………….
Na Salum Vuai, Maelezo
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,
amesema wahitimu wa fani mbalimbali za afya wanaosomeshwa na serikali
hawana budi kubaki nchini na kuitumikia jamii yao. Dk.
Shein ametoa wito huo jana baada ya kuzindua majego mapya ya dahaklia
ya wnafubzi wa kike na jengo la madarasa, katika Chuo cha Taaluma ya
Sayansi za Afya, Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Akizungumza
na wanafunzi na wananchi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo, Dk. Shein
alisema, serikali inatumia gharama kubwa kuwasomesha wanafunzi wake,
hivyo nao wanapaswa kutimiza ihsani na utu kwa kufanya kazi nchini
badala ya kukimbilia nje. Amesema
kwa bahati mbaya, wapo baadhi ya wananchi na watumishi wa umma wakiwemo
wafanyakazi wa sekta ya afya ambao husomeshwa kwa fedha nyingi za
serikali lakini baada ya kumaliza masomo yao huondoka nchini na kukwepa
wajibu wao wa kuwatumikia wananchi wanyonge waliogharamia fedha hizo
“Hili siyo jambo zuri kwani siku zote ni vyema binadamu azingatie ihsani anayofanyiwa na wenzake”, alisisitiza. Akitoa
mfano kwa kunukuu hadithi ya Mtume Muhammad (S.A.W), Rais Shein
aliwanasihi vijana wote wanaopata fursa ya kusomeshwa na serikali, kuwa
na uzalendo na mapenzi kwa jamii yao inayowategemea kuihudumia. Alisema
kwa hadithi hiyo, alisema Mtume Muhammad (S.A.W) anautanabahisha umma
juu ya ubaya wa kuwaacha watu wanaoutegemea kwa kusema:
“Yatosha kwa mtu kupata dhambi kwa kumtupa yule anayemtegemea” Hata
hivyo, alisema kama mtu anataka kuondoka kwenda kutafuta kazi nje ya
nchi, serikali haimzuii, lakini kwanza ni lazima alipe fedha zote
zilizotumika kumsomesha, kwa mujibu wa agizo la serikali kwa wizara zake
zote. Alifahamisha kuwa, iwapo mtu atashindwa kulipa gharama hizo, wazee au familia yake italazimika kufanya hivyo.
Akizungumzia
kukamilika kwa ujenzi wa majengo hayo pamoja na kupatikana vifaa vya
kisasa, alisema hiyo ni njia moja ya kuimarisha mazingira ya utoaji
mafunzo kwa vijana wanaojiunga na chuo hicho kwa masomo mbalimbali
yanayotolewa hapo. Pamoja
na kuwapongeza vijana waliobahatika kujiunga na chuo hicho katika
huduma tafauti za afya, Dk. Shein alisema ni imani yake kuwa wanachuo
wanaojiunga hapo, huchaguliwa kwa kutimiza sifa, na kwamba nao huamua
kujiunga kwa kuelewa ugumu wa kazi yenyewe baada ya kumaliza masomo yao.
Alisema
utoaji bora wa huduma za afya, lazima utanguliwe na huruma na
ubinadamu, na kwamba kazi hizo humtaka mhudumu kuzingatia wito wa
kuwahudumia wagonjwa kwa upendo pamoja na maadili ya taaluma yenyewe. “Kwa
bahati mbaya, wapo baadhi ya wafanyakazi wa sekta ya afya ambao huweka
pembeni vigezo hivyo na matokeo yake hutokea manung’uniko kwa wagonjwa
wanaohudumiwa”, alieleza Dk. Shein Alisema, mlahaka mzuri na lugha nzuri kwa mgonjwa ni miongoni mwa mambo muhimu katika kumuhudumia mgonjwa.
Pamoja
na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo na chuo hicho, Dk.
Shein aliwapongeza viongozi na wafanyakazi wa hospitali za Unguja na
Pemba na taasisi za afya kwa kujitahidi kuondoa udhaifu huo kwa lengo la
kuwahudumia vizuri wagonjwa Alieleza
kuwa, siku zote mgonjwa anahitaji huruma na imani kutoka kwa
anaemuhudumia wakiwemo wanafunzi wanaohitumu kwenye chuo hicho.
Aliwahakikishia
wanafunzi na watendaji wa sekta hiyo, kuwa daima serikali inatambua na
kuthamini mchango wao kwa jamii, na hivyo inajitahidi kuimarisha maslahi
yao kila uwezo unapopatikana. Aidha,
alisema serikali inaendelea na sera yake ya kutoa matibabu bure kwa
wananchi, ingawa katika baadhi ya maeneo, inapokwazwa na ufinyu wa
bajeti huwataka kuchangia, lakini si nia ya serikali kuona wananchi
wanapata shida.
Pia
alifahamisha kuwa, katika kutanua wigo wa taaluma chuoni hapo, serikali
imeamua kukiweka chini ya Chuo cha Taifa Zanzibar (SUZA), pamoja na
kuanza kutoa digriii ya uuguzi kuanzia mwaka huu.
Aliishukuru
serikali ya Oman chini ya uongozi wa Sultan Qaboos Bin Said, kwa uamuzi
wake wa kujenga na kukiendeleza chuo hicho, akisema hiyo ni dalili ya
mahaba makubwa kwa wananchi wa Zanzibar, ambao wana uhusiano wa miaka
mingi na wenzao wa Oman.
Mapema,
akitoa taarifa za ujenzi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Saleh
Mohammed Jidawi, alisema hadi kukamilika kwake, ujenzi huo umegharimu
dola za Kimarekani milioni 2.36, na samani zake dola 277,000.
Naye
Waziri wa Afya Juma Duni Haji, alisema kujengwa chuo hicho na kuongezwa
kwa dakhalia hizo, kutawaondoshea wanafunzi na walimu usumbufu kwani
saa watapata nafasi ya kusoma na kufanya kazi kwa utulivu. Mkuu
wa chuo hicho Dk. Haji Mwita, aliishukuru serikali kwa kushirikiana na
uongozi na bodi ya chuo katika jitihada za kukiendeleza huku akiainisha
changamoto kadhaa zinazohitaji kupatiwa ufumbuzi zikiwemo uhaba wa
walimu, usafiri, vitendea kazi na uvamizi wa eneo la chuo unaofanywa na
watu mbalimbali.
Kwa
upande wake, Mshauri wa masuala ya afya wa serikali ya Oman, Dk. Sultan
Al Busaidy, akitoa salamu sake kwa niaba ya nchi yake, alisema nchi
yake inaona fahari kubwa kuiona Zanzibar ikipiga hatua katika kustawisha
hali za watu wake, hasa katika sekta ya afya na elimu.
Alisema
serikali ya nchi yake, inajivunia uhusiano wa dhati na udugu wa damu
uliopo kati ya wananchi wa nchi mbili hizo, na akawaombea Wazanzibari
mafanikio zaidi katika kuleta maendeleo. Ujenzi
wa majengo hayo uliofanywa na kampuni ya Mazrui Building Contractors,
uliwekwa mwezi Januari 2011, baada ya kuwekwa jiwe la msingi na Rais Dk.
Shein tarehe 6 ya mwezi huo





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)