Karibu mpenzi msomaji wangu katika safu hii ya mapenzi na maisha. Wiki iliyopita niliishia pale niliposema kwamba, ni dhahiri kwamba, katika uhusiano kila mmoja aliyemkubali mwenzake aliamua kutoka moyoni kwamba ndiye chaguo lake.
Nilisema kwamba, wengi walidiriki kugombana na ndugu zao, marafiki au hata kukejeliwa na jamii kwa sababu ya kuwa na uhusiano na mtu f’lani lakini kwa vile waliona ndiyo chaguo waliamua liwalo na liwe.
Watu wa kundi hili, inapotokea kuumizwa kimapenzi hulia sana kuliko mtu aliyefiwa. Kilio kikubwa kinatokana na kumbukumbu za kuonywa, kupoteza vitu au kuharibu uhusiano ili ampate ampendaye ambaye aliona ni chaguo lake.
Hulia sana kwa sababu aliamini huyo ndiye angekuwa mshauri mkuu katika maisha na angemzika au kumzika atakapomaliza safari ya maisha yake hapa duniani.
TUNAENDELEA TATIZO LIKO HAPA SASA
Unapompata mwenza ambaye kinyume na matarajio yako anakusaliti huku ukiwa unampenda kupita kiasi ndipo maumivu au kulizwa kunapotokea.
Lakini kwa kawaida, mwenza anapomliza mwenzake, kwa wakati ule huwa hajui kama maumivu yale yanaweza kuja kumtokea siku moja katika maisha yake.Wengi wanaposababisha wenza wao kulia wenyewe hujiona wapo sawa. Hawana tatizo na wala hawasababishi kilio chochote bali huenda hao wanaolia ni kwa kukosa kufikiri tu.
UTAFITI WANGU WA KINA NA KWELI
Mimi katika utafiti wangu wa kina na wa kweli, nimebaini kwamba, kila anayemsababishia mwenzake maumivu kwenye uhusiano, yeye akawa ‘komfotabo’ ni lazima siku moja na yeye atakuja kulizwa na mwingine. Iko hivyo!
Wapo wanawake, wanaume wameshawaliza wenzao kwa kuanzisha mahusiano mengine ambayo waliyaona ni bora na yaliyojaa starehe lakini baadaye wakaja kulizwa wao baada ya mategemeo yao kule kugonga mwamba.
NI VYEMA IKAWA HIVI
Wapo wanaume, wanawake wanaojijua kwamba tabia zao si za kudumu na mpenzi. Wapo! Na wanajijua kabisa! Sasa hawa ndiyo walizaji wakubwa. Wao kuliza si ishu na wala hawajutii, lakini natoa onyo kwamba, walio wengi wenye tabia hii huishia kulia wao kwa siku zao za maisha mpaka kifo.
Ni vyema kama unajijua una tabia hii, ukajirekebisha ili uweze kudumu katika mapenzi na kuepuka na wewe kuja kulizwa, hususan kama mlizaji atakutana na mlizaji mwenzake.
UJUMBE WANGU KWA WOTE
Nimalize mada yangu kwa kusema kwamba, unaweza kukaa ukachagua kazi ya kufanya, ikikushinda ukageukia nyingine. Unaweza kuchagua nyumba ya kupanga ikikushinda ukachagua nyingine. Wala hakuna atakayekulaumu wala kusema ulikosea, lakini hakuna kitu kibaya katika maisha kama kukosea jinsi ya kumchagua mwenza.
Ni vyema unapotaka kuwa na mwenza wa maisha yako ukachukua muda kumsoma unayedhani ndiye kumbe siye. Kwani unaweza kumuona mtu aliyevaa koti kubwa kwa nje bila kuona nguo zake za ndani zina rangi.
Kama utamgundua mtu unayetaka awe mwenza wako siye ni bora ukasitisha zoezi mapema hata kama mlifikia hatua ya kukaribia kufunga ndoa. Hakuna sababu ya kuingia kwenye ndoa kwa sababu eti ulishalipia mahari, utalia kwa muda mrefu sana.GPL
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)