Mahakama ya Wilaya ya Bariadi imewahukumu watu wanne, mmoja kifungo cha miaka 20 jela na watatu miaka 15 kila mmoja waliostakiwa kuwa kutungua helikopta kwenye Pori la akiba Maswa wilayani Meatu na kusababisha kifo cha rubani wake baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na silaha.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mfawidhi wa Wilaya hiyo, Mary Mrio alisema anawapa adhabu hiyo washtakiwa hao baada ya kukiri kosa la kukutwa na silaha hiyo kinyume cha sheria na hivyo kutoisumbua mahakama.
Katika hukumu hiyo, Njile Gunga ambaye anadaiwa kutungua ndege hiyo Januari 29 atatumikia kifungo cha miaka 20, huku akisubiri kesi nyingine mbili ya mauaji ya rubani huyo na uhujumu uchumi ambazo zitatajwa Mahakama ya Mkoa wa Simiyu.
Juzi washtakiwa hao, Shija Mjika, Dotto Pangani, Njile Ngunga na Moses Mandagu, walikiri kukutwa na silaha, lakini Hakimu Mrio hakuweza kutoa hukumu kwa kuwa ushahidi ulikuwa haujawasilishwa mahakamani. Baada ya kuwasilishwa ushahidi huo jana, alitoa hukumu hiyo ambayo inatokana na mashtaka matano dhidi yao.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Yamiko Mlekano alitaja makosa hayo kuwa ni kumiliki na kukutwa na silaha kinyume cha sheria.
Shtaka la tatu ni kukamatwa na risasi tano za bunduki aina ya rifle, shtaka ambalo Pangali na Gunga walikiri.
Katika shtaka la nne linalowakabili washtakiwa wote wanne, Wakili Mlekano alidai ni umiliki risasi kinyume cha sheria, ambazo walikamatwa nazo Februari 8 na bunduki aina ya Rifle 303.
Washtakiwa hao waliomba kupunguziwa adhabu kwa kile walidai ni mara yao ya kwanza kutenda makosa kama hayo, lakini Mlekano aliomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
Hakimu Mrio alisema kwa kosa la kwanza, pili na nne mahakama inawahukumu kifungo cha miaka mitano jela kila mmoja, kosa la tatu miaka mitano au kulipa faini ya Sh10 milioni.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)