Matatizo ni sehemu ya maisha.Kujiua siyo sahihi, usahihi ni kusaka tiba ya tatizo lako Jana ulimwengu uliadhimisha ‘Siku ya Kuzuia Kujiua
Duniani’, ambayo kimsingi iko chini ya usimamizi wa Shirika la Afya
Duniani (WHO), yenye ofisi pia hapa nchini.
Kwa kawaida siku hii iliyoanza mwaka 2003, tangu
wakati huo imekuwa ikiendelea kuadhimishwa kila ifikapo Septemba 10,
lengo kubwa ni kuamsha hisia za umma juu ya tatizo hilo la watu kujiua
ambalo linaendelea kuonekana kubwa nchini na Duniani kwa ujumla.
Makadirio ya shirika hilo la afya, yanaonyesha
kuwa watu 1000,000 ulimwenguni hujiua kila mwaka, sawa na watu 3,000
wanaojiua kila siku, sawa pia na mtu mmoja anayejiua katika kila baada
ya sekunde 40. Walio na umri kati ya miaka 15 na 25 ndio wanaoongoza kwa
visa vya kujiua. Kadhalika ripoti inaeleza takwimu za watu
wanaojaribu kujiua ukilinganisha na miaka mitano iliyopita kwamba
zimezidi hadi kuwa kati ya mara 10 hadi 20.
Hali ngumu za kiuchumi, kusambaratika kwa
familia, unywaji wa pombe, dawa za kulevya ni baadhi ya masuala ambayo
huchochea watu kujiua, huku masuala yanayohusiana na mapenzi (kina
pendapenda) yakielezwa kuwa ndiyo kinara hasa kwa vijana.
Hali ya kujiua nchini
Kulingana na taarifa za Wizara ya Mambo ya Ndani
Tanzania, watu wanaojiua wanaongezeka. Kwa mfano inasema katika miaka
mitano mfululizo watu zaidi ya 3,420 walijiua, huku kasi ya hao
wanaojiua ikionekana kuongeza kwa zaidi ya asilimia kati ya sita na 10,
huku wanaume ndiyo wakielezwa kuongoza kujiua, kwa asilimia 70.
Hali kadhalika watoto 59 wenye umri chini ya miaka
18 walijiua. Kwa jumla wastani wa watu 684 wamekuwa wakijiua au
kuthubutu kutaka kujiua kwa mwaka. Kulingana na taarifa za Jeshi la Polisi, watu
walio na umri wa miaka 15 na 25, ndio wanaoongoza, sababu kubwa ni
matatizo ya kimapenzi na mengine ya kijamii na kifamilia.
Wengine ambao nao hujiua ni wafanyakazi wastaafu kutoka ofisi za Serikali na watu binafsi na sababu kuu ni hali ngumu ya uchumi. Sababu nyingine ni kuambukizwa magonjwa mbalimbali
yakiwamo yale yasiyo na tiba hasa Ukimwi. Wengi wanaojiua huamini hilo
ni jambo zuri kwao kuwaondolea hali ya sononeko moyoni ambayo imekuwa
ikiwasumbua, kitu ambacho siyo kweli.
Prof. Gad Kilonzo wa Chuo kikuu cha Sayansi na
Tiba Muhimbili (Muhas) anaeleza dalili za mtu anayeweza kuonyesha ishara
mbaya ya kuweza kujiua kuwa ni kuonyesha kukata tamaa au kuonyesha
mabadiliko makubwa ya tabia hasa za kutaka kujitenga na watu wengine
akiwa mwenye sononeko au kutopata majibu ya shida inayomkabili.
CHANZO:MWANANCHI NEWSPAPER.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)