Neno Fupi La Usiku: Mawili Ya Lazima Katika Demokrasia... - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Neno Fupi La Usiku: Mawili Ya Lazima Katika Demokrasia...

Ndugu zangu,

Kwenye jamii yeyote ile, pasipo na uhuru wa kujieleza na pasipo na utii wa sheria, basi, hakuna demokrasia.

Kila mtu aweze kusema kwa uhuru kabisa. Na si kusema tu, asikilizwe anachosema. Hata kama mawazo yake hayapendwi kiasi gani.

Wenye fikra tofauti, hata wakiwa wachache ni vema wakasikilizwa. Ni haki yao. Fikra zao ziruhusiwe na zishindwe tu kwenye majadiliano ya hoja. Na hata wakishindwa kwa hoja, uhuru wao wa kuendelea kujadili jambo waliloshindwa lazima uheshimiwe na ulindwe. Maana, wachache hao wanaweza kuyapanga upya mawazo yao na hata kufanikiwa kuwashawishi walio wengi kukubaliana nao.

Na walio wengi nao wana haki ya msingi ya kuyasimamia mawazo yao hata pengine kuwaridhisha wachache kuwa kilichoamuliwa kwa mawazo ya wengi ni sahihi. Maana, siasa ni majadiliano endelevu ya hoja na si kugombana kwa kutiana kabali au kutishana.

Na katika kulumbana huko kwa hoja kuna wakati lazima kulumbana huko kukatishwe na maamuzi yafanyike. Bila hivyo hakutakuwa na kazi yoyote inayofanyika isipokuwa kulumbana tu.

Kama ilivyo, kuwa walio wachache ni vema wakasikilizwa, mawazo ya walio wengi hayana budi pia kuheshimiwa. Maana, uamuzi utakaotolewa utakuwa umetokana na mawazo ya walio wengi. Utakuwa ni uamuzi wa watu na si kikundi kidogo cha watu.

Na kwa vile maamuzi yenye kutokana na matakwa ya wengi ndio yenye kufanya sheria, basi, la pili la muhimu katika demokrasia ni utii wa sheria. Ni lazima kila mmoja atii sheria, ni pamoja na wale walioipinga kabla ya kupitishwa na wengi kwa kufuata misingi ya kidemokrasia.

Ni Neno Fupi La Usiku.

Maggid Mjengwa,
Iringa.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages