Imeandikwa Na Nicodemus Ikonko
WAZAZI wa kizazi chetu hiki tuna
changamoto lukuki katika suala zima la malezi ya watoto wetu. Moja kati
ya changamoto tunazokabiliana nazo na ambazo kwa bahati mbaya hatuwezi
kuzikwepa ni pamoja na malezi ya watoto wetu.
Tunapoamka asubuhi kila mzazi makini
tayari huanza mapema kabisa kukimbizana na ratiba yake ya siku hiyo.
Kuna wanaokwenda mashambani, maofisini, viwandani ama kwenye biashara
zao. Inapofika jioni wengine bado huwa kwenye pilikapika na wengine
wakienda madarasani ili kujiongezea ujuzi.
Lakini kwa upande wa pili wa shilingi
wazazi tunalo jukumu kubwa la kuwalea watoto wetu kwa maana ya kusimamia
elimu zao, afya zao, mavazi yao na mahusiano yao mema na jamii.
Majukumu hayo hatuna namna ya kuyakwepa.
Changamoto hizi sasa zinapata ukali zaidi kutokana na mfumo wa maisha
unaosongwa na utandawazi kwa maana ya kurahisishwa kwa mfumo wa
mawasiliano ya simu za mkononi, mtandao wa kompyuta, mitandao ya kijamii
kama vile Facebook, twitter, YouTube na mingine mingi.
Utandawazi kwa ujumla unawapatia maarifa
na ujanja watoto wetu, yakiwemo mazuri kama mtoto atajielekeza huko
lakini kuna maarifa mabaya pia atakayopata kama wazazi wakijisahau na
haya mabaya ni haraka sana kwa watoto kuyakimbilia.
Kama Mzazi, safu yako hii leo ingependa
ikumegee kisa kimoja kilichotokea hivi karibuni jijini Dar es Salaam
katika moja ya sekondari zetu za kata. Kutokana na maadili ya kazi hii,
nisingependa kuitaja shule husika. Mzazi mmoja anayejali malezi ya
watoto wetu ndiye aliyenisimulia kisa hiki tulipokutana baada ya kazi za
kutwa nzima.
Alisema mwanafunzi mmoja wa shule ya
sekondari ya kata alifanya kosa kubwa shuleni lakini walimu hawakupenda
kumpatia adhabu moja kwa moja hadi aende na mzazi wake. Kutokana na uzito wa kosa lenyewe
hakuruhusiwa kuingia darasani. Kwa bahati nzuri mwanafunzi husika alijua
jinsi wazazi wake walivyo makini na ambavyo hawataki mchezo kwa masuala
yanayohusu nidhamu ya watoto.
Kijana haraka haraka akapanga jinsi ya kupotezea au kutatua suala hilo bila wazazi wake kujua. Kwa mujibu wa mzazi aliyenipa kisa hiki,
kijana akazua ishu kwa wazazi wake wampatie fedha kiasi kadhaa kwa
madai kwamba zinahitajika kwa ajili ya masuala ya kwenda ziara ya
kimasomo na wazazi bila hiana wakampatia fedha hizo.
Akazichukua na kumtafuta njemba mmoja na
kumweleza yanayomsibu na kumtaka aende naye shuleni kwake akazungumze
na walimu kwa kujifanya ndiye mzazi wake halisi. Akamkatia 'pochi' na bila kusita jamaa
akaongozana naye hadi shule kama walivyokubaliana. Lakini alipofika na
kuonana na walimu na kuelezwa kinagaubaga kosa la mwanafunzi huyo,
'mzazi' huyo alimgeuka palepale na kuanza kumwadhibu kwa fimbo mbele ya
walimu wake. Ghafla kijana naye akavimba.
Akaanza kumrushia ngumu ‘mzazi wake’
huku maneno yakimtoka kwamba alimlipa ili amtetee na siyo kumwadhibu na
kumwumbua mbele ya walimu wake. Siri ikafichuka na ndipo walimu
walipobaini kuwa kumbe walikuwa na mzazi bandia na hivyo kumlazimisha
kijana akawalete wazazi wake halisi. Mpo hapo wazazi wenzangu?
Tuimarishe mawasiliano baina ya walimu,
wazazi au walezi na wanafunzi ili sote kwa pamoja tuzungumze lugha moja
badala ya kusubiri kuchezewa mchezo wa kuigiza kama huu.
Usikose safi hii Jumatatu ijayo. O766 843382
nvikonko@gmail.com
Chanzo: Mwananchi Online.





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)