Salvatory Rweyemamu:Mhandisi anayependa kufuatilia mabadiliko ya teknolojia - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Salvatory Rweyemamu:Mhandisi anayependa kufuatilia mabadiliko ya teknolojia

Ni Meneja wa Viwanda 2 vya TBL
Ashauri masomo ya sayansi yapewe kipaumbele mashuleni
Wakati mabadiliko ya teknojia yanajitokeza kila siku hadi siku duniani na kubadili mitindo ya maisha na utendaji wa kazi katika sekta na taaluma mbalimbali wapo baadhi ya watu makini ambao wakati wote wamekuwa wakifuatilia mabadiliko hayo ili kuhakikisha hayawaachi nyuma.
Miongoni mwa wafuatiliaji wa mabadiliko ya kiteknolojia na anayeamini kuwa bila kutumia teknolojia za kisasa hususani katika uzalishaji wa viwanda sio rahisi kufanya uzalishaji wenye tija na ufanisi ni Mhandisi Salvatory Rweyemamu ambaye ni Meneja wa Kiwanda cha kuzalisha bia cha TBL cha Arusha na Kiwanda cha kusindika Shayiri cha TBL kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro.

Katika mahojiano hivi karibuni Mhandisi Rweyemamu alisema kuwa pamoja na majukumu mengi ya kazi aliyonayo huwa anahakikisha anasoma mambo mbalimbali kuhusiana na teknolojia mpya zinazoibuka kila kukicha duniani kote ili kuhakikisha anakwenda sambamba na mabadiliko hayo.
“Naipenda taaluma yangu ya uhandisi wa umeme  kwa kiasi kikubwa kiasi kwamba muda wangu mwingi huwa nautumia kusoma mambo mengi yanayohusiana na fani hii kwa kuwa  teknolojia duniani inakuwa kwa kasi kubwa kiasi kwamba ukitaka kuwa mtaalamu na kufanya kazi kwa ufanisi na kwenye kampuni kubwa kama nilipoajiriwa unahitaji kuhakikisha muda wote unakwenda na wakatii hususani kujua mabadiliko ya kiteknolojia yanayotokea kila kukicha”.Alisema
Alisema mara nyingi huwa anawaza ni jinsi gani  wasomi wa fani ya sayansi nchini ni kwa jinsi gani wanaweza kutumia taaluma zao kuleta mabadiliko kwenye jamii na kufanya ubunifu wa kiteknojia badala ya kutegemea ubunifu wa wataalamu wa nje ambao kila  kukicha wanatuletea mambo mapya  ambayo watu wetu wanayatumia na kuyafurahia hata mengine yakiwa sio mazuri.
Mhandisi Rweyemamu alisema kuwa amepata elimu ya juu katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ambako alisomea shahada ya Kwanza ya uhandisi wa umeme na alikuwa miongoni  mwa wahitimu waliofanya vizuri katika mwaka wao wa 1988.
Baada ya kumaliza masomo ya Chuo Kikuu aliajiriwa na Kampuni ya TBL katika kiwanda cha Ilala akiwa kama mhandisi wa umeme.Baada ya kufanya kazi kwa kipindi kifupi alibahatika kupata nafasi ya masomo ya shahada ya uzamili nchini Ujerumani akiwa amejikita zaidi katika uhandisi wa umeme wa viwandani na mitambo inayotumia teknolojia za kisasa.
Baada ya kurejea nchini aliendelea kufanya kazi za uhandisi katika kiwanda cha TBL na  kupandishwa cheo kutokana na ufanisi wake katika kazi mpaka kufikia nafasi aliyonayo akiwa Meneja anayesimamia viwanda viwili.
Mbali na kupata elimu za vyuoni akiwa mwajiriwa wa TBL tayari amehudhuria kozi mbalimbali za ndani ya kampuni  ambazo zimezidi kumpatia maarifa katika fani yake na kumfanya awe miongoni mwa wahandisi nguli wanaoaminika nchini katika fani ya uhandisi wa umeme na uendeshaji wa mitambo ya kisasa.
“TBL kuna mafunzo ya aina nyingi  na kuna mitambo ya kisasa na mara nyingi tumekuwa tukipata mafunzo ya aina mbalimbali  ikiwemo ya mifumo ya uendeshaji viwanda kwa ufanisi mfano ‘SABMiller Manufacturing Way’.  ambayo tunaitumia na imeonyesha mafanikio makubwa  na kufanya viwanda vyetu kuwa na uzalishaji wenye tija kiasi kwamba kila mara tunashinda tunapokea wageni kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza uendeshaji wa viwanda”.Alisema.
Pia alisema kuwa anaweza kufanya kazi zake vizuri kutokana na ushirikiano mzuri anaopata kutoka kwa wafanyakazi wenzake “TBL ni tanuru la kupika wataalamu na imeajiri watu wenye uwezo mkubwa katika fani zao hivyo nafanya kazi na wataalamu ambao wana upeo mkubwa na wanaoelewa nini wanachokifanya bila kuhitaji usimamizi mkubwa.
Kuhusu changamoto anazokumbana nazo katika kazi yake alisema ni za kawaida na kutokana na elimu yake na uzoefu wa kazi alionao anaweza kuzitatua kwa urahisi na maisha kuendela kama kawaida.
Mhandisi Rweyemamu alisema kuwa anajivunia kufanya kazi na kampuni kubwa kama TBL ambayo imemuwezesha kujifunza mambo mengi ikiwemo kupata mafanikio mbalimbali katika maisha yake mojawapo ikiwa ni kuihudumia familia yake vizuri.
Malengo yake ya baadaye baada ya kustaafu kazi ni kujiajiri kwa kufanya kazi za ushauri wa kitaalamu wa fani yake ya Uhandisi umeme ambayo anaamini kuwa inazidi kukua na kuhitaji wataalamu tofauti na ilivyokuwa  miaka ya nyuma.
Rweyemamu anatoa wito kwa vijana wa kitanzania kutokimbia masomo ya hesabu ya sayansi wanapokuwa mashuleni bali wajitahidi kukomaa nayo kwa kuwa  katika dunia hii ya sayansi na teknolojia bila wataalamu katika nyanja hii itakuwa vigumu kwa taifa kupiga hatua ya maendeleo.

Alimalizia kwa kuwaasa vijana kuacha tamaa ya maisha na kuwa wavumivu, kutulia na kuwa tayari kujifunza. “Vijana wengi wa siku hizi wanakuwa sio wavumilivu na wanapanga malengo makubwa ambayo inakuwa vigumu kuyafikia kwa muda mafupi matokeo yake wanajikuta wamejiingiza kwenye vitendo vya wizi wa kuwaibia waajiri wao hali inayosababisha  wasiaminike.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages