Machi 22 2016 Dar es Salaam: Kampuni ya Tigo
Tanzania imetoa msaada wa madawati 500 yenye thamani ya shilingi milioni 82.5 kwenye shule kumi za msingi katika mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni mchango wa kampuni hiyo katika kuisaidia serikali kukabiliana na upungufu wa madawati katika shule za msingi nchini.
Akizungumza leo katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Shule ya Msingi Kawawa iliyopo katika kata ya Mabibo katika manispaa ya
Kinondoni, Mkurugenzi Mkuu wa Tigo Diego Gutierrez amesema mchango huo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya kampuni hiyo ya kuunga mkono jitihada mbalimbali za kuleta maendeleo nchini.
“Mchango huu ni sehemu ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Tigo katika kusaidia utekelezaji wa miradi yenye tija kubwa kwa jamii. Tunaamini kwamba kupitia msaada huu, Tigo inatoa mchango wake katika kujenga viongozi wa baadaye wa taifa hili na wanataluuma mbalimbali wakiwamo madaktari, wahandisi na wengineo, "amesema Gutierrez.
Gutierrez amesema mwaka jana Tigo ilikabidhi msaada kama huo wa madawati katika shule za msingi katika mikoa ya Shinyanga, Mbeya Iringa na Morogoro na kuongeza kwamba kampuni hiyo itaendelea
kutoa madawati zaidi sehemu mbalimbali nchini siku za zijazo.
Makabidhiano yalihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ambaye alisema madawati hayo 500 yataboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto katika Mkoa wa Dar es Salaam na kutoa wito
kwa wadau wengine kuunga mkono zoezi hilo.
“Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa kampuni ya Tigo kwa kuwa mdau muhimu kwetu katika jitihada zinazoendelea za kujaribu kupunguza tatizo la ukosefu wa madawati ya kutosha katika shule za msingi za mkoa wetu wa Dar es Salaam. Ni dhahiri kwamba msaada huu wa madawati 500 yatawawezesha mamia ya wanafunzi wetu kupata sehemu za kukaa na hivyo kujipatia elimu zao katika mazingira bora zaidi,” alisema Makonda.
|
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)