Sehemu ya mlima unaolalamikiwa kumilikiwa na mwekezaji
Wananchi wa kijiji cha Chalangwa Kata ya Chalangwa alfajiri majira ya saa kumi wamefunga barabara ya Mbeya kwenda Chunya baada ya Jeshi la Polisi kumkamata Mohammed Katembo kwa kosa la kutishia kuua.
Baada ya kukamatwa Katembo nyumbani kwake baada ya kufungwa pingu akiwa chini ya ulinzi akidai sababu za kukamatwa kwake ilipigwa mbiu kijijini hali iliyopelekea wananchi kujitokeza kwa wingi na kuamua kuifunga barabara hiyo huku mtuhumiwa akitoroka akiwa na pingu mkononi.
Hali hiyo ilisababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo wakiwemo abiria waliokuwa wanakwenda na kutoka mikoa ya kaskazini,huku wananchi wakimtaka Mkuu wa wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro aje kutatua mgogoro huo.
Mwenyekiti wa kijiji Oscar Mwamwendesya amesema unatokana na mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Joseph Mwazyele kupora eneo la mlima katika kijiji hicho bila taarifa ya uongozi wa kijiji kupitia mkutano mkuu wa kijiji ambao ndio wenye dhamana ya kutunza raslimali za kijiji.
Mkuu wa wilaya ya Chunya Deotatus Kinawiro alilazimika kuingilia kati na kuifungua barabara hiyo majira ya saa nne na nusu asubuhi kisha kukutana na wananchi wa Chalangwa ambapo aliwataka kutoa kero zao ili kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.
Wananchi walidai kuwa Mwazyele amekuwa akitumia Polisi kwa kuwakamata wananchi wanaohoji juu ya umiliki wa machimbo katika mlima kijijini hapo hivyo wamekuwa wakiishi kwa hofu lakini pia hawjui uhalali wa umiliki wake kwa kuwa kijiji hakina nyaraka zozote.
Katika mkutano huo Mkuu wa Wilaya alipiga marufuku tabia za kujichukulia sheria mkononi ikiwa ni pamoja na kufunga barabara na mauaji yaliyokithiri kijijini hapo na wilaya ya Chunya kwa ujumla na Jeshi la Polisi limekuwa likifanya kazi kubwa kudhibiti hali hiyo.
Aidha amepiga marufuku shughuli zote za machimbo kijijini hapo na Mohammed Katembo ajisalimishe na pingu za Polisi lakini wananchi walikataa wakidai afunguliwe papo hapo ambapo Mtuhumiwa alijitokeza na kufunguliwa pingu mbele ya Mkuu wa wilaya.
Mkuu wa wilaya alimaliza kwa kuwataka wananchi kuchangia shilingi elfu mbili kwa ajili ya uwanja wa kisasa wa michezo hali ambayo wananchi waliafiki na kukubali kuchangia.
Na Ezekiel Kamanga wa Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)