Mwajuma akiwa kazini.
Asema
netiboli imemwezesha kupata ajira.
Mwajuma Ally Ramadhan,dereva ni mhudumu wa ofisi katika
kampuni ya TBL kiwanda cha Arusha na anasema kuwa
anaifurahia kazi yake na anatoa ushauri kwa wanawake wenzake kupambana na
maisha na kutokata tamaa.
“Maisha siku zote sio lelemama kinachotakiwa ni kupambana ,
kutokata tamaa,kuwa na malengo,na kuchukia kuishi maisha ya utegemezi wakati
nguvu na akili za kufanya kazi unazo”.Anasema Mwajuma.
Mwajuma anatoa ushauri kwa wazazi kutowadekeza watoto hasa wa
kike ili wakiwa watu wazima wawe na uwezo wa kujimudu kufanya kazi mbalimbali
zinazowawezesha kujipatia kipato na kuendesha vizuri maisha yao.
Akielezea historia yake yake ya kazi alisema kuwa tangu
alipokuwa na umri mdogo alikuwa anapenda sana kuwa mwanamichezo na alipokuwa
anasoma shule ya msingi Wilayani Handeni mkoani Tanga alishiriki kucheza mchezo
wa netiboli katika timu ya shule na aliendelea kucheza mchezo huo hata alipokuwa anasoma sekondari.
“Mchezo wa netiboli ndio umenifikisha hapa nilipo kwa kuwa
nilijiunga na kampuni ya TBL mwaka 1988 nikiwa mchezaji wa netiboli kwenye timu
ya kampuni ambapo baadaye ndipo niliajiriwa kama mhudumu wa ofisi “.Anasema.
Mwajuma alisema baada ya kufanya kazi ya uhudumu wa ofisi kwa
muda mrefu aliamua kujifunza kozi ya udereva katika chuo cha Kilimanjaro
Driving School ambapo alifuzu na kuweza kupata leseni ya kuendesha magari
madogo.
Baada ya kupata leseni mwajiri wake aliweza kumpandisha
daraja kuwa dereva wakati huohuo akifanya kazi ya uhudumu “Hivi sasa naendesha
magari ya kampuni na naaminika kufanya kazi mbalimbali ikiwemo kupokea wageni
wa kampuni na kuwazungusha kwenye ziara
za kazi,naifurahia kazi yangu na kuipenda na nina mabosi wanaotoa ushirikiano
ambao mara zote hunitia moyo na kuniongoza”.Anasema.
Kuhusu changamoto anazokabiliana nazo katika kazi yake
alisema zipo changamoto za kawaida kama zilizopo kwenye kazi nyingine . “Wakati
mwingine hujitokeza hitilafu kwenye gari au kupata pancha inakuwa shida
kurekebisha hali hiyo au wakati mwingine unapokuwa kwenye mizunguko ya kikazi
unajikuta unafanya kazi masaa mengi na kuwa na muda mchache wa kukaa na
familia.
Mwajuma ambaye ni mama mwenye watoto anasema kuwa anafurahi kufanya kazi katika
kampuni kubwa ya TBL kwa kuwa ina mifumo mizuri ya ajira yenye maslahi mazuri
ikiwemo taratibu za kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara wafanyakazi wake na anakiri kuwa ajira yake imemwezesha kujua
mambo mengi na kupata mafanikio kimaisha.
Kuhusu mipago yake ya baadaye alisema kuwa anatamani
kujifunza kuendesha magari makubwa na
alimalizia kwa kuwataka akina mama wajitokeze na kujiamini kufanya kazi zote
bila kuchagua kwa kuwa hakuna kazi kwa ajili ya wanaume peke yao au wanawake
peke yao.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)