Taarifa maalumu kutoka Polisi Kanda maalumu ya Dar Es Salaam juu ya wahalifu waliotiwa nguvuni - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Taarifa maalumu kutoka Polisi Kanda maalumu ya Dar Es Salaam juu ya wahalifu waliotiwa nguvuni


Watuhumiwa wanne wamekamatwa jijini Dar es Salaam katika makutano ya barabara ya Bibi Titi na Ohio karibu na Hotel ya Serena baada ya kumpora raia wa kigeni wakiwa na gari dogo rangi ya kijivu yenye nambari za usajili T787 DBU Toyota Cienta.

Hivi karibuni kumeibuka wimbi la wahalifu kuwapora pesa na vitu vya thamani kama mikufu, bangili, hereni pia pete na vitu mbalimbali vya thamani raia wa kigeni na akina mama ambao hupenda kutembea na pochi. Wahalifu hawa hutumia gari dogo ambalo mara kwa mara hubadilishwa namba zake za usajili na wakati mwingine gari hili wanalitumia kama Tax bubu.

Leo tarehe 21/04/2015 majira ya saa 09:00 asubuhi katika eneo la Posta Mpya watuhumiwa hawa walimdangavya bwana CEES S/O JAN CONIJN, Miaka 27, raia wa Uholanzi aliyetaka kufika Klabu ya Leaders kwamba wangempeleka eneo hilo kwa kutumia gari tajwa hapo juu. Baada ya kuondoka na dereva kila baada ya mita 200 dereva huyo alikuwa anasimamisha gari na kuongeza mtu mwingine kama abiria hadi walipotimia wote wane.

Walimpeleka hadi maeneo ya Kinondoni kwa Manyanya na walipofika eneo hilo walimweleza wazi kuwa wao ni wahalifu na walimtaka awapatie pesa vinginevyo wangemuua. Aliwapatia pesa zote alizokuwa nazo Tshs 75,000/= lakini hawakuridhika ndipo walipomtaka awapatie kadi ya benki (ATM CARD) na nambari za siri (Pass Word). 

Baada ya tukio hilo wakamtupa karibu na Hospitali ya Mwananyamala na wao wakageuza gari kurudi katikati ya  mji. Wakati tukio hilo linatokea raia wema walishuhudia na kutoa taarifa kwa Polisi. Polisi walifuatilia haraka na kuweka mtego uliowanasa watuhumiwa wote katika eneo la makutano ya barabara ya Bibi Titi na Ohio karibu na Hotel ya Serena.
Majina ya watuhumiwa waliokamatwa ni:
1. SALUM S/O SAID MTUMWA @ MARO, Miaka 25, Mkazi wa Chang’ombe Bora.
2. ALEX S/O INNOCENT MANGUKA @ MAKA, Miaka 30, Mkazi wa Kimara Temboni.
3. MOHAMED S/O ALLY ABDALLA @ MEDY, Miaka 27, Mkazi wa Mwananyamala.
4. STEPHANO S/O ALBERT KIKINDI @ KING, Miaka 32, Mkazi wa Mwananyamala.

Walipopekuliwa watuhumiwa hawa walikutwa na simu  mbalimbali za mkononi zipatazo 11 ambazo zinachunguzwa kuhusiana na mbinu ya uhalifu wanaoutumia. Pia ilikamatwa ATM CARD iliyochukuliwa kwa mlalamikaji kabla watuhumiwa hao hawajaitumia. Aidha gari namba T787 DBU Toyota Cienta linashikiliwa kwa uchunguzi zaidi.

Miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa, wawili ambao ni MOHAMED S/O ALLY ABDALLA @ MEDY, na STEPHANO S/O ALBERT KIKINDI @ KING, tayari wanazo kesi nyingine mahakamani na wako nje kwa dhamana.

Sambamba na tukio hili oparesheni ya kuwakamata wahalifu wengine wenye mtindo huu wa kuwapora wageni au wakina mama wenye mikoba inaendelea na tunawaomba wananchi waonyeshe ushirikiano wa kutosha ili kutokomeza vitendo hivyo viovu. Aidha hakuna silaha yoyote iliyotumika au kukamatwa kama ilivyoripotiwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

S. H. KOVA,
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM,
DAR ES SALAAM.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages