Meneja Masoko na Mawasiliano wa Taasisi ya Kifedha ya Bayport Financial Services, Ngula Cheyo, kushoto, akizungumza jambo baada ya kutangaza kusogeza mbele huduma ya mikopo ya viwanja vya Vikuruti, wilayani Kibaha, mkoani Pwani, ambapo sasa huduma hiyo imepelekwa mbele hadi Juni 30, mwaka huu. Picha na Mpiga Picha wetu.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TAASISI ya Kifedha ya Bayport Financial Services inayojihusisha na mambo ya mikopo imesogeza mbele huduma yao mpya ya mikopo ya viwanja vilivyopo Vikukuruti, wilayani Kibaha, mkoani Pwani kwa ajili ya kutoa fursa zaidi ya Watanzania kupata viwanja hivyo vilivyopimwa.
Awali ofa ya huduma hiyo ilipangwa kumalizika Juni 10 mwaka huu, lakini sasa imepelekwa mbele hadi Juni 30, ikiwa ni ongezeko la siku 20 zaidi kama njia ya kuhakikisha kwamba wale wenye nia hiyo wanafanikisha ndoto zao za kumiliki viwanja.
Meneja Biashara wa Taasisi ya Kifedha ya Bayport Financial Services, Thabit Mndeme, kulia akizungumza jambo baada ya kutangaza kusogeza mbele huduma ya mikopo ya viwanja vya Vikuruti, wilayani Kibaha, mkoani Pwani, ambapo sasa huduma hiyo imepelekwa mbele hadi Juni 30, mwaka huu. Picha na Mpiga Picha wetu.
Akizungumza leo mchana jijini Dar es Salaam,Meneja Biashara wa Bayport Financial Services, Thabit Mndeme, alisema kwamba wamekuwa wakipokea maombi mengi kutoka kwa Watanzania wenye uhitaji wa viwanja hivyo, jambo lililowafanya wakae na kuona namna gani wataongeza siku chache kwa wananchi na wateja wao. Alisema kama ilivyokuwa mwanzo, wateja wao watalazimika kuchukua fomu za maombi ya mikopo ya viwanja hivyo katika ofisi yoyote ya Bayport, bila kusahau wakala wao ambayo ni tawi lolote la Bank of Africa (BOA), huku akitakiwa kulipa malipo ya awali kuanzia Sh 150,000.
“Kama ilivyokuwa mwanzo, mara baada ya mteja wetu kuchukua fomu na kulipa Sh 150,000 kwa kupitia benki ya BOA, ataleta nyaraka zake kwetu na atapatiwa kiwanja chake, huku gharama za kiwanja cha chini kabisa ni Sh 1,400,000, ambapo Bayport itamlipia gharama zilizosalia, huku akilazimika kulipia Sh 105,181 kwa mwezi kwa kipindi cha miezi 24,” alisema Mndeme.
Naye Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula
Cheyo, alisema kwamba huduma yao ni muhimu kwa watumishi wa umma,
wafanyakazi wa kampuni binafsi na wajasiriamali ambao wote kwa pamoja
wanachotakiwa kufanya ni kuchukua fomu na kuchagua viwanja watakavyo, kutoka kwenye mradi huo wenye viwanja 1878, huku pia mteja akiweza kiwanja kwa fedha taslimu ya kuanzia Sh 1,400,000 na kuendelea.
“Viwanja hivyo vina uwezo wa kujengwa nyumba za kupanga na kupangisha, hoteli na maduka, vituo vya elimu na ibada, hospitali na kumbi mbalimbali, huku mradi wa umeme na maji vikiwa vinapatikana ndani ya mradi huo ambao ni kilomita 50 kutoka Kisutu jijini Dar es Salaam na kilomita 6.5 kutoka barabara Kuu ya Morogoro,” alisema Cheyo.
Kwa wateja wa malipo ya fedha taslimu, mara baada ya mtu kulipa malipo ya awali katika akaunti ya Bayport iliyopo Bank of Africa (BOA) na kukabidhi nakala ya malipo na fomu za maombi kwa wakala au ofisi ya Bayport, mteja atatengewa eneo kutokana na maombi yake na kuombwa kumalizia kiasi kilichosalia, huku hati ya umiliki wa kiwanja akiipata ndani ya siku 90 baada ya kumaliza malipo yake, na wanaotaka kupata viwanja kwa njia ya mkopo kwa watumishi wa umma, wafanyakazi wa kampuni binafsi na wajasiriamali, wakipata hati
zao baada ya kumaliza mkopo wao.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)