Mtaalamu wa masuala ya vyombo vya habari jamii na Mkufunzi Bi Rose Haji Mwalimu (aliyesimama) wakati wa ufunguzi kijiji cha Usagara, wilayani Misungwi mkoani Mwanza hivi karibuni.
Na Modewjiblog team, Mwanza
Tabia ya watu kukwepa kutoa ushahidi mahakamani ni sababu mojawapo ya wahalifu wa mauaji ya albino kutotiwa hatiani na kuachiwa huru.
Hayo yameelezwa katika warsha zilizoendeshwa mfululizo wilayani Misungwi, Kahama na Bariadi za ushirikishwaji wa jamii katika kuzuia na kutokomeza ukatili, unyanyasaji na unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism) nchini.
Wakichangia mada kuhusu changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu wa ngozi, washiriki wamesema kwamba imekuwa ni kawaida kwa watu kutokuwa tayari kutoa ushahidi mara wanapoitwa mahakamani kwa sababu zisizokuwa na mashiko.
Sababu hizo ni kuogopa kuuawa na wahusika na shinikizo kutoka kwa wanafamilia.
“Mara nyingi tumeshuhudia watu wanaoitwa mahakamani kutoa ushahidi hawaendi siku kesi inaposikilizwa hata kama aliandikiwa na mahakama kufanya hivyo, wengine huamua kuhama kabisa eneo analoishi kwa kukwepa lawama kutoka kwa jamii au familia na kuogopa kuuawa baada ya kugundulika kuwa katoa ushahidi,” alisema mmoja wa washiriki.
Kuachiwa kwa watuhumiwa wanaodaiwa kuhusika na ukatili hususan kukatwa viungo na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi kumezua mjadala mkubwa katika jamii kwamba jeshi la polisi haliwajibiki kikamilifu au kuhisiwa kuwa na ushirikiano wa namna fulani na watuhumiwa hao.
Afisa mtetezi na ushawishi kutoka shirika linaloshughulika na watu wenye Albinism la Under The Same Sun (UTSS), Kondo Seif akisisitiza jambo kwa washiriki katika warsha ya siku tatu iliyofanyika katika kijiji cha Nyakasungwa wilayani Sengerema mkoani Mwanza hivi karibuni.
“Mtuhumiwa anapoachiwa huru wanajamii wanaona kama polisi imepewa rushwa kuwachia, hawaelewi kwamba wao wenyewe wameshiriki kwa mtuhumiwa huyo kuwa huru kwa sababu hawana ujasiri wa kujitokeza mahakamani kama walivyoweza kutoa maelezo ya awali kwa polisi,” wamedai washiriki hao.
Tanzania imekumbwa na wimbi kubwa la ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu jambo ambalo limelitia doa taifa.
Kwa mujibu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa Mashambulizi hayo ambayo yanahusishwa na matumizi ya viungo vya miili ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa imani za kishirikina yamepoteza maisha ya watu wapatao 73 wenye ulemavu huo nchini kuanzia mwaka 2000.
“Huku kwetu imani za kishirikina zimeenea na waganga wa jadi ni wengi sana. Ni kawaida kabisa kwa mtu wa sehemu hizi kwenda kwa mganga wa kienyeji ili apigiwe ramli endapo kuna mtoto mgonjwa au kifo kimetokea katika kaya badala ya kwenda kituo cha afya,” alisema Bahame Maduhu, mwenyekiti Kata ya Nkololo wilayani Bariadi.
Maduhu amesema kwamba watu wajanja wamechukua udhaifu wa wanajamii kutoka kanda ya Ziwa kuamini ushirikina kiasi kwamba waganga wengine wenye tamaa za kutajirika kutoka sehemu mbalimbali za nchi wamehamia katika ukanda huo.
Washiriki wakiandaa mpango kazi kwa ajili ya utekelezaji ili kudhibiti ukatili dhidi ya ukatili ya watu wenye ulemavu wa ngozi katika kijiji cha Nkololo, Kata ya Nkololo wilayani Bariadi.
“Waganga hasa wanaotumia ramli na mapepo machafu ndio wenye kuendesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ili kukamilisha huduma za wateja wao ambao hutaka utajiri, kuchimba madini, uvuvi na biashara nyingine, alieleza mwenyekiti huyo.
Kuzorota kwa hali ya usalama kwa watu wenye ulemavu wa ngozi serikali ililazimika kuwahamishia katika vituo maalum kwa ajili ya ulinzi.
Hata hivyo kwa sababu za msongamano hali ya vituo hivyo imezorota kutokana na kukosekana kwa huduma muhimu hususan za afya, chakula, mavazi na malazi .
Vituo hivyo ni Mitindo, Misungwi mkoani Mwanza, Buhangija mkoani Shinyanga, Kabanga mkoani Kigoma na Shule ya Msingi Pongwe mkoani Tanga.
Hadi sasa ni vigumu kuelewa sababu za ukatili huo lakini kwa mujibu wa washiriki wa warsha hizo utamaduni uliojenga imani za ushirikina zilizoota mizizi katika jamii, elimu duni, biashara za uvuvi, uchimbaji wa madini, utapeli uliojipenyeza katika tiba asili na unyanyapaa zimetajwa kuwa miongoni mwa chanzo cha ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Hali hii imelisukuma Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuandaa warsha nne mfululizo zilizowakusanya wanajamii 160 kutoka vijiji 12 zenye lengo ya kubaini matatizo na kutafuta suluhisho katika jamii kwa kuihusisha jamii yenyewe katika kupambana na ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Miongoni mwa walioshirikiana na UNESCO kutoa elimu hiyo ni wataalamu kutoka Shirika la Serikali la Haki za Binadamu (CHRAGG), Baraza la Tiba Asili Muhimbili na shirika la kimataifa linaloshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu wa ngozi ‘Under The Same Sun’ (UTSS).
Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza ilitoa vijiji vitatu ambavyo ni Nyanzenda, Nyakalilo na Nyakasungwa; Mwanza kijiji cha Luchili, Idetemya na Fela. Wilaya ya Bariadi ilishirikisha kijiji cha Nkololo, Nkindwabiye na Gasuma wakati Msalala ilitoa vijiji vitatu ambavyo ni Ndala, Busungo na Chela.
Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili Dakta Edmund Kayombo akielezea umuhimu wa waganga wa jadi kujisajili katika warsha ya siku tatu iliyofanyika katika kijiji cha Nyakasungwa wilayani Sengerema mkoani Mwanza kuhusu ushirikishaji jamii katika kuandaa na kutekeleza mikakati itakayochangia kuzuia na kutokomeza unyanyasaji na dhulma zinazofanywa dhidi ya watu wenye albinism iliyoshirikisha waganga wa asili, wauguzi na wakunga, viongozi wa dini, walimu pamoja na watu maarufu iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Mshiriki wa warsha ya ushirikishwaji jamii kudhibiti ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi akiwasilisha mpango kazi wa kikundi kazi.
Baadhi ya washiriki kutoka kata ya Nkololo wakifuatilia kwa makini maelezo ya warsha ya siku tatu kuhamasisha ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Picha ya pamoja ya washiriki wa warsha inayoshirikisha wanajamii kuandaa mpango mkakati wa kudhibiti ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi iliyofanyika Usagara wilayani Misungwi mkoa wa Mwanza.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)