MADEREVA DALADALA JIJINI MWANZA WATISHIA KUGOMA IKIWA MAJIPU YA TAX BUBU HAYATATUMBULIWA. - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MADEREVA DALADALA JIJINI MWANZA WATISHIA KUGOMA IKIWA MAJIPU YA TAX BUBU HAYATATUMBULIWA.

Ridhione Senga (wa pili kushoto) ambae ni Mwenyekiti wa Madereva wa Daladala wanaofanya shughuli zao katika barabara ya Bugarika-Mzunguko Jijini Mwanza, jana akilalamikia suala la uwepo wa tax bubu linalowasumbua katika shughuli zao.

Alisema licha ya madereva wa tax bubu wanaobeba abiria kama daladala katika eneo wanalofanyia kazi hususani kubeba abiria wanaoenda na kutoka katika hospitali ya Rufaa ya Bugando kuzuiliwa, bado madereva hao wa tax bubu wameendelea na biashara hiyo kama kawaida.

Senga alibainisha kwamba hatua hiyo inawaweka katika wakati mgumu katika kutimiza majukumu yao kutokana na kupata hasara kila kukicha ambapo amesema ikiwa itaendelea wataitisha mgomo ili kushinikiza kilio chao kufanyiwa kazi.

"Sisi tunalipa mapato, lakini jambo la ajabu hawa madereva wa tax bubu ambao hawana leseni ya kubeba abiria wamekuwa ndio wanafanya kazi ya daladala licha ya kupigwa marufuku katika kikao tulichokaa ijumaa iliyopita baina ya Sumatra, halmashauri ya Jiji, Polisi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza pamoja na wawakilishi wengine bila kuwasahau viongozi wa daladala na tax. Kama hali hii itaendelea tutafanya mgomo hapa na hakuna huduma yoyote ya kubeba abiria itakayotolewa".Alisema Senga.

Ramadhan Idd ambae ni Kaimu Mwenyekiti wa Madereva wa daladala za Bugarika-Muzunguko Jijini Mwanza aliunga mkono hoja ya mwenyekiti huyo na kusema kuwa ikiwa mamlaka husika zitashindwa kutatua suala la tax bubu katika eneo hilo, wao watachukua hatua ya kusitisha huduma ya usafirishaji katika barabara hiyo ya Bugarika-Buzuruga.

"Hizi tax bubu tunasikia ni za wakubwa na ndiyo maana hawa madereva wanaoziendesha wana jeuri mno. Sisi tunasema haya ni majipu na tunawaomba viongozi wengine wakubwa akiwemo Mhe.Magufuli, waangalie huku Jijini Mwanza maana kuna majipu makubwa ya kutumbua".Alisema Athuman Bin Malick ambae ni mmoja wa madereva wa daladala za Bugarika-Mzunguko Jijini Mwanza.

Kaptaini Michael Rogers ambae ni Afisa Mfawidhi wa Sumatra Mkoani Mwanza, ameshauri suala hilo kutatuliwa na jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani kwa kuwa ndilo lenye jukumu la kukamata vyombo vya usafiri vinavyofanya kazi kwa kukiuka sheria na taratibu zilizoweka na mamlaka husika ikiwemo halmashauri ya Jiji Mwanza ambayo ndiyo inasimamia taratibu la utendaji kazi wa tax.

Juhudi za kuwatafuta madereva wa tax hizo zinazodaiwa kufanya kazi kinyume cha sheria (tax bubu) bado zinaendelea ili kujua kuzungumzia malalamiko yanayowakabiri.
Ramadhan Idd ambae ni Kaimu Mwenyekiti wa Madereva wa daladala za Bugarika-Muzunguko akitoa malalamiko yake.
Athuman Bin Malick ambae ni mmoja wa madereva wa daladala za Bugarika-Mzunguko Jijini Mwanza.
Kulia ni Kaptaini Michael Rogers ambae ni Afisa Mfawidhi wa Sumatra Mkoani Mwanza akitoa ufafanuzi wake.Imeandaliwa na George Binagi-GB Pazzo

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages