Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Dar es salaam
MICHUANO ya kombe la mataifa ya Afrika mashariki na kati, CECAFA Challenge imeendelea leo hii kwa timu za kundi C kushuka dimbani kusaka pointi tatu muhimu.
Mchezo wa jioni uliwakutanisha mabingwa watetezi, korongo wa Kampala, timu ya Taifa ya Uganda dhidi ya Rwanda, Amavubi na kushuhudia The Cranes wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye uwanja wa Nyayo , jijini Nairobi.
Katika mchezo wa leo, shughuli ilikuwa pevu na ilisubiria dakika ya 88 ambapo Uganda waliandika bao lao pekee kupitia kwa nyota wao Dan Sserunkuma .
Amavubi walionesha kandanda safi na kutawala mchezo kwa kiasi kikubwa na kupata nafasi za kufunga, lakini walishindwa kuzibadili kuwa mabao na wakafanya kosa moja dakika za lala salama na kushuhudia Uganda wakipachika gozi kimiana na kulaza mechi hiyo kwa ushindi huo wa kwanza katika harakati zao za kuteta ubingwa wao.
Nyota wa mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Dar Young Africans, Khamis Friday Kiiza `Diego wa Kampala` alicheza kwa upande wa Uganda na mwenzake Haruna Hakizimana fadhili Niyonzima alionesha maujanja yake katika kikosi chake cha Rwanda.
Mbali na mchezo huo wa jioni, kuna mchezo wa kwanza ambao Sudan walishuka dimbani kupepetana na Eritrea kwenye Uwanja wa Kenyatta, Machakos.
Katika mchezo huo, Sudan waliibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0. Mabao yamefungwa na Salah Ibrahim akifunga mawili na Tahir Mohammed akijipigia moja.
Mechi za leo zimekamilisha mechi za kwanza za makundi na mechi za pili zitaanza kesho.
Ethiopia watakuwa kibaruani kuvaana na Mashujaa wa visiwani, Zanzibar Heroes, wakati wenyeji Kenya watakabiliana na Sudan Kusini kwenye uwanja wa Nyayo. Hizo zitakuwa mechi za kundi A.
Katika mechi za kwanza za kundi hilo, Zanzibar iliifunga Sudan Kusini 2-1 na Kenya ilitoka sare ya bila kufungana na Ethiopia.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)