Huzuni
ikipitiliza humpelekea mtu kukata tamaa na kutoona thamani ya maisha na hata
kufikia hatua ya kunywa sumu au kujiua wakati furaha ikizidi humfanya mtu
akasahau majukumu mengine mazito yaliyo mbele yake.
Matokeo ya kidato
cha nne yaliyotoka hivi karibuni yamewaacha wanafunzi na wazazi wengi kwenye
majonzi huku wengine wakiwa na furaha. Hii ni kutokana na idadi ya wanafunzi
waliomaliza kuwa na matokeo ya wastani katika mitihani yao.
Pamoja na
hilo, kubwa ni kuangalia namna bora ya kusonga mbele kwa wale ambao hawakufanya
vema wakijipanga upya kuangalia ni yepi ya kufanya ili kuweza kusonga mbele
baada ya jitihada zao zilizotangulia kutofanikiwa wakati wale waliofaulu vizuri
wakiweka mipango na mikakati madhubuti itakayowawezesha kuendelea zaidi.
Jambo la
kwanza analopaswa kulitambua mwanafunzi ni kukubali matokeo aliyoyapata.
Kuukana ukweli huu hakutakuwa na msaada kwake. Ni wazi zinaweza kuwapo kasoro
za hapa na pale katika masuala ya usahihishaji lakini mchango wake katika
matokeo ya jumla unaweza usiwe mkubwa sana.
Kwa muhtasari, matokeo ya kidato cha nne unaweza
kuyagawa katika makundi yaliyopangwa katika Muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Points
Average ama GPA) ambayo ni daraja la
‘A’ kundi la fauli Uliojipambanua
(Distinction) litakuwa na alama kati ya 3.6-5.0, ‘B’ Kundi la Kundi la
ufaulu mzuri (Merit) litakuwa na alama
kati ya 2.6.3.5, ‘C’ kundi la ufaulu wa wastani (Credit) litakuwa na
alama kati ya 1.6-2.5, ‘D’ Kundi
ufaulu hafifu (Pass) 0.3-1.5 na ‘F’
Kundi la ufaulu usioridhisha
(Fail) 0.0-0.2.
Aidha unaweza
kuyagawa katika makundi manne ya walio na sifa za kuendelea na kidato cha tano
na vyuo vya ufundi; wasio na sifa za kuendelea na kidato cha tano na vyuo vya
ufundi lakini wana fursa za kuendelea na vyuo vingine; na waliofeli kabisa
amabo wanakosa sifa za kuendelea na masomo kwa vigezo vya ufaulu wa kidato cha
nne.
Kujiunga kidato cha tano na vyuo vya ufundi
Awali ya yote ifahamike kuwa wanafunzi wanaochaguliwa
moja kwa moja kujiunga na kidato cha tano au vyuo vya serikali ni wale
wanaotoka shuleni (school candidates) na si watahiniwa wa kujitegemea (private candidates).
Kadhalika
wanafunzi wanaochaguliwa moja kwa moja katika vyuo vya ufundi mfano Dar es
Salaam Institute of Technology (DIT), Arusha Institute of Technology (AIT) na
kama hivyo, huwa na sifa sawa na wale wanaochaguliwa kuijunga na kidato cha
tano katika michepuo ya sayansi. Idadi ya wanafunzi hawa huwa si kubwa sana.
Mwanafunzi
aliyefaulu kwa Distiction na Merits ana nafasi kubwa ya kuchaguliwa kuendelea
na masomo ya kidato cha tano au chuo cha ufundi katika shule na vyuo vya
serikali. Aidha hata waliopata Credit na Pass wana nafasi ya kuchaguliwa. Si
tukio la kawaida mwanafunzi aliyepata divisheni F kuchaguliwa kujiunga kidato
cha tano au chuo cha ufundi.
Mara nyingi
changamoto wanayokuwa nayo wanafunzi waliofaulu kwa viwango vya juu ni aina ya
michepuo na shule za kuendelea nazo. Ni jambo la kawaida kukuta kijana akifaulu
masomo mengi na kisha kusoma mchepuo ambao hana mapenzi nao sana. Hili
husababishwa na mazingira ya ujazaji fomu za michepuo ya kuendelea nayo baada
ya kuhitimu masomo. Hutokea kuwa mchepuo anaoupenda sana ana shaka ya kufanya
vizuri na hivyo kuchaguwa michepuo mingine. Ama kwa upande wa shule, hutegemeana
na nafasi, ufaulu wa wanafunzi na idadi ya wanafunzi walioomba katika Shule
husika.
Baadhi ya
wanafunzi wanapokosa michepuo au shule walizoomba huhangaika na kutumia muda
mwingi wakitaka kubadilisha. Uzoefu unaonyesha kwamba ni sehemu ndogo za sana
ya wanafunzi hao ambao hufanikiwa. Ushauri wetu ni kwamba endapo kijana
atachaguliwa katika shule asiyoipenda na hakuna sababu za kiafya za kumfanya
asiende katika shule hiyo pengine kutokana na hali ya hewa, au kachaguliwa mchepuo
asioupenda na familiya yake haina uwezo wa kumsomesha shule binafsi, basi
atulizane katika hicho alichopata na ajikite zaidi katika masomo kwani anaweza
pia kufanikiwa katika fursa hiyo aliyoipata.
Changamoto
nyingine ambayo huwakuta vijana wa kundi hili ni kuanza kusoma tuisheni za
masomo ya kidato cha tano kabla ya uchaguzi kufanyika. Utata wa jambo hili ni
kama tulioueleza hapo juu wa mwanafunzi kuchaguliwa mchepuo tofauti kabisa na
masomo anayosoma. Kwa mfano kuna kijana tunayemfahamu akisoma masomo ya mchepuo
wa Economic, Geography na Mathematics (EGM) lakini akachaguliwa mchepuo wa
History, Kiswahili na Language (HKL). Tofauti iliyoje! Katika hilo inashauriwa
kuwa kama mwanafunzi hana hakika ya kusoma katika shule binafsi, asianze masomo
hayo mpaka baada ya uchaguzi wa kidato cha tano kufanyika. Na ikibidi kujisomea
asome vitu vya jumla kama masomo ya lugha, kompyuta nk.
Kwa wale
waliokwisha amua au lazima wasome katika shule binafsi, ni muhimu kufanya
utafiti juu ya ubora wa shule hizo kitaaluma, maadili na stadi nyingine za
maisha. Aidha ni muhimu kufuatilia juu ya kiwango cha ada, muda wa kuchukuwa na
kurejesha fomu za maombi, tarehe ya usaili na ya kufungua shule. Hutokea
mwanafunzi akapoteza muda na hatimaye kuhangaika kutafuta shule wakati shule
nyingi zimeshasimamisha kupokea wanafunzi.
Kuna
wanafunzi waliopata Pass na Credit ambao hawatapata nafasi ya kujiunga na
kidato cha tano. Hata hivyo vijana waliopata Pass na sehemu ndogo ya waliopata Credit
huwa wanapata sifa na wanaweza kujiunga na kidato cha tano katika shule binafsi
endapo uwezo wa familiya unaruhusu. Hii ni kutokana na kanuni za Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambazo zinamruhusu mwanafunzi kuendelea na masomo ya
kidato cha tano endapo amefaulu katika kiwango cha angalau alama C kwa masomo
matatu au zaidi hata kama masomo aliyofaulu hayatengenezi mchepuo wowote mfano
Civics, Biology na English huku akiwa amepata alama D au chini yake katika
masomo mengine. Endapo familiya itamudu kumsomesha kidato cha tano kati shule
binfasi, ni vema kijana akapata ushauri wa wazazi, walimu na wazoefu wengine
juu ya mchepuo stahiki inayomfaa. Mara nyingi wanafunzi wa aina hii huwa
wanashindwa kutofautisha baina matashi ya nafsi na uwezo binafsi wa kimasomo.
Kwamba kijana tuliyemtaja hapo juu asome CBG au HGL ni suala linalohitaji
tafakuri pamoja na mhusika.
Kujiunga na vyuo vya Ualimu
Kuna
wanafunzi waliopata Pass na hata Credit ambao hawatachaguliwa kujiunga na
kidato cha tano lakini watachaguliwa kujiunga na vyuo vya ngazi ya Diploma
mfano vyuo vya Ualimu. Kwa mujibu wa kanuni zilizopo sasa, kiwango cha ufaulu
cha mwisho kuchukuliwa ni Credit. Pamoja na kujaza nafasi za masomo ya Ualimu,
mwanafunzi atapaswa kuomba rasmi nafasi hizo kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya ufundi au katika vyuo binafsi baada ya matokeo kutoka na nafasi kutangazwa
rasmi. Aidha kutokana na uchache wa nafasi katika vyuo huwa si wote walio na
sifa wanaoweza kuchaguliwa serikalini lakini nafasi ni nyingi sana katika vyuo
binafsi.
Kujiunga na Vyuo Vingine
Wapo vijana
ambao licha ya kuwa na sifa za kuchaguliwa katika vyuo vya ualimu, huwa
hawachagui au hawaendi hata baada ya kuchaguliwa kwasababu zao binfasi. Kama
uwezo wa familia unaruhusu na mnaona kusoma ualimu si kipaumbele chenu haina
tatizo. Hata hivyo, ni vema kuangalia fursa zilizopo na uwezo wa familia
kiuchumi. kijana anapaswa kufahamu kufahamishwa kuwa si busara kwa familia
yenye uwezo duni wa kiuchumi, kama zilivyo familia nyingi za kitanzania,
kumsomesha kijana katika ngazi hii kwa gharama kubwa wakati kuna wengi
wanahitaji kuendelezwa kitaaluma katika familia.
Wale wote
waliokosa nafasi ya kujiunga na kidato cha tano, vyuo vya ufundi, vyuo vya
kawaida au vyuo ualimu, fursa pekee waliyonayo ni kujiunga na vyuo vingine
vinavyotoa kozi mbalimbali kama, biashara, utawala, ufundi, nk. Vyuo kama
College of Business Education (CBE), Tanzania Institute of Accountancy (TIA), Institute
of Social Work (ISW), Institute of Information Technology (IIT) ni mifano michache
katika ya vyuo vingi vilivyopo. Changamoto kubwa katika vyuo hivi ni uwezo wa kuzimudu
gharama zake za mafunzo hayo.
Mwanafunzi
aliyefeli kabisa na kupata Sifuri (0), hana fursa yoyote katika zote
zilizotajwa hapo juu. Hata hivyo anakuwa amepata cheti cha kuhudhuria masomo
(leaving certificate) ambacho huwa na msaada fulani katika maisha kwa kuna
wakati huhitajika vijana waliomaliza kidato cha nne bila kujali ufaulu wake.
Pia kuna
fursa zinazohitaji vijana waliomaliza shule ya msingi ambazo bado zinaweza
kutumiwa na vijana hawa. Kwa mfano kuna fani mbalimbali zinazotolewa na vyuo
vya VETA kama ufundi, udereva, usafi,utunzaji bustani, upishi nk ambazo
zinaweza kutumiwa vema na vijana ambao hawakufaulu mitihani ya kidato cha nne.
Ni muhimu
kutaja hapa kwamba si waliofeli tuwanaoweza kuzitumia fursa za mafunzo ya VETA bali
hata wale waliopata divisheni Pass na hata Credit ambao ama hawakupata fursa za
kuchaguliwa kidato cha tano au familiya zao hazimudu kuwasomesha katika shule
au vyuo vya kujilipia.
Kurudia Mitihani
Wanafunzi
wengi wanaofanya vibaya katika mitihani yao, jambo la haraka linalowajia
vichwani ni kurudia mitihani. Ndio maana siku hizi vituo vinavyotoa mafunzo kwa
wanaorudia mitihani vimekuwa vikiongezeka kila kukicha. Ni kwakuwa soko
linakuwa na wateja wameongezeka.
Pamoja na
kuunga mkono na kuheshimu juhudi za wanaotoa mafunzo hayo, tungependa
tutanabahishe kwamba ni ili kuepusha upotevu mwingi wa muda na pesa, ni vema
mwanafunzi akawa akijiandaa kurudia mitihani huku akijufunza ujuzi mwingine.
