Wakandarasi na Washauri wakiwa wanamsikiliza kwa makini Mtendaji Mkuu wa TANROADS mhandisi Patrick Mfugale (hayupo pichani).Mameneja wa TANROADS toka Mikoa mbalimbali ya Tanzania wakiwa wamehudhuria sherehe za kuweka saini mikataba hiyo.
Baadhi ya wabunge wanaotoka katika mikoa ambayo miradi hiyo ya ujenzi wa barabara itafanyika wakishuhudia sherehe za kutia saini mikataba ya ujenzi wa barabara hizo mapema hii leo jijini Dar es Salaam.Mwakilishi toka Benki ya Maendeleo ya Afrika bwana Patrick Musa akielezea mipango ya Benki hiyo kuendelea kutoa mikopo katika maradi mbalimbali ya maendeleo nchini.Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) Bwana Onishi Yasunori akieleza mikakati ya shirika hilo kutoa mikopo katika shughuli mbalimbali za maendeleo hapa nchini huku akionesha moja ya ramani ya ujenzi wanaotarajia kufanya hapa nchini.
Waziri wa Ujenzi Dkt John Magufuli akisistiza jambo kwa waandishi wa wakandarasi mapema hii leo jijini Dar es Salaam, wakati wa utiaji saini mikataba mitatu ya ujenzi wa barabara.Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale (wa pili kulia) akiweka saini Mkataba ujenzi wa barabara ya Mayamaya hadi Mela, wa pili kulia ni mwakilishi wa Kampuni ya china Henan International Cooperation Group Co. Ltd. Bwana Ghuo Zhijian, kulia ni Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) Bwana Onishi Yasunori na kushoto ni Mwakilishi toka Benki ya Maendeleo ya Afrika bwana Patrick Musa.
Picha Zote na Eliphace Marwa – MAELEZO
Na Eliphace Marwa (Maelezo)
Serikali imetia saini mikataba mitatu ya ujenzi wa barabara yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni Tsh.538 za Kitanzania kwa ushirikiano toka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) mapema hii
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa sherehe za kutia saini mikataba hiyo,Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrck Mfugale alisema kati ya fedha hizo ADB wanachagia asilimia 65.80 , JICA asilimia 29.2 ambazo wametoa mkopo na Serikali inachangia asilimia tano.
“Mikataba iliyotiliwa saini hii leo ni pamoja na ujenzi wa sehemu ya Mayamaya hadi Mela yenye urefu wa kilomita 99.35 inayojengwa na Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) kwa gharama ya zaidi bilioni mia moja kwa muda wa miezi thelasini na sita,” alisema Mfugale.
Alizitaja barabara nyingine ni Mela hadi Bonga yenye urefu wa kilomita 88.8 inayojengwa na Kampuni ya China Railway Seventh Group kwa gharama ya zaidi Sh. bilioni 88 , ambapo muda wa utekelezaji ni miezi thelasini na sita.
Mkataba wa mwisho ni wa ujenzi wa barabara ya Mangaka hadi Mtambaswala yenye urefu wa kilomita 65.5 itakayojengwa na Kampuni ya Sichuan Road and Bridge (Group) Corporation kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 59 na muda wa utekelezaji ni miezi ishirini na nne.
“Napenda kuwapongeza Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na Shirika la Maendeleo la Japan kwa ushirikiano wao kwani sio mara ya kwanza kutupatia mkopo kwa ajili ya ujenzi wa barabara zetu na tunaahidi kuzisimamia ili ziwe katika ubora unaotakiwa”, alisema Mfugale.
Aidha naye Waziri mwenye dhamana ya ujenzi Dkt. John Magufuli alishukuru ADB na JICA kwa mkopo huo na kutoa angalizo kwa wakandarasi wasio makini na kazi zao kukaa chonjo kwani sasa hakuna huruma kwao tena.
“Napenda kuwatahadharisha nyie makandarasi mlioko hapa kama kuna yeyote kati yenu hataweza kufanya kazi kwa ubora na wakati basi asisaini mkataba huu”, alisema Dkt Magufuli.
Nao wawakilishi toka ADB na JICA walimshukuru Waziri Magufuli kwa usimamizi imara wa miradi mbalimbali ujenzi inayoendelea kote nchini. Hii si mara ya kwanza kwa ADB na JICA kutoa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwani Machi mwaka , 2010 walitoa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa barabara za Iringa mpaka Dodoma yenye urefu wa kilomita 260 na barabara ya Namtumbo mpaka Tunduru yenye urefu wa kilomita 193.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)