Beka Ibrozama aachia video ya cover ya wimbo ‘Hello’ wa Adele - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Beka Ibrozama aachia video ya cover ya wimbo ‘Hello’ wa Adele


Muimbaji mahiri wa nchini Tanzania, Beka Ibrozama ameachia video ya cover ya wimbo maarufu wa msanii wa Uingereza, Adele ‘Hello’ uliopo kwenye albamu yake 25 iliyotoka November 20 mwaka jana.

Hello umekuwa wimbo maarufu zaidi kutoka mwaka 2015 huku hadi sasa video yake ikiwa imeangaliwa kwa zaidi ya mara milioni 940 kwenye mtandao wa Youtube huku albamu yake ‘25’ ikiuza nakala milioni 7.4 ndani ya sita tu nchini Marekani.

 Hello umekuwa wimbo uliofanyiwa cover nyingi zaidi hadi sasa na wasanii kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo wakongwe kama vile Joe Thomas, Celine Dion, Demi Lovato na wengine. 

Beka anadai aliamua kuwa mmoja wa waimbaji waliofanya cover za wimbo huo ili kuwaonesha wapenzi wa muziki duniani uwezo mkubwa alionao kiuimbaji.

“Ni wimbo fulani mgumu sana, ni wimbo wenye sauti za juu, una melody nzuri na ili uweze kupita kwenye hizo njia ni lazima kidogo uwe unajua muziki,” anasema Beka.

Anasema pamoja Hello kuwa na sauti ngumu kuweza kuzimudu, alipata tabu katika kuweza kutamka vizuri matamshi ya Kiingereza kutokana na kuwa lugha asiyoijua kabisa.

“Ukweli uko hivyo kwamba sijui Kiingereza lakini nimeimba wimbo wa Kiingereza kwa uwezo wangu naamini nimefanya kwa uwezo mkubwa ukizingatia kuwa sijui hata nilichokuwa nakiimba, naamini ni kipaji cha ajabu sana Mungu amenipa,” anasisitiza.

“Kwahiyo watu hata wakisikia baadhi ya maneno sijayatamka kama Muingereza mwenyewe anavyoyatamka, wajue kuwe sijui hicho kitu ila nimejitahidi kwa uwezo wangu.”

Msanii huyo ambaye kwa sasa hupenda kujiita Fundi, anadai kuwa jina hilo amepewa kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa kuchezea sauti kama anavyotaka na uwezo wa kuimba aina zote za muziki kwa umahiri mkubwa.

“Nina vitu vingi sana vikubwa watu hawajavigundua kutoka kwangu.”

Amesema mwaka 2016 utakuwa mwaka muhimu kwake sababu amedhamiria kuuthibitishia ulimwengu kuwa yeye ni dhahabu iliyoanguka kwenye tope na inahitaji sikio la mtu anayejua muziki kuiona, kuikota na kuiutumia vyema ili kuitangaza Tanzania kwa kipaji kikubwa alichobarikiwa na mwenyezi Mungu.

Beka alijipatia umaarufu mkubwa kwa wimbo wake ‘Natumaini Remix’ aliouandika kwa ufundi mkubwa huku akitumia kuunganisha mantiki wa wimbo huo kwa kutumia majina na nyimbo za wasanii mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages