Ncaa, unesco waangalia utalii endelevu Ngorongoro - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Ncaa, unesco waangalia utalii endelevu Ngorongoro

DSC_0015
Mkufunzi ambaye pia ni mtaalamu mshauri wa Unesco, katika masuala ya utalii endelevu, James Banks akiendesha mafunzo kwenye warsha ya siku nne ya kutengeneza mkakati wa utalii endelevu hifadhi ya Ngorongoro iliyomalizika mwishoni mwa wiki mji mdogo wa Karatu, mkoani Arusha na kuandaliwa na Shirika la UNESCO kwa kushirikiana na Ngorongoro Conservation Area Authority (NCAA). Pichani chini kulia ni Mmoja wa wakufunzi wa warsha hiyo, Tamim Amijee.(Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog)

Na modewjiblog, Karatu
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) likishirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wameandaa kongamano la siku nne lililofanyika mjini hapa kuangalia mkakati mpya wa kuendeleza utalii kama kitovu cha mapato katika hifadhi ya Ngorongoro.

Kongamano hilo ni moja ya makongamano kadhaa ambayo yameandaliwa kwa pamoja kwa lengo la kutoa mwelekeo mpya katika hifadhi hiyo ambayo binadamu na wanyama huishi pamoja.

Akizungumza na mtandao huu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues, alisema kwamba kongamano hilo limeandaliwa kwa lengo la kujenga uwezo kwa wadau mbalimbali wa sekta ya utalii kutambua haja ya utalii endelevu ambao pia utazingatia maslahi ya wananchi wanaoishi katika eneo hilo.
Alisema wakati NCAA inaangalia upya mkakati wake wa maendeleo katika hifadhi hiyo ambayo pia ni urithi wa dunia, UNESCO kama washirika wa karibu wamekubaliana kuendesha kongamano ambapo wadau wote kuanzia wananchi wanaoishi katika hifadhi hiyo na waendesha utalii zikiwemo hoteli na watawala kuangalia namna bora ya kuendesha hifadhi na kuneemesha wananchi.
DSC_0207
Zulmira alisema kwamba hifadhi hiyo inaingiza fedha nyingi ambazo zingeweza pia kuwafikia wananchi moja kwa moja kwa kuanzisha mikakati ambayo inahusisha wananchi wenyewe na wadua mbalimbali wa sekta hiyo.
Alisema kwamba idadi ya watalii wanaoingia hapo wanaingiza fedha nyingi serikali kuu lakini kiasi hicho hakionekani wazi wazi kwa wananchi na hivyo ipo haja ya kuangalia mwelekeo mpya ambao utaendelea kuhifadhi urithi huo huku wananchi wake wakifaidika na uwapo wa urithi huo.
Wakati wa kongamano hilo washiriki walifanya ziara katika maeneo mbalimbali ya kitalii kabla ya kufanya majadiliano na kuweka mwelekeo wa namna bora ya kutengeneza mkakati utakaoshirikisha wadau wote wa utalii katika eneo hilo.
Alisema kwa muda mrefu tangu hifadhi hiyo iwe urithi UNESCO na NCAA walikuwa wakiangalia zaidi suala la hifadhi kiasi cha wananchi kuona kama wameachwa nyuma hivyo mkakati wa sasa ni kuwawezesha wananchi kufaidi matunda ya urithi huo kwa kila kada kupewa wajibu wake na kuona namna ya kuutekeleza ili ndoto iwe kweli.
DSC_0030
Mkufunzi ambaye pia ni mtaalamu mshauri wa Unesco, katika masuala ya utalii endelevu, James Banks akiwaelekeza jambo washiriki wa warsha hiyo iliyomalizika mwishoni mwa wiki mji mdogo wa Karatu, mkoani Arusha.
“Tumedhamiria kujenga uwezo… kusaidia wananchi kuongeza kipato chao kutoka kwa watalii … ukiangalia katika kreta unaweza kuona magari mengi yakiwa na watalii… tunataka watu wanaoishi katika eneo hili pia wafaidike …” alisema.
Hifadhi hii inatambulika duniani kwa kreta yake kubwa, mbuga yenye wanyama wengi na eneo ambalo inasadikiwa binadamu wa kwanza aliishi kabla ya kutawanyika duniani
Ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 8,300 Hifadhi ya Ngorongoro ndio hifadhi pekee duniani ambapo wanadamu wanaishi pamoja na wanyama kwa usalama.
NCA ilianzishwa mwaka 1971na kutangazwa kuwa urithi wa dunia na UNESCO mwaka 1979 lakini kwa muda sasa kumekuwepo na mawazo kwamba dhima kubwa imekuwa kulinda wanyama na mazingira na kusahaua kwamba pale pana binadamu ambao wanamahitaji na wanataka kufaidika pia na mazingira ambayo wanayalinda.
DSC_0164
Pichani juu na chini ni washiriki na wadau wa sekta ya utalii kwenye warsha ya siku nne ya kutengeneza mkakati wa utalii endelevu hifadhi ya Ngorongoro iliyomalizika mwishoni mwa wiki mji mdogo wa Karatu, mkoani Arusha na kuandaliwa na Shirika la UNESCO kwa kushirikiana na Ngorongoro Conservation Area Authority (NCAA).
Kwa mwaka zaidi ya watalii 450,000 huzuru Ngorongoro ikiwa ni asilimia 60 ya watalii wanaofika nchini.
Mtaalamu mshauri wa Unesco, James Banks, ameelezea kufurahishwa kwake na kongamano hilo na kusema kwamba linatoa mwanya wa wadau mbali mbali muhimu Ngorongoro kuona mwelekeo mpya unaostahili kuchukuliwa ili kuwa na utalii endelevu.
Alisema matokeo ya mkakati huo sio tu utaongeza mapato serikalini bali pia utaimarisha utalii kutokana na ushiriki wa moja kwa moja wa jamii zinazoishi ndani ya hifadhi hiyo.
Mshiriki mwingine wa kongamano hilo Flora Assey, Afisa Utalii kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha alielezea kufurahishwa na kongamano hilo hasa kwa kuchukua mlengo wa masomo kwa vitendo hali ambayo anaamini itabadili kabisa utekelezaji wa mkakati unaobuniwa kwa sasa.
DSC_0035
Naye Meneja mkuu wa Ngorongoro Serena Safari Lodge, Dismas Simba alielezea kuridhishwa kwake na kongamano hilo na kusema litawezesha wadau wote kufanyakazi kwa pamoja kuhakikisha kwamba utalii unakuwa endelevu katika eneo hilo hasa kwa kuzingatia kwamba eneo hilo ndilo pekee duniani ambako wanyama na wanadamu wanaishi pamoja.
Naye Ofisa Mwandamizi wa Miradi na Mratibu wa UNESCO katika masuala ya urithi wa dunia na utalii endelevu, Peter DeBrine amepongeza hatua iliyofikiwa na wadau katika kongamano hilo na kusema raundi ya pili Juni mwaka huu itatoa mwangaza zaidi kwani utarejesha majibu ya maswali ambayo kila mtu amepewa kuyafanyia kazi.
Alisema amefurahishwa na kiwango cha kujituma cha wajumbe waliofika katika kongamano hilo na kusema kwa jinsi ilivyo mabadiliko yanayofikiriwa na NCAA yatafanikiwa ili wananchi nao wawe wanafaidika moja kwa moja na uwapo wa urithi huo wa dunia katika maisha yao.
DSC_0042
DSC_0233
Flora Assey, Afisa Utalii kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha akinakili mambo muhimu wakati wa kuhitimisha warsha hiyo ya siku nne iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano Kudu Lodge and Campsite iliyopo mji mdogo wa Karatu mkoani Arusha.
DSC_0106
Mwenyekiti wa Baraza la wakina Mama kata ya Oloirobi, Kijiji cha Mokilal mkoani Arusha, SEKETO OLDUMU akishiriki kwenye kikundi kazi wakati wa warsha ya siku nne ya kutengeneza mkakati wa utalii endelevu hifadhi ya Ngorongoro iliyomalizika mwishoni mwa wiki mji mdogo wa Karatu, mkoani Arusha na kuandaliwa na Shirika la UNESCO kwa kushirikiana na Ngorongoro Conservation Area Authority (NCAA).
DSC_0057
Meneja Mkuu wa Ngorongoro Crater Lodge | &BEYOND, Markus Schroeder (kulia) akishiriki kuchangia maoni wakati wa warsha ya siku nne ya kutengeneza mkakati wa utalii endelevu hifadhi ya Ngorongoro iliyomalizika mwishoni mwa wiki mji mdogo wa Karatu, mkoani Arusha. Kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni (UNESCO) Zulmira Rodrigues.
Kwa matukio zaidi bofya hapa

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages