Mbunifu nyota kutoka Zanzibari kuandaa onyesho la mavazi - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Mbunifu nyota kutoka Zanzibari kuandaa onyesho la mavazi

 Zimesalia siku chache ambapo ulimwengu wa mitindo na watanzania kwa ujumla watashuhudia usiku wa staili ambao haujawahi kutokea.  Mbunifu wa kimataifa mwenye makazi Zanzibar Doreen Mashika  kwa kushirikiana na wanamitindo wenye vipaji vya pekee kutoka Tanzania na Kenya pamoja na mtayarishaji kutoka nchini uingereza wanakuletea usiku wa kipekee ujulikanao kama “Fashion Night In by Doreen Mashika” utakaofanyika siku ya tarehe 27 Februari katika hotel ya Hyatt Regency mjini  Dar-es-Salaam. Tukio hili la kihistoria litatoa fursa kwa kampuni ya Doreen Mashika ijulikanayo kama DMZ kuonyesha bidhaa zake zenye viwango vya juu na pia itakuwa fursa kwake kujikita Tanzania bara.

Tukio hili la kipekee litavuta hisia za wale wote wenye mapenzi ya dhati katika ulimwengu wa mitindo. Wanamitindo wakitanzania, wabunifu na wapenzi mtindo, Huna haja ya kuja kwenye onyesho hilo kama mwanamitindo lakini utajikuta ukiondoka kama moja wao! Na hii ndio sababu kubwa ya tiketi la onyesho hili la kifahali kukimbiliwa sana na kuisha kwa haraka.

Doreen Mashika ana kipaji cha kipekee. Ni mbunifu mwenye makazi Zanzibar ambako ndipo anapofanyia shughuli zake zote za ubunifu tangu ametoka nchini Uswisi. Ubunifu wa Doreen Mashika unahamasisha sana na kutokana na hiyo ameweza kupata tuzo nyingi za kimataifa na nchini. Ameshinda tuzo ya African Designers for Tomorrow competition (ADFT), aliyowashinda wabunifu wengine tisa kutoka nchi mbali mbali. Shindano ambalo lilifanyika Julai 2014 na liliandaliwa na FA254 kwa kushirikiana na Vogue kutoka Ujerumani kampuni yenye lengo la kuwapa wabunifu wa Afrika fursa ya kuonyesha na kuuza bidhaa zao katika soko la Ulaya. Doreen anaushirikiano na kampuni ya mitindo ya EDUN iliyopo marekani. Pia ameweza kushirikiana na kampuni ya ANTHROPOLOGIE, iliyopo Marekani inayomiliki maduka  zaidi ya 400 ya rejareja nchini humo.

Doreen anasema kuwa, "Hakika ushirikiano huu umeongeza uaminifu na thamani kwa bidhaa za DMZ, lazima nikiri hili. DMZ sio tu imekuwa ikitajwa kwenye Vogue  lakini pia tumeshinda tuzo la onyesho lijulikanalo kama African Designers for Tomorrow contest, liliofanyika mjini Nairobi. Kama sehemu ya tuzo hiyo DMZ na mimi kama Mkurugenzi wa kampuni hii tutasafiri kwenda kuonyesha bidhaa zetu za kiafrika katika onyesho la Vogue Salon 2015 litakalofanyika Ujerumani mjini Berlin. Hii ni heshima na furaha kubwa sana kwa kampuni.

Mbali na mafanikio haya ya hivi karibuni, Doreen Mashika kupitia kampuni yake ya DMZ alihusika katika onyesho la ‘Ethical Fashion’ la mwaka 2012 lililofanyika  Paris nchini Ufaransa ambako alishinda  tuzo mbili. Mwaka huohuo Katika shindano la Mercedes Benz Africa Fashion Week, alishinda tuzo ya ‘Accessory Designer’ wa Mwaka. Mwaka 2013 alishirikiana na Kampuni ya Samsung katika show ya ‘Amaze Africa show’ iliyofanyika mjini Johannesburg. Tuzo nyingine ni pamoja na Origin Africa Designer Showcase katika onyesho la  Afrika Fashion Week lililofanyika Addis Ababa ambayo ilimpatia tuzo ya ‘US Retail Award’ pamoja na ‘Ethical Fashion Award’.

Sekta ya Ubunifu wa mitindo Tanzania bado ni changa . Inakabiliwa na mabadiliko kutokana na vijana wenye vipaji vya ubunifu wanayo ibuka na kua na nia ya kuliteka   soko la kimataifa. Pamoja na haya yote, Doreen Mashika bado anathibitisha kuwa mwamba imara katika tasnia hii. Doreen anaongelea kuhusu wale watu wanaotaka kuonekana wa kisasa katika njia za asili zaidi, akisema "wabunifu tunajaribu kugundua bidhaa ambazo zitakidhi haja za waafirika, wale wanaopenda mavazi ya kiasili na wale wanaopenda mavazi ya kisasa zaidi”

Doreen akizungumzia changamoto katika sekta hii anasema kuwa, "Sekta hii ina hamasa kubwa lakini hili peke yake halitoshi. Hakuna shule zinazofundisha mitindo na ubunifu, hii ni changamoto kubwa kwa wabunifu wengi. Pia kuna ugumu wa upatikanaji wa vifaa vya ubunifu, kutokana na hili kunakuwa na ugumu wa upatikanaji wa vifaa vyenye ubora.”.

DMZ ni zaidi ya jina la kampuni. Ina jukumu kubwa katika kuwawezesha wanawake kiuchumi, Doreen anafanya kazi kwa karibu na wanawake kutoka maeneo ya vijijini ambao wana sanaa na ujuzi wa kutengeneza vitu mbalimbali vya  jadi za Kiafrika. Bidhaa za DMZ ni mchanganyiko wa vifaa kiafrika na mitindo ya kimagharibi ambao humpatia mvaaji muonekano wa kisasa. Hii hujumuisha mavazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na  vito vya samani ya mapambo ya mikononi, shingoni, nguo, viatu, mikoba, kava za simu, vyote hivi hupambwa kwa  utamaduni wa Kiafrika. Kisiwani Zanzibar bidhaa za DMZ hupatikana mtaa wa Hurumzi. Bidhaa zake pia hupatikana kwa kununua kwa njia ya mtandao.

Tiketi zinapatikana kwa  urahisi kwa wale wanaotaka kuwa sehemu ya onyesho hilo la  ‘Fashion Night In’ na Doreen Mashika na kutokana na upekee wa tukio hili ni vyema kujipatia tiketi yako mapema. Zinapatikana katika mgahawa Epidor ambayo ipo barabara ya Haile Selassie Road ukielekea Seacliff. Kwa Maswali zaidi unaweza wasiliana na waandaaji wa onyesho hilo Spearhead Africa Ltd kupitia barua pepe: contact@spearheadafrica.com au simu: 0713 252 254.

Katika tasnia yenye ushindani kama hii ya ubunifu wa mitindo, watu wanaohusika hawana budi kuwa na  maadili, ubunifu, na uelewa na ufahamu wa mwenendo mzima wa mitindo, pamoja na akili ya kibiashara. Doreen Mashika anaamini kwamba kiini cha utamaduni wa jadi barani  Afrika bado una nguvu, na ni moja ya vitu tunavopaswa kujivunia.

Kuhusu Doreen Mashika
Doreen Mashika alizaliwa na kukua nchini Tanzania, alisoma na kufanya kazi nchini Uswiss.

Alianza kazi katika sekta ya fedha akiwa Uswisi. Akijikita kwenye bidhaa za kifahari huko ndipo alipoanzia kupenda maswala mtindo  na ubunifu. Akiongozwa kwa hisia utamaduni na utajiri uliopo barani Afrika, alirejea Tanzania na kukaa Zanzibar na kuazisha kampuni yake.

Hivi sasa, anamiliki duka lenye bidhaa zinazovutia kimataifa. Ameunda bidhaa za kipekee na kisasa zenye mchanganyiko wa mitindo ya  kimagharibi   na vifaa vya jadi.

Bidhaa za DMZ zinavutia rangi, mahiri na ni maridadi. Bidhaa hizo ni pamoja na  viatu, mikoba, vito na nguo zinazotengenezwa kwa kutumia nguo za jadi za Kiafrika kama vile Kanga, vitenge na turubai. Katika kubuni mifuko na viatu, Mashika anashirikiana na vikundi vya wanawake kutoka vijijini wanaotengeneza vitu hivyo kwa kutumia mikono, na pia kwa kutumia mbinu za jadi za kiafrika.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages