Pages

Mwajuma Ally Ramadhan: Dereva na mhudumu wa ofisi kampuni ya TBL

 Mwajuma akiwa kazini.

Asema netiboli imemwezesha kupata ajira.
Mwajuma Ally Ramadhan,dereva ni mhudumu wa ofisi katika kampuni ya  TBL  kiwanda cha Arusha na anasema kuwa anaifurahia kazi yake na anatoa ushauri kwa wanawake wenzake kupambana na maisha na kutokata tamaa.

“Maisha siku zote sio lelemama kinachotakiwa ni kupambana , kutokata tamaa,kuwa na malengo,na kuchukia kuishi maisha ya utegemezi wakati nguvu na akili za kufanya kazi unazo”.Anasema Mwajuma.

Mwajuma anatoa ushauri kwa wazazi kutowadekeza watoto hasa wa kike ili wakiwa watu wazima wawe na uwezo wa kujimudu kufanya kazi mbalimbali zinazowawezesha kujipatia kipato na kuendesha vizuri maisha yao.

Akielezea historia yake yake ya kazi alisema kuwa tangu alipokuwa na umri mdogo alikuwa anapenda sana kuwa mwanamichezo na alipokuwa anasoma shule ya msingi Wilayani Handeni mkoani Tanga alishiriki kucheza mchezo wa netiboli katika timu ya shule na aliendelea kucheza  mchezo huo hata alipokuwa anasoma sekondari.

“Mchezo wa netiboli ndio umenifikisha hapa nilipo kwa kuwa nilijiunga na kampuni ya TBL mwaka 1988 nikiwa mchezaji wa netiboli kwenye timu ya kampuni ambapo baadaye ndipo niliajiriwa kama mhudumu wa ofisi “.Anasema.

Mwajuma alisema baada ya kufanya kazi ya uhudumu wa ofisi kwa muda mrefu aliamua kujifunza kozi ya udereva katika chuo cha Kilimanjaro Driving School ambapo alifuzu na kuweza kupata leseni ya kuendesha magari madogo.

Baada ya kupata leseni mwajiri wake aliweza kumpandisha daraja kuwa dereva wakati huohuo akifanya kazi ya uhudumu “Hivi sasa naendesha magari ya kampuni na naaminika kufanya kazi mbalimbali ikiwemo kupokea wageni wa kampuni  na kuwazungusha kwenye ziara za kazi,naifurahia kazi yangu na kuipenda na nina mabosi wanaotoa ushirikiano ambao mara zote hunitia moyo na kuniongoza”.Anasema.

Kuhusu changamoto anazokabiliana nazo katika kazi yake alisema zipo changamoto za kawaida kama zilizopo kwenye kazi nyingine . “Wakati mwingine hujitokeza hitilafu kwenye gari au kupata pancha inakuwa shida kurekebisha hali hiyo au wakati mwingine unapokuwa kwenye mizunguko ya kikazi unajikuta unafanya kazi masaa mengi na kuwa na muda mchache wa kukaa na familia.

Mwajuma ambaye ni mama mwenye watoto  anasema kuwa anafurahi kufanya kazi katika kampuni kubwa ya TBL kwa kuwa ina mifumo mizuri ya ajira yenye maslahi mazuri ikiwemo taratibu za kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara wafanyakazi wake  na anakiri kuwa ajira yake imemwezesha kujua mambo mengi na kupata mafanikio kimaisha.

Kuhusu mipago yake ya baadaye alisema kuwa anatamani kujifunza kuendesha magari makubwa  na alimalizia kwa kuwataka akina mama wajitokeze na kujiamini kufanya kazi zote bila kuchagua kwa kuwa hakuna kazi kwa ajili ya wanaume peke yao au wanawake peke yao.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)