofanyika katika kiwanda cha Dar es Salaam.
Alisema kwa kujiunga na VICOBA wanawake hao watakuwa na uwezo wa kupata mikopo yenye masharti nafuu na kupata mafunzo ya fursa mbalimbali za kibiashara zilizopo na kuwakutanisha na wanawake wenzao ili waweze kubadilishana uzoefu wa maisha.
“Kuna dhana kwamba VICOBA ni kwa ajili ya akina mama wasio na ajira na wanawake wengi walioajiriwa kutotaka kujiunga na vikundi hivi kwa ajili ya kuwakwamua kiuchumi matokeo yake waajiriwa wengi wanaachwa nyuma kiuchumi kutokana na kutegemea mshahara wa mwisho wa mwezi tu”.Alisema Likokola.
Aliwaasa wanawake kuchangamkia fursa hii ambayo pia imeanza kuchangamkiwa na wanaume na kuwataka waajiri kuwezesha wafanyakazi wao kupata mafunzo ya ujasiriamali ili yawaandae kujiajiri baada ya muda wao wa ajira kumalizika na hata wakiwa makazini bado kuna shughuli mbalimbali za ujasiriamali wanaweza kuzifanya kwa ajili ya kuinua vipato vyao.
Katika mafunzo hayo wanawake wafanyakazi wa DARBREW walipatiwa mwongozo wa kujiunga na vikundi vya VICOBA ambapo pia walipatiwa elimu ya ujasiriamali,jinsi ya kuibua miradi na kuiendesha pia walipatiwa ushauri wa jinsi ya kutumia fedha kwa malengo ya kufanikiwa na umuhimu wa kujiwekea akiba.
VICOBA ambayo ilianzishwa ikiwa na mtizamo wa kusaidia vikundi vya wanawake wa vijijini kiuchumi imezidi kupanua huduma kwa wanawake wengi nchini ambapo hivi sasa inao mtandao wa vikundi zaidi ya 10,000 nchi nzima vyenye wanachama zaidi ya 500,000 na mtaji unaofikia zaidi ya shilingi bilioni 75
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)