Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (pichani) ambaye yuko katika ziara ya kikazi mkoani Iringa ameagiza kufanyika kwa uchunguzi kuhusu utendaji wa vituo vya mizani mkoani Iringa. Agizo hilo lilitolewa katika mkutano ambao Waziri huyo wa Ujenzi alikutana na wafanyakazi wa taasisi zinazosimamiwa na Wizara ya Ujenzi mkoani humo.
Wakati akisomewa taarifa za utekelezaji wa majukumu ya kila taasisi mkoani humo ndipo lilipojitokeza suala la tozo iliyokusanywa kwa magari yaliyokamatwa yakiwa yamezidisha uzito kwa kipindi cha mwezi mmoja wa Julai mwaka huu wa 2013 katika kituo cha mizani cha Wenda kilichop kati ya Iringa na Ifunda katika barabara kuu ya TANZAM.
Meneja wa Tanroads wa mkoa wa Iringa Injinia Poul Lyakurwa alimtaarifu Waziri Magufuli kuwa kiasi cha Shilingi milioni 31.9 kilikusanywa katika kipindi hicho cha mwezi mmoja.
Akishitushwa na kiwango hicho Waziri Magufuli alibainisha kuwa, kiasi hicho kilichosomwa katika taarifa kimetokana na magari 735 yaliyokamatwa kati ya magari 20,700 yaliyopimwa sawa na asiliamia 3.5. “Takwimu hizi sizikubali kwani wastani wa magari yanayokamatwa katika nchi nzima unakaribia asiliamia 40 iweje barabara kuu kama hii iwe na kiwango kidogo kiasi hicho cha magari yaliyokutwa na makosa” hapa ni lazima pafanyike uchunguzi” alisisitiza Mheshimiwa Magufuli na kueleza kuwa hali hiyo hawezi kuiruhusu hata kidogo kuendelea.
Katika hatua nyingine Waziri Magufuli amempongeza Meneja huyo wa Tanroads kwa kufukuza wafanyakazi 18 katika Kituo cha Mizani cha Makambako kwa kutokuwa waaminifu katika kazi zao. Waziri huyo wa Ujenzi aliendelea kubainisha kuwa, takriban asilimia 70 ya wafanyakazi waliokuwa katika vituo mbali mbali vya mizani ya barabara nchi nzima wamebadilishwa baada ya kukamilika kwa zoezi la kutangaza nafasi hizo upya.
Akisisitiza zaidi, Waziri Magufuli alisema “Wizara ya Ujenzi itaendelea kushirikia na taasisi mbali mmbai zikiwemo PCCB, Jeshi la Polisi, TRA na hata kwa kutumia makondakta na wasaidizi katika magari ya usafirishaji ili kuendelea kubaini mbinu mbali mbali ambazo zinaendelea kutumika katika suala zima la vitendo vya rushwa katika vituo vya mizani hapa nchini”.
Kwa upande mwingine Wakala wa Majengo Nchini pamoja na Wakala wa Ufundi na Umeme wametakiwa kuwa wabunifu ili waweze kukabiliana kikamilifu na changamoto mbali mbali zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)