Uzoefu unaonyesha kuna wanafunzi wanaorudia mitihani na matokeo yao kuwa mabaya
kuliko ya mwaka uliotangulia. Aidha kuna wanafunzi waliorudia mitihani zaidi ya
mara moja na bado hawakufanikiwa kupata alama C au zaidi (credits) tatu walizohitaji ili wajiunge na
kidato cha tano.
Endapo
mwanafunzi atajiandaa kurudia mitihani huku anapata ujuzi mwingine mfano
udereva, ufundi,nk anakuwa katika nafasi nzuri ya ajira hata asipofaulu
mitihani yake anayorudia. Ni uzuri ulioje endapo atapata vyote - credits na
huku ana cheti cha ujuzi wake.
Jambo hili
linawezekana endapo kijana ataugawa vizuri muda wake chini ya muongozo wa
familia kwa mfano asubuhi akienda chuoni kupata ujuzi na jioni akienda tuisheni
kwa ajili ya kurudia mitihani. Aidha endapo mwanafunzi hatofanikiwa kupata
credits, anaweza kuanza kazi huku ajiandaa taratibu kurudia mitihani yake.
Wengi wamefanikiwa kwa utaratibu huu.
Kukata rufaa juu ya matokeo
Wapo
wanafunzi ambao wanakuwa hawakuwa hawakuridhika na matokeo waliyopata wakiamini
hawakutendewa haki katika usahihishaji pengine kwa kuzingatia rekodi za matokeo
yao katika mitihani ya shuleni au kwa jinsi walivyofanya mitihani.
Kwamba
hatupingi jambo hili ndivyo pia tungependa kusisitiza kuwa wakati ukikusudia hilo
ni vema ukaendelea na mipango mingine ya kujiendeleza kama tulivyoitaja hapo
juu. Hii ni kwasababu ni wanafunzi wachache sana ambao matokeo yao hubadilika
baada ya mitihani yao kusahihishwa upya. Aidha unaweza kupoteza muda mwingi
ukisubiri hatma ya rufaa yako na kisha majibu kuja usivyotarajia.
Ufadhili wa Masomo
Hutokea
wanafunzi waliopata nafasi za masomo katika shule binafsi au vyuo vinavyohitaji
kujilipia wakawa hawana uwezo wa kujisomesha na hivyo kuhangaika huku na kule kutafuta
ufadhili. Ukweli ni kuwa ni wachache sana ambao hufanikiwa. Hii ni kutokana na
kutokuwa na taasisi rasmi zinazotoa ufadhili katika viwango hivi ya elimu
nchini.
Pamoja na
kutokatishana na tamaa, ni vema mtu
unapokuwa katika hali hiyo kutafuta shughuli itakayokuwezesha kujenga nguvu za
kiuchumi na kisha kuweka akiba kwa ajili ya kujisomesha. Unaweza kuweka malengo
ya kusoma huku ukifanya kazi. Endapo shughuli zako hazikupi fursa ya kusoma
huku ukifanya kazi, unaweza kuahirisha kusoma hadi kipindi fulani baada ya
kujiimarisha kiuchumi. Endapo hilo litakuwa gumu kulitekeleza, familia iangalie
uwezekano wa kuuza sehemu ya rasilimali endapo inazo na ambazo hazitaithiri
familia nzima endapo zitauzwa.
Tuhitimishe
kwa kusema, matokeo vyovyote yawavyo hayawezi kuwa ndio mwisho wa maisha. Siku
zote wanaofanikiwa ni wale wanaotazama mbele huku wakijifunza kwa
yaliyowatokea. Walofaulu washukuru huku wakijipanga; waliofanya vibaya wasubiri
huku wakijifuza. Tumia vizuri kila fursa unayoipata bila kujali udogo wake.
Jifunze kwa wengine, uliza, pata miongozo kwa waliokutangulia, na amini kuwa
ipo siku ufanikiwa. Washindi hawaachi, na wenye kuacha hawashindi.
KUVUNJIKA KWA KOLEO SI MWISHO WA UHUNZI
Kwa Msaada zaidi wa ushauri na namna bora ya kusoma
tafadhali wasiliana nasi kwa namba 255
767 488856
au barua pepe marshk86@hotmail.com
Tupo pamoja JL
ReplyDelete