Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya, unapenda kutoa taarifa fupi kuhusu tukio la Shambulio nchini Kenya - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya, unapenda kutoa taarifa fupi kuhusu tukio la Shambulio nchini Kenya


Tarehe 21/09/2013 majira ya saa tano na nusu asubuhi (11.30am) watu wanaosadikiwa kuwa magaidi wakiwa na silaha aina ya Ak 47, magrumeti ya kurusha kwa mkono na vesti zinazosadikiwa kuwa na milipuko (suicide vests) walivamia jengo la maduka (shopping mall) la ‘Westgate’ lililopo eneo la ‘Westlands’ jijini Nairobi, Kenya.

Kwa kuzingatia taarifa iliyotolewa na Serikali hadi sasa zaidi ya watu 68 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 179 wamejeruhiwa vibaya na wanaendelea kupata matibabu katika hospitali za Aga Khan, Hospitali ya Nairobi ( Nairobi Hospital), na Hospitali ya MP Shah.



Taarifa kuhusu watanzania

Hadi kufikia tarehe ya leo 23 Septemba, 2013, Ofisi ya Ubalozi imepokea taarifa ya Mtanzania mmoja, Bwana Vedastus Nsanzungwanko, Meneja, Child Protection, UNICEF ambaye amejeruhiwa kwa risasi na magrunet katika miguu yake yote miwili.

Hivi sasa Bwana Vedastus amelazwa hospitali ya Aga Khan na anendelea kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri. Hata hivyo Ubalozi unaendelea kufuatilia kwa lengo la kupata taarifa zaidi endapo kutakuwepo na watanzania wengine katika tukio hilo.



Katika hatua nyingine Ofisi ya Ubalozi kwa kushirikiana na Uongozi wa Chama cha Watanzania hapa Kenya (TWA) unaandaa utaratibu maalum utakaowezesha jumuiya ya watanzania hapa Kenya kuitikia wito ulitolewa wa kujitolea damu kwa ajili ya kuwasaidia wahanga wa tukio hilo. Zoezi hillo hadi sasa linaendelea vizuri.

Pia Umoja wa Mabalozi wa Nchi za Afrika nchini Kenya (ADC) ukiratibiwa na Balozi wa Tanzania nchini Kenya ulikutana na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kenya kwa lengo la kuwasilisha Salaam za Rambirambi kutoka kwa Wakuu wa nchi zao na hatimaye waliweza kukutana na Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta na kuweza kutoa Salaam za pole na kuahidi ushirikiano wao kwa Serikali ya Kenya.

Mh. Balozi na kwa niba ya Wafanyakazi wa Ubalozi kwa ujumla anatoa shukrani za dhati kwa Watanzania wote ambao wamekuwa wakifuatilia suala hili kwa ukaribu kwa njia ya simu, email nk.

Taarifa zaidi zitaendelea kuwasilishwa kwenu kwa kadiri tutakavyokuwa tunazipata.


Ubalozi wa Tanzania Nairobi

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages