Pages

TBL yafanya uwekezaji unaoendeleza jamii na kuzingatia utunzaji wa mazingira

Richmond akitoa mada

Baadhi ya wajumbe wa semina wakimsikiliza kwa makini

Kampuni ya kutengeneza vinywaji ya TBL Group iliyopo chini ya kampuni mama ya kimataifa ya SABMiller imefanikiwa  kutekeleza mpango wa uzalishaji unaozingatia utunzaji wa mazingira na kunufaisha jamii zilizopo maeneo ilipowekeza  kwa kujenga viwanda vyake.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa kiwanda cha TBL cha Mwanza,Richmond Raymond wakati akitoa mada kwenye semina kuhusu kujenga uchumi na maendeleo endelevu iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Amesema kwa muda mfupi wa utekelezaji wa mpango huo mafanikio yameanza kuonekana na taasisi nyingi zinatembelea kwenye viwanda vyake kwa ajili ya kujifunza.

Akitolea mfano wa kiwanda cha Mwanza ambacho anakiongoza,Richmond alisema uendeshaji wake unafuata mifumo bora na kuhakikisha  jambo lolote linalofanyika linaenda sambamba na malengo yaliyowekwa na kampuni mama ya SABMiller ambayo mtazamo wake unaelekeza kwenye utunzaji wa mazingira , kufanya uzalishaji usio na athari kwa mazingira na kuhakikisha jamii zilizopo maeneo ya kiwanda zinanufaika na uwekezaji.

Richmond alisema kiwanda cha Mwanza katika kuhakikisha  uzalishaji wake hauathiri mazingira kimefunga mitambo inayozalisha nishati ya umeme kwa kutumia pumba za mpunga badala ya mafuta. “Uzalishaji huu mbali na kupunguza gharama za uendeshaji pia umeongeza mapato ya wananchi ambao wanauzia pumba za mchele kiwanda kwa ajili ya kuendeshea mitambo yake wakati siku za nyuma walikuwa wanazitupa”.Alisema
.
Pia alisema TBL inahakikisha inapata malighafi kutoka kwa wazalishaji  wa ndani hususani wakulima wanaoiuzia malighafi ambapo inawawezesha kwa kuwapatia mitaji na utaalamu wa kilimo ili waweze kupata mazao ya kutosha ambayo wanayauza kwa kiwanda  wakati huo huo kuboresha maisha yao.

Alisema  mafanikio ambayo kampuni imepata na mikakati yake ya uwekezaji zaidi nchini katika siku za usoni inazingatia zaidi malengo  ya Kampuni  ya SABMiller yenye mwelekeo wa Maendeleo endelevu na kanuni za pamoja.

Richmond aliyabainisha malengo hayo  kuwa ni ‘dunia yenye  nuru njema,lengo  hili limelenga kuharakisha ukuaji wa kampuni na maendeleo ya kijamii katika mfululizo wake wa maadili.

Alilitaja lengo lingine  kuwa ni ‘kujenga dunia changamfu’ ambalo linalenga kuifanya bia kuwa kinywaji cha asili kwa mnywaji na kuondoa dhana kuwa unywaji wa bia ni ulevi, bali kuhamasisha unywaji  ambao utawezesha kuwepo wanywaji wa wastani  kwenye jamii ambao pia watazingatia kutekeleza majukumu yao.

Aidha alilitaja lengo lingine kuwa ni  ‘kujenga  dunia imara na dunia iliyo safi’ ambalo limelenga kupata raslimali ya pamoja ya maji ya kutosha ambayo yanatumika kwa kiasi kikubwa katika biashara ya kampuni.”Katika kutekelea lengo hili kampuni kwa muda mrefu imekuwa mstari wa mbele  kulinda na kutunza vyanzo vya maji na kuhakikisha maji yanayopatikana yananufaisha jamii ya wananchi inayowazunguka”.

Lengo lingine alilibainisha kuwa  ni kujenga dunia yenye nguvu kazi lengo kubwa likiwa ni kusaidia matumizi bora na endelevu ya ardhi .

Richmond alisema malengo haya ambayo baadhi yake yanashabihiana na malengo endelevu ya Umoja wa Mataifa yanadhihirisha kuwa kampuni ya TBL Group ni kampuni iliyodhamiria kufanya uwekezaji wenye kuleta tija na mabadiliko kwa jamii ya watanzania.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)