Mgeni rasmi wa katika Kongamano hilo Mhe. Getrude Mongella akiwa na baadhi ya wabunge wanawake wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania wakiimba nyimbo mbalimbali.
kundi la ngoma za kiasili kutoka mkoani Dodoma tayari kwa kutumbuiza katika kongamano hilo.
Wanawake wagombea waweka mikakati ya kushinda udiwani na ubunge 2015
Kwa Mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka
2012, Idadi ya Watanzania sasa imefikia milioni 44.9 huku wanawake wakiwa ni
asilimia 51.3 ilihali wanaume ni asilimia 48.7. Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ya Mwaka 1977 inabainisha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni
ya kidemokrasia, ya kidunia ambayo inaendeshwa kwa misingi ya kidemokrasia na
haki ya kijamii. Ibara ya
8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatamka wazi kwamba nchi hii ni
nchi ya kidemokrasia na haki za kijamii.
Akidi nzima ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni Wabunge 357 kwa mujibu wa Katiba. Hata hivyo viti maalum pekee ni 102 (28.6%)
vilivyogawanywa miongoni mwa vyama vya siasa kwa kuzingatia matokeo yao ya
uchaguzi, kati ya viti 239 vya majimbo (vikiwemo kutoka Zanzibar), ni wanawake 21 tu (8.8%) ndio walipata viti
vya kuchaguliwa bungeni. Idadi ya madiwani wa kuchaguliwa asilimia 4, Wenyeviti
wa Vijiji Asilimia 2, Wenyeviti wa Mitaa ni asilimia 12 wakati Wenyeviti wa Vitongoji ni asilimia
3tu!!.
Pengo hili la ushiriki wa Wanawake katika nafasi
za uongozi zimepelekea asasi za kiraia kuendeleza harakati za kudai
ushirikishwaji sawa au usawa katika vyombo vya uawakilishi kati ya Wanawake na wanaume. Kama
sehemu ya kuendeleza mapamabno ya kudai ushiriki wa Wanawake kwenye uongozi,
ActionAid Tanzania kwa kushirikiana na TGNP Mtandao waliandaa Kongamano la
Wanawake wagombea kwa nafasi zote za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu
2015 kuanzia tarehe 14 hadi 15 Juni 2015 lililofanyika mjini Dodoma, ambapo wagombea
Wanawake, vijana na watu wanaoishi na ulemavu zaidi ya 200 walikutana na
kujadiliana kwa pamoja changamoto wanazokumbana nazo katika harakati za
kutafuta ushindi. Waliokutana ni Wanawake , vijana na walemavu walioonesha nia
ya kuomba ridhaa ya vyama vyao ili wawe viongozi.
Katika kongamano hilo la aina yake viongozi/wabunge na viongozi wastaafu Wanawake ambao wamekuwa madarakani
kwa muda mrefu na kupambana na changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili
Wanawake katika nafasi za uongozi waliweza kushiriki na kutoa ushauri kwa waonesha nia hao.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Meneja
wa Haki za Wanawake kutoka ActionAid
Scholasitica Haule alisema jinsi mchakato ulivyo na kasi kubwa ni lazima
makundi yote yawe makini na vyama vya siasa navyo viangalie nyuma ili
kuhakikisha kila anayestahili kuwa kwenye kasi ya mchakato anapata nafasi.
“tunajua mchakato
wa uchaguzi mkuu unakwenda kwa kasi sasa, tunavitaka Vyama vya siasa vioneshe
kwa vitendo nia ya kujenga demokrasia ya ushindani kwanza kwa kuonesha
mabadiliko ndani ya uongozi wa vyama. Vyama vya siasa sharti viwe mstari wa
mbele kwenye kuonesha kwa vitendo dhana wanazosimamia, kama vile demokrasia,
utawala bora na wa sheria. Kwa mantiki hii, sharti mifumo iliyoko ndani ya
vyama pamoja na taratibu zake zijengeke kwenye misingi shirikishi, ya
kidemokrasia isiyowabagua wanawake au makundi mengine yaliyoko pembezoni”
alisema Haule
Naye Mkuu wa wilaya ya Chamwino Farida Mgomi, aliyekuwa mgeni wa
heshima katika ufunguzi wa Kongamano hilo, aliwataka Wanawake walionesha nia ya kugombea uongozi
kutokukata tamaa wala kuogopa.
“msiogope, masikate tamaa, simameni imara ili kuhakikisha mnashinda, wanawake walipata
fursa wamefanya vizuri na sote tumneona,
na hata wao ukiwauliza wanakuambia kwamba wamekumbana na changamoto
nyingi lakini wamefanikiwa, jambo la msingi ni kuwa na msimamo, kutaa kwa dhati
rushwa, matumizi makubwa ya fedha kwenye
uchaguzi ili mnakundi yote hasa
wanawake, vijana na wanaoishi na ulemavu waweze kushiriki na kufanikiwa”
alisema DC Mgomi.
Alieleza kwamba Ili kuwapa fursa wanawake, vijana na watu wanaoishi
na ulemavu washinde katika uchaguzi huu ni lazima Jamii nzima iunganishe nguvu
katika kudai vyama vya siasa vizingatie usawa wa
kijinsia katika kupendekeza majina ya wagombea, kuwawezesha kifedha na kuwaunga
mkono ili washinde.
Pia Mkuu huyo wa wilaya alivitaka Vyama
vya siasa vitoe fursa za pekee kwa wagombea wanawake katika kutumia vyombo vya
habari vyote kutangaza habari za
uchaguzi kwa kuzingatia usawa wa kijinsia bila kujali itikadi na kuweka
taratibu za kuwezesha watu wenye ulemavu washiriki kikamilifu katika uchaguzi
kama wapiga kura na kama wagombea uongozi katika nyadhifa mbalimbali.
Balozi Mstaafu na aliyekuwa Rais
wa Bunge la Afrika Dk. Getrude Mongela ambaye aliwafunda Wanawake hao namna ya
kuwa viongozi bora na mbinu za kushinda uchaguzi alisema kwamba, Wanawake wanatakia kujenga hoja na kubeba
ajenda za msingi za wananchi wote bila kuwabagua na sio kushambulia wanasiasa
wengine majukaani.
Aidha Mongela aliwataka Wanawake
kuhakikisha kwamba wao wenyewe wanaunganisha nguvu bila kujali itikadi zao za
kichama, kuvua tofauti zao wanapokutana ili kuwa na ajenda moya ya kuhakikisha
Wanawake wenye uwezo wanashinda na wanabeba ajenda ya wananchi wote.
“Tukishaanza mipango ya kujigawa kwa
itikadi zetu, hatuwezi kushinda, ninawataka
kuunganisha nguvu pamoja na kuhamkikisha hakuna anayeachwa nyuma, lakini
tusijenge chuki za kivyama, achana na chama, sema ni mwanamke kwanza, halafu
mengine ya vyama yatakuja baadaye, hapo tutaona mabadiliko” alisema Dk. Mongela
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)