Nimesukumwa kuandika makala hii kwa sababu ya hali ya mwenendo wa kisiasa unaoendelea hapa nchini kwetu na zaidi nimesukumwa na mienendo ya vijana wenzangu katika hali hiyo.Vijana tumekuwa wachezaji wa mapigo ya ngoma za kisiasa zinazopigwa na wanasiasa wetu wasiolitakia jema taifa letu; wakati mwingine tumekuwa wahusiaka wakuu yaani wapigaji wa ngoma hizo kutokana na kutokutambu nafasi yetu katika taifa letu na mpango wa Mungu ndani yetu; hali inayochochewa na ufinyu wa akili, uvivu wa kufikiri, ulafi na tamaa ya pesa/tamaa ya utajiri wa haraka na kupenda maendeleo makubwa kwa haraka tofauti na kazi/nguvu/mipango tulionayo katika kufanikisha azma hiyo.
Leo tunachezeshwa mapigo ya ngoma za siasa za uongo zenye lengo la kutugombanisha kwa minajili ya dini zetu, makabila yetu, kanda zetu, huku sisi tukifurahia na kuzishabikia ama kwa faida ya siku chache ama kwa faida ya wachache. Bila ueledi na uelewa wa kutosha katika kutambua wajibu wetu kwa taifa tunaingia na kuzicheza hata bila kuuliza. Tutaiangamiza Tanzania kwa uvivu wetu wa kufikiri na kupenda majibu mepesi kwenye maswali magumu.
Leo vijana tumesahau wajibu wetu kwa taifa tumeanza tabia ya kujikomba na kujipendekeza kwa wanasiasa waliona fedha,majina makubwa na umaarufu nchini. Tumesahau misingi yetu hasa misingi inayotuunganisha na jamii yetu; leo tunashinda mitandaoni kutukuza watu, na kupigania watu kana kwamba wao ni kila kitu, badala ya kujadili namna ya kuiwezesha Tanzania kusonga mbele. Vijana wanapewa fedha kutoa matamko yenye lengo lakufarakanisha jamii. Bila kufikiri, tukitanguliza tamaa mbele hao kwenye vyombo vya habari na mitandaoni.
Ukiongozwa na kweli sihitaji kulielezea hili sana kwakuwa liko dhahiri. Vijana hutukuza na hubeba agenda za wanasiasa hao. Na kinachosikitisha wanaofanya hivyo wengi wao wanajinadi kusoma mpaka ngazi ya vyuo. Wameweka kando usomi wao na kuingia kwenye mitego ya kiusaliti. Mara zote nimekuwa nikiamini kuwa Elimu humbadilisha mtu na kumwezesha kufikiri, kubuni, kujitambua, kuhoji, kudadisi kupenda kazi, kuwa na mwenendo mwema na kuboresha afya na maisha yake binafsi na jamii lakini vijana wenzangu elimu imetufanya watumwa wa watu na vyama.
Vijana ni nguvukazi ya taifa na injini ya maendeleo katika taifa lolote lile. Wajibu huu usipomea kwenye akili na damu zetu ni dhahiri tunaanda taifa maskini zaidi duniani. Maandiko yansema "Fahari ya Vijana ni nguvu zao na Uzuri wa wazee ni kichwa chenye mvi". Neno nguvu hapa limebeba tafsiri pana sana, nguvu zao ina maana ya akili, juhudi, udhubutu, maarifa, uzalendo, hamasa na ujasiri wao. Sasa lazima tuulizane tulikokosea na tujirekebishe tulikoenda tofauti na mahitaji hayo ya kimaumbile asilia. Ndiyo maana wako walioamni kuwa ukitaka kufahamu kesho ya taifa lolote lile angalia vijana wake wa leo.
Tukumbuke wazee watatusaidia tu kutuongezea busara katika kuitumia fahari yetu yaani nguvu zetu. Wazee wameshafanya ya kwao tena makubwa sana mpaka sasa hivi tunalo taifa huru, wametimiza wajibu wao, maono yao yameishia hapo. Mwenyezi Mungu kaweka Maono ya taifa kwetu vijana na ndio maana katupa na nguvu kutekeleza yote hayo; suala la kutotambua wajibu wetu na kucheza na hayo maono ni bayana tunaliangamiza taifa letu kwa mikono yetu wenyewe. Na hii ni dhambi kubwa ya usaliti kwa taifa. Na tukumbuke yote haya ni matokeo ya ubinafsi wetu.
Nisisitize, hakika kijana anaeangalia zaidi maslahi yake binafsi kuliko maslai ya umma ni msaliti kwa taifa lake. Yako maswali ambayo ningependa tujiulize, kama kila kijana ataangalia zaidi maslahi yake binafsi taifa la Tanzania litasalia kuwepo? Na je kwa sisi ambao tumefanikiwa kupata elimu za vyuo vikuu tena kwa kodi za watanzania, tungeipata kweli hiyo nafasi kama kila mtu angeangalia lake? Na je ambao hawakufika vyuo vikuu kutokana na sisi tuliopata fursa hiyo kutumia kilichokuwepo watumikiwe na nani? Au faida ya wengine kujinyima ili sisi tusome haionekani tena baada ya sisi kusoma?
Tunajukumu zito la msingi kulitendea taifa, lasivyo siku moja wajukuu au vitukuu vyetu watajauliza ni nini babu zetu walituandalia au kutujengea? Lazima tujifunze kuwa wazalendo wa taifa letu sawa na jinsi ambavyo Mungu anataka. Na uzalendo huu huchochewa kwa sisi kuifahamu historia, na misingi ya taifa letu. Kufahamu tulikotoka, tuliko na tunakokwenda, kutatufanya kuto yumbishwa na yeyote yule au chama chochote. Ni vyema tukumbushane kuwa watu hufa na vyama hupita na hufa lakini Tanzania itasalia.
Tunahitaji kujitambua, na ni kawaida kila kijana anaejiona amesoma kwa ngazi fulani ya kielimu kujiona anajitambua. Kujitambua ninakokusema mimi ni kule kuwa na hali ya ufahamu au uelewa (kujua) wa kutosha juu ya maisha yako kwa ujumla pamoja na mazingira yanayokuzunguka na hivyo kukufanya uishi maisha yanayofanana au kulingana na kusudi la Mungu kwako, uishi katika ubora wa maisha yanayolingana na kiwango cha ufahamu ulionao au kiwango cha kujitambua kwako kutegemeana na nguvu ya taarifa unazopata.
Haijalishi uko chama gani cha siasa, kutofautiana kwa minajiri ya vyama ni jambo la kawaida na jambo la kimaumbile asilia maana Mungu ametuumba hivyo, ninachotaka kionekane hapa ni ile hali ya kutanguliza zaidi taifa mbele kwa kuzingatia wajibu wetu kwa jamii ya kitanzania.
Najua kila mtu ana mtizamo wake wa Kifalsafa na Kiitikadi. Mitizamo hiyo pia hutofautiana chama hadi chama. Kwa nchi yetu mahala ambako unaweza kupitia kwa mujibu wa katiba na kuitumikia jamii yako kama kiongozi wa kisiasa ni kupitia chama cha siasa. Uchaguzi u-mikononi mwako ukiona CHADEMA kinakufaa sawa, ukiona CCM kinakufaa sawa, ukiona CUF inakufaa sawa, ukiona NCCR kinakufaa sawa. Fanya siasa kwenye chama chochote kile lakiniuzalendo na uadilifu/maadili kwa taifa liwe jambo la kwanza. Taifa lenye watu wenye maadili safi litabaki kuwa taifa Imara.
Misingi hiyo ikiwa dira kwetu kamwe hutosikia vijana wametumika kuwa daraja la kuwavusha wanasiasa mchwara, wanaojiona bora kuliko wengine, wenye dhambi ya usaliti na ulafi wa mali huku kwenye jamii wakijipambanua kama watetezi wa jamii.
"Hata kama hatutashinda mapema, tutatoa funzo kwa vizazi vyetu vijavyo kwamba kuchagua kulinda utaifa ni heshima na kuliuza ni uasi mkubwa ambao historia haitasahau milele."
Na. Alex Nicholaus Thomas MUSHI,
DODOMA-TANZANI.A
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)