MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei mpya itakayoanza kutumika leo ambapo mafuta ya petroli na dizeli yamepanda huku mafuta ya taa yakishuka.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano EWURA, Titus Kaguo, alisema bei ya jumla na rejareja ya mafuta aina zote imebadilika ikilinganishwa na bei elekezi iliyotolewa Aprili, mwaka huu.
Alisema bei ya rejareja kwa mafuta ya petroli imeongezeka kwa Sh 111 kwa lita sawa na asilimia 6.32 huku dizeli ikiongezeka kwa Sh 23 kwa lita sawa na asilimia 1.37.
“Kuanzia leo lita moja ya petroli itauzwa kwa shilingi 1,866 kwa Jiji la Dar es Salaam na shilingi 2,097 kwa mikoa ya pembezoni ikiwamo Kigoma ambapo bei ya zamani ilikuwa ni shilingi 1,755 Dar es Salaam na shilingi 1,986 kwa Mkoa wa Kigoma,” alisema Kaguo.
Alisema mafuta ya dizeli yatauzwa kwa Sh 1,695 Dar es Salaam na Sh 1,938 kwa mikoani ambapo bei ya awali ilikuwa ni Sh 1,672.
Kaguo alisema mafuta ya taa yameshuka kwa Sh 31 kwa lita sawa na asilimia 1.86 ambapo yatauzwa kwa Sh 1,624 Dar es Salaam na Sh 1, 867 kwa mikoani.
Akifafanua zaidi, Kaguo alisema bei ya jumla ya kwa petroli ni Sh 1,761.05, dizeli Sh 1,589.58 na mafuta ya taa Sh 1,518.86.
Alisema mabadiliko hayo yametokana na kupanda kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia pamoja na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)