Mahakama kuu yapinga mapinduzi Madagascar
Mahakama ya kikatiba nchini Madagascar imefutilia mbali uamuzi wa bunge kumfuta kazi rais Hery Rajaonarimampianina.
Mahakama hiyo ilitamka kwa kinywa kipana kuwa hakukuwa na ushahidi wowote kuwa Rais
Rajaonarimampianina alikuwa ''amekaribia hata kwa nia tu'' kukiuka sheria zozote za Madagascar.
Wanasiasa wanaompinga wametaja uamuzi huo wa mahakama kuwa wa kutamausha.
Bwana Rajaonarimampianina alikwenda mahakamani kupinga kufurushwa kwake kutoka madarakani akisema kuwa asilimia kubwa ya wabunge wanaodaiwa kupiga kura hiyo iliyomuondoa madarakani hawakuwa bungeni wakati wa kura hiyo.
Rajaonarimampianina anadaiwa kuhujumu uchumi wa taifa hilo na pia kushindwa kutekeleza ahadi alizowapa wapiga kura wakati wa kampeini za uchaguzi mkuu.
Rajaonarimampianina alikuwa ameliongoza kisiwa hicho kwa kipindi cha miezi 16 pekee na alikuwa anatazamiwa kuleta utulivu katika taifa hilo lililokuwa katika hatari ya kurejea katika misukosuko ya kisiasa na unga'nga'niaji madaraka kati ya vyama vya kisiasa na viongozi wao.
Mwakilishi wa chama cha rais huyo cha HVM , Rivo Rakotovao, ameunga mkono uamuzi huo wa mapema leo huku msemaji wa chama cha upinzani Pierre Houleder akiutaja kuwa wa ''kushangaza mno.''
Wandani wa maswala ya Madagascar wanasema kuwa rais Rajaonarimampianina anapigwa vita baridi na kiongozi wa zamani Andry Rajoelina na pia rais mwengine wa zamani Marc Ravalomanana.
Viongozi hao japo maarufu walilazimishwa na wahisani wa kimataifa kutoshiriki uchaguzi wa pamoja wa urais uliofanyika mwaka wa 2013 kama sehemu ya makubaliano ya kuleta suluhu ya mgogoro wa kisiasa uliotokana na aliyekuwa rais wa taifa hilo bwana Rajoelina kumn'goa madarakani rais wakati huo (2009)bwana Ravalomanana.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)