Mshehereshaji wa Mjadala wa wazi ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa wenye kauli mbiu "The Future We Want" katika kuadhimisha wiki ya Umoja wa mataifa kusheherekea miaka 68 ya kuanzishwa kwa Umoja huo akiwatambulisha Wachokonozi wa Mada Meza kuu Mh Janeth Mbene, Naibu waziri wa Fedha (wa pili kushoto) Bi. Dorothy Usili, Mwakilishi Msaidizi wa UNFPA ( wa pili kulia), Paul Mashauri Mwenyekiti wa East Africa Speakers Bureau ( wa kwanza kulia) na Dakta. Lwidiko Mhamilawa, Mwenyekiti wa Asasi ya Vijana wa Umoja wa Mataifa (YUNA).
.Ajira kwa vijana si bomu kama watapata mafunzo ya ujasirimali na mitaji
.Serikali yaahidi kuendelea kusaidia vijana kwa maslahi mapana ya taifa
Na Moblog Team
SERIKALI imewataka vijana kuachana na fikra potovu za kuajiriwa pindi wanapomaliza masomo yao na badala yake wafikiri zaidi kujiajiri ili kuweza kupambana na kuondoa kabisa tatizo la ajira nchi. Moblog inaripoti.
Kwa muda mrefu watu wa kada mbalimbali wasomi, viongozi wa dini na wanasiasa wameonya kwamba tatizo la ajira kwa vijana nchini ni bomu linalosubiri kulipuka wakati wowote kutokana na ukweli kwamba fursa za ajira zimekuwa chache nchini.
Akizungumza kwenye Mjadala wa Wazi katika kusheherekea Maadhimisho ya wiki ya Umoja wa mataifa jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Janet Mbene amesema asilimia 75 ya watu hapa nchini ni vijana chini ya umri wa miaka 35 ambayo ndiyo nguvu kazi ya taifa.
Pichani juu na chini ni Naibu Waziri wa Fedha Bi. Janeth Mbene akitoa mada yake juu ya mstakabali wa Vijana katika kupambana na tatizo la Ajira nchini na nafasi ya Serikali katika kuwasaidia vijana kujikwamua kutoka katika lindi la umaskini.
‘Ni muhimu kwa vijana nchini kutambua kwamba kwa wingi wao wanaweza kubadilisha mwelekeo wa nchi na mustakabali wa maisha yao kwa ujumla kwa kutambua kwamba wao wana fursa adhimu ya kufanya mabadiliko kwa maslahi mapana ya taifa,’ amesema
“Vijana wa Tanzania lazima waanze kuchangamkia fursa za mikopo mbalimbali iliyotegwa na Serikali kupitia Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana kwa sababu kwa sasa Serikali si mwajiri mkubwa kama zamani,” alisisitiza
Amesema kuwa vijana wameacha fursa kadhaa za kujifunza na kupitia malengo na mikakati kadhaa ya Serikali kwa sababu ya kutokupenda kujisomea na kufuatilia sera na mipango mbalimbali ya vijana inayotolewa na Serikali.
Mbene amesema Wizara ya Fedha kupitia benki kuu ya taifa inayo programu ya kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwapa mikopo ya ujasirimali ili waweze kujiajiri na kuondokana na tatizo la ajira.
Amesema Serikali itaendelea kutengeneza mazingira mazuri kwa vijana kujiajiri kwa kuwapatia mikopo, stadi za maisha na mafunzo ya ujasirimali ili waweze kuwa wabunifu katika biashara zao na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Mwenyekiti wa East Africa Speakers Bureau Bw. Paul Mashauri akiwaslisha mada yake juu ya Ujasiriamali na stadi za maisha kwa vijana ambapo pia amewasisitiza umuhimu wa Vijana wa kutokukata tamaa kwenye biashara.
Kwa Upande wake Dakta ,Lwidiko Mhamilawa, Mwenyekiti wa Asasi ya Vijana wa Umoja wa Mataifa (YUNA) amesema vijana kutokana na wingi wao wana kila sababu ya kuunganisha nguvu zao na kupaza sauti kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesema kwa muda mrefu vijana wamekuwa nyuma katika kufuatilia mipango ya Serikali kuhusu vijana na hata sera mbalimbali zinazotungwa bungeni kwa ajili ya kundi hili vijana wengi hawazijui.
“lazima vijana wakae chini na wajue wanataka kwenda wapi na wako wapi na nini changamoto zao kwa sasa katika nchi yao ili waweze kuchangia mijadala mbalimbali yenye maslahi mapana ya nchi na wao kwa ujumla.
Dakta Mhamilawa amesema ni fursa pekee kwa vijana kupata wasaa wa kushiriki katika mijadala mbalimbali ya umoja wa mataifa yenye kuleta hamasa ya kujifunza kwa bidii stadi mbalimbali za maisha.
Baadhi ya Wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa maadhimisho hayo.
Mwakilishi Msaidizi wa UNFPA Bi. Dorothy Usili akiwasilisha mada chokonozi ya umuhimu wa Vijana kujitambua katika kujiletea maendeleo.
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakiwamo raia wa kigeni wakifuatilia mada hizo.
Dakta. Lwidiko Mhamilawa, Mwenyekiti wa Asasi ya Vijana wa Umoja wa Mataifa (YUNA) akiwasilisha mada yake ya umuhimu wa Vijana kujijengea tabia ya kujisomea na kufuatilia sera, mipango na mikakati mbalimbali ya Serikali itolewayo kwa Vijana.
Pichani Juu na Chini ni baadhi ya Wanafunzi wa vitivo tofauti chuo kikuu cha Dar es Salaam wakiuliza maswali wa wachokonozi wa mada.
Afisa Habari wa Kitengo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC) Bi. Usia Nkhoma Ledama.
Afisa Mshiriki wa UN Cares Beatrice Mkiramweni akizungumza na waandishi wa habari juu ya umuhimu wa kutoa mafunzo ya maabukizi ya Virusi vya Ukimwi na unyanyapaa.
Afisa Mtaalamu wa Kitaifa wa UNAIDS Bw. Emmanuel Mziray akizungumzia madhara ya unyanyapaa yanavyoweza kuchangia maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi kwenye sehemu za kazi na maeneo mbalimbali wakati wa mjadala wa wazi kwa Vijana katika kusheherekea wiki ya Umoja wa Mataifa nchini uliofanyika kwenye Ukumbi wa Nkurumah Chuo Kikuu cha Dar es Saalaam.
Baadhi ya wafanyakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa wakibadilishana mawazo na baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusiana na matumizi sahihi ya Condom.
Baadhi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa nje ya ukumbi wa Nkurumah Chuo Kikuu cha Dar es Salaam palipofanyika mjadala wa wazi jijini Dar.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)