Pages

HOFU YA MAGAIDI TANZANIA; KAZI IMEANZA

Stori: Shakoor Jongo na Musa Mateja
BAADA ya Kampuni ya Global Publishers kupitia gazeti hili na lile la michezo la Championi kufichua udhaifu wa ulinzi katika maeneo ya Mlimani City jijini Dar na Uwanja wa Taifa, sasa kazi imeanza ya kuhakikisha mashambulizi ya magaidi wa Al-Shabaab kama yaliyotokea nchini Kenya hivi karibuni, hayatokei Bongo.............

Timu ya Risasi Mchanganyiko iliyokuwa ikifuatilia kwa karibu hali ilivyo katika maeneo hayo baada ya kuandikwa kwa habari hizo, imebaini kuwa watu wa usalama wamezinduka na sasa ukaguzi na ulinzi umekuwa wa kutisha tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

UWANJA WA TAIFA
Ulinzi na ukaguzi katika Uwanja wa Taifa umekuwa ni mkubwa sana na zoezi hilo limeanza tangu Jumamosi iliyopita kwenye mechi ya Simba na Ruvu Shooting ambapo hakuna aliyeruhusiwa kupita bila kukaguliwa kwa kifaa maalum. Kufuatia mpango huo wengi walinaswa wakiwa na vitu wasivyostahili kuingia navyo uwanjani hapo.


HAKUNA KUINGIZA GARI NDANI
Vilevile utaratibu mpya ulioanzishwa katika uwanja huo ni kutoruhusu mtu yeyote kuingia ndani ya uwanja na gari isipokuwa ya watu maalum tu.

MLIMANI CITY
Tofauti na hali ilivyokuwa siku chache nyuma, ulinzi wa sasa ‘si wa kitoto’ kwani mbali na magari kukaguliwa kwa umakini mkubwa, pia watu hupitishiwa kifaa maalum mwilini ambacho huweza kubaini uwepo wa silaha au kitu kingine cha hatari.


Ukaguzi wa magari umekuwa ukifanyika getini lakini pia wananchi wanaofika eneo hilo kwa ajili ya huduma mbalimbali, kabla ya kuingia kwenye lango kuu hukaguliwa hadi kwenye mabegi waliyobeba.


“Kweli sasa ulinzi unatisha kila kona ya nchi na hata kama hao magaidi wana mpango wa kuvamia Tanzania, watakuwa na kazi kubwa ya kufanya. Lakini hili suala la kuruhusu magari yenye namba za serikali yapite maeneo yenye mkusanyiko wa watu bila kukaguliwa siyo sawa,” alisema Hassan Maulid wa Kimara jijini Dar.


GLOBAL YAPONGEZWA
Kufuatia habari za kiuchunguzi ambazo zimekuwa zikiandikwa na magazeti yanayochapishwa na Kampuni ya Global Publishers likiwemo hili la Risasi Mchanganyiko, wadau wametoa pongezi zao na kuomba juhudi ziendelee ili kuweka mambo kwenye mstari.


Wakizungumza na gazeti hili juu ya oparesheni hizo, wadau hao wamesema zimekuwa na faida kwa taifa kwani maeneo yaliyokuwa legelege kiusalama sasa yameimarishwa nchi nzima hivyo kuwafanya wananchi wawe na amani.


“Kwa kweli kazi inayofanywa na magazeti haya ni kubwa na ni yenye manufaa kwa taifa, tusipopongeza tutakuwa wanafiki. Sasa hivi unaingia Mlimani City una amani, unakwenda Taifa bila hofu tofauti na kipindi cha nyuma. Lakini si maeneo hayo tu, sehemu nyingi sasa zimeimarika kiusalama,” alisema Sakina Musa wa Kinondoni jijini Dar.


Picha kubwa iliyotumika ukurasa wa 16 ni ya mwanamke gaidi anayedaiwa kuongoza mashambulizi nchini Kenya, Samantha Lewthwaite ‘Mjane Mweupe’.Chanzo Global Publishers Blog

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)