Calvin Martin: Meneja wa kiwanda anayeamini kuwa falsafa ya ‘Hapa Kazi’ itakomboa watanzania - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Calvin Martin: Meneja wa kiwanda anayeamini kuwa falsafa ya ‘Hapa Kazi’ itakomboa watanzania

 Calvin Martin akimwonyesha Waziri wa Viwanda na Biashara,Charles Mwijage alipotembelea kiwanda hicho hivi karibuni
Calvin akintembeza Afisa Mwandamizi wa SABMiller Olga Luskotova alipofanya ziara nchini hivi karibuni
Ashauri vijana wasikimbie kilimo na masomo ya sayansi na ufundi.
Wakati nchi yetu inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kupiga hatua kiuchumi na kusababisha wananchi wengi kubaki maskini, wapo baadhi ya watanzania wana maono kuwa Tanzania inazo fursa nyingi za kuondokana na umaskini bali tatizo lililopo ni wananchi wengi kutowajibika ipasavyo hususani katika kufanya kazi wanavyostahili.

Calvin Martin, Meneja wa kiwanda cha kutengeneza Bia cha Tanzania Breweries kilichopo jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa watanzania wanaoamini kuwa nchi yetu inazo fursa nyingi za kuondokana na umaskini, kuboresha  huduma za kijamii na wananchi kuishi maisha mazuri.

Ana imani kuwa falsafa ya ‘Hapa Kazi tu’iliyoanzishwa na Rais wa awamu ya tano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli, ikitekelezwa ipasavyo nchi yetu itapiga  hatua kubwa kiuchumi kwa kuwa upo ushahidi wa baadhi ya mataifa hususani barani Asia ambayo kwa kupitia falsafa kama hii wameweza kupiga hatua kubwa kiuchumi kwa haraka.
 
Katika mahojiano hivi karibuni Calvin alisema kuwa ana imani kuwa mtu yeyote akifanya kazi kwa bidii na maarifa ni lazima afanikiwe katika jambo lolote na imani hiyo imemsaidia  kufanikiwa katika mambo mengi hadi kufikia hatua alipo ya kuwa Meneja wa kiwanda cha kutengenezwa vinywaji chini cha Tanzania Breweries.

“Siku zote naamini kuwa kufanya kazi kwa bidii na ueledi kunaleta mafanikio na huwa nasikitika sana kuona baadhi ya watu hususani vijana ambao wanakaa bila kufanya kazi wakati wana nguvu za kutosha na  nguvu kazi inapotea bure badala ya kushiriki katika uzalishaji kwa manufaa yao na manufaa ya taifa”. Alisema.

Alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuwajengea watanzania mazingira mazuri ya  kufanya kazi ziwe kwa kuajiriwa ama kujiajiri wenyewe na kuongeza kuwa ajira nyingi ziko katika sekta ya kilimo, ufugaji, viwanda na kwenye ufundi wa aina mbalimbali.
Calvin alisema kuwa amepata elimu ya juu katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ambako alisomea shahada ya kwanza ya  Sayansi na alikuwa miongoni  mwa wahitimu waliofanya vizuri katika mwaka 1993
 
Baada ya kumaliza masomo ya  Shahada ya kwanza Chuo Kikuu, alijiunga na masomo ya Shahada ya uzamili chuoni hapo akijikita zaidi katika Sayansi ya viwanda na utawala ambako alihitimu mwaka 1997.
Ajira yake ya kwanza ilikuwa katika kampuni ya East Africa Breweries ambako alikuwa kwenye kitengo cha uzalishaji na kwa muda mfupi aliweza kuielewa fani ya uzalishaji bia kwa vitendo na nadharia, kuhitimu Stashahada ya utengenezaji bia (Diploma in Brewing) ya Uingereza na baada ya kufanya kazi na kampuni hiyo kwa miaka mitatu na nusu aliamua kujiunga na kampuni anayofanyia kazi kwa sasa hivi ya TBL Group.
Akiwa na kampuni hii ameweza kushika nyadhifa mbalimbali  hadi kufikia nafasi aliyonayo hivi saa ya kusimamia kiwanda kikubwa cha TBL Cha Dar es salaam. Moja ya kazi kubwa anazojivunia nazo ndani ya kampuni hiyo ni kusimamia ujenzi na uanzishwaji wa kiwanda cha Mbeya.
“Kazi ya kuanzisha kiwanda hiki ilikuwa moja ya changamoto ya kikazi kwangu  lakini kutokana na ujuzi na uzoefu kwa kushirikiana na wenzangu tulifanikiwa na najivunia kuona kiwanda hiki ni moja ya viwanda vya kampuni vinavyofanya vizuri kikiwa chini ya uongozi na wafanyakazi watanzania.
Mbali na kupata elimu za vyuoni akiwa mwajiriwa wa TBL tayari  Calvin amehudhuria kozi mbalimbali ndani ya kampuni  ndani na nje ya nchi ambazo zimezidi kumpatia maarifa ya kitaalamu, kiufundi, utawala, uendeshaji na usimamiaji wa viwanda kwa ufanisi.
“TBL kuna mafunzo ya aina nyingi  na kuna mitambo ya kisasa na mara nyingi tumekuwa tukipata mafunzo ya aina mbalimbali  ikiwemo ya mifumo ya uendeshaji viwanda kwa ufanisi mfano ‘SABMiller Manufacturing Way’ ambayo tunaitumia na imeonyesha mafanikio makubwa.
Pia alisema kuna mafunzo ya  utawala na mifumo mbalimbali inayowawezesha Mameneja wa viwanda na wakuu wa vitengo kuendesha shughuli zao vizuri wakiwa wanajua jinsi ya kutoa vipaumbele kwenye mambo mbalimbali na mpangilio mzuri wa ratiba za kazi.
Calvin aliongeza kusema kuwa anaweza kufanya kazi zake vizuri kutokana na ushirikiano mzuri anaopata kutoka kwa wafanyakazi wenzake “TBL ni tanuru la kupika wataalamu na imeajiri watu wenye uwezo mkubwa katika fani zao hivyo nafanya kazi na wataalamu ambao wana upeo mkubwa na wanaoelewa nini wanachokifanya, wanaojituma bila kuhitaji usimamizi mkubwa.
Kuhusu changamoto anazokumbana nazo katika kazi yake alisema ni za kawaida na kutokana na elimu yake na uzoefu wa kazi alionao anaweza kuzitatua kwa urahisi na maisha kuendela kama kawaida.
Anasema  anajivunia kufanya kazi na kampuni kubwa kama TBL Group ambayo imemuwezesha kujifunza mambo mengi ikiwemo kupata mafanikio mbalimbali katika maisha yake mojawapo ikiwa ni kuihudumia familia yake vizuri.

 Alimalizia kwa kutoa wito kwa vijana wa kitanzania kutokimbia masomo ya hesabu na sayansi wanapokuwa mashuleni bali wajitahidi kukomaa nayo kwa kuwa  katika dunia hii ya sayansi na teknolojia bila wataalamu katika nyanja hii itakuwa vigumu kwa taifa kupiga hatua ya maendeleo na muda wote wajue kuwa mafanikio yanapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages