LADY JAYDEE,JB NA AFANDE SELE WAJIUNGA NA CHADEMA. - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

LADY JAYDEE,JB NA AFANDE SELE WAJIUNGA NA CHADEMA.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea kuwavuta wasanii kujiunga na chama hicho, ambapo sasa wasanii wanne wa muziki wa kizazi kipya, maarufu Bongofleva na filamu, wanatarajiwa kutangazwa kuhamia chama hicho wiki hii. 

Wasanii hao wanadaiwa tayari kukubali kuingia kwenye chama hicho na wanatarajiwa kutangazwa rasmi hadharani katika mkutano wa hadhara utakaofanyika jijini Dar es Salaam. Kukubali kwao kuingia katika siasa, kunatajwa kutokana na ushawishi mkubwa uliofanywa na wabunge vijana wa chama hicho, pamoja na Diwani wa CCM kutoka kata moja ya Wilaya ya Kinondoni, ili chama hicho kivune kura za vijana katika uchaguzi mkuu wa 2015.
 
Wabunge hao wa Chadema na majimbo yao katika mabano ni Halima Mdee (Kawe); Kabwe Zitto (Kigoma Kaskazini); John Mnyika (Ubungo) na Joseph Mbilinyi, jina la kisanii Sugu (Mbeya Mjini).
 
Habari kutoka kwa watu wa karibu na wasanii hao pamoja na ndani ya Chadema, zinawataja wasanii hao kuwa ni wanamuziki Judith Wambura maarufu Lady Jaydee na wa miondoko ya Hip hop, Selemani Msindi ama Afande Sele.
 
Taarifa zinawataja wengine kuwa ni mwanamuziki Fredy Maliki maarufu Mkoloni na mwigizaji wa filamu, Jacob Steven kwa jina la kisanii JB.
 
Inadaiwa wasanii hao lengo la kuingia katika siasa kupitia chama hicho, ni kuwania ubunge ambapo Jaydee anatajwa kutaka kugombea wilayani Musoma; Afande Sele Morogoro Mjini; Mkoloni Jimbo la Tanga na JB Jimbo la Mkoa wa Dar es Salaam.
 
Hata hivyo gazeti hili lilipowatafuta kuzungumzia taarifa hizo wote walikana ingawa wapo waliokiri kushawishiwa kuingia kwenye chama hicho na viongozi wa Chadema na wananchi, ili wagombee ubunge.
 
 Afande Sele alikana kujiunga na chama hicho na kusema hana taarifa hizo isipokuwa ni kweli ameshawahi kufuatwa na viongozi wa Chadema wa Mkoa wa Morogoro, wakimtaka ajiunge na chama hicho na agombee ubunge Morogoro Mjini.
 
“Nimeshafuatwa na viongozi wa Chadema wa mkoa na kata nijiunge na chama hicho na nigombee ubunge …tena hata vijana wengi na baadhi ya wazee wamenitaka nigombee ubunge kwa kupitia Chadema lakini nimekataa.
 
“Pia Sugu ni mshikaji wangu na anapokuja Morogoro, vijiwe vyake ndio vyangu naye vijana wameshamfuata wakimwambia anishawishi nigombee ubunge kupitia Chadema, amekuwa akiniambia vijana wananitaka lakini mimi sitaki, sijawahi kujiunga na chama chochote na naona mbunge wa sasa (Abdulaziz Aboud) anafanya kazi nzuri.
 
“Mimi sio mwanasiasa, lakini ni mwanaharakati kupitia muziki na mtandaoni na nimekuwa nikitoa maoni mengi na kukosoa lakini narudia si mwanasiasa na sijawahi kujiunga na chama chochote,” alisema Afande Sele.
 
Vilevile amekanusha kushawishiwa na viongozi wa kitaifa wa Chadema au wabunge, ingawa amekiri kuna wabunge wa chama hicho kuwa ni marafiki zake wakiwemo Mbilinyi na Zitto.
 
Kwa upande wa Jaydee alisema hafuati itikadi ya chama chochote cha siasa na hapendi siasa kutokana na imani kuwa siasa ni uongo na yeye hapendi uongo. Alisema hana nia ya kujiunga na chama chochote cha siasa wala kugombea ubunge kupitia chama chochote.
 
Hata hivyo alipoulizwa iwapo atagombea baada ya Katiba kuruhusu mgombea binafsi, alisema kwa wakati huo atajua.
 
Hata hivyo, Licha ya kuwaona wanasiasa ni waongo, anakiri wapo wanasiasa anawaamini kutokana na kazi zao na kumtaja miongoni mwao ni Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo na Mbunge wa Afrika Mashariki, Shy-rose Bhanji.
 
Mwanamuziki huyo alisema licha ya kuwa na marafiki wa Chadema na CCM kama Sugu na Profesa Jay wa Chadema na Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige na Bhanji wa CCM, hawajawahi kumshawishi kujiunga na vyama vyao. 
 
Mkoloni Akizungumzia taarifa hizo za kujiunga na Chadema, JB alikana na kusema; “mimi na siasa ni vitu tofauti, sijawahi kufuatwa na mtu wa Chadema na angalau kungekuwa na dalili basi uniulize, hiyo ni taarifa ya kutengenezwa na wewe ndiye uliyetengeneza hakuna aliyekupa ni udaku huo.”
 
Kwa upande wa Mkoloni, alisema hajawahi kufuatwa wala kushawishiwa kujiunga na chama chochote, isipokuwa ni mwanachama wa muda mrefu wa Chadema na amekuwa akishiriki kampeni, mikutano ya hadhara na matukio yote ya uhamasishaji ndani ya chama hicho. 

Alisema kuhusu kuombwa kuwania jimbo mkoani Tanga kwa tiketi ya chama hicho, alisema hajawahi kuombwa na chama hicho kufanya hivyo.
 
“Sijawahi kuombwa nigombee jimbo, na kuhusu nia ya kugombea, ni mapema mno kuzungumzia suala hilo sasa na hata kanuni za chama changu haziruhusu labda uniulize swali hilo mwakani naweza kuwa na jibu,” alisema Mkoloni.
 
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, alikataa kuzungumzia taarifa hizo akidai yuko barabarani na masuala yote yanayohusu chama hicho aulizwe Msemaji wa chama hicho.
 
Hata hivyo msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene alisema hana taarifa kuhusu kufanyika kwa mkutano wa chama hicho Dar es Salaam na kutaka apewe muda afuatilie taarifa hizo. Habari leo

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages