Na Mwandishi wa Thehabari.com
VIONGOZI wakuu na watendaji wa idara mbalimbali
kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto nchini leo
wamepewa mafunzo ya namna ya kuandaa bajeti kwa kuzingatia usawa wa
kijinsia.
Mafunzo hayo ya siku nne yanayofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM) yameandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia
taasisi yao ya Chuo cha Jinsia (GTI), ambapo washiriki hao kutoka Wizara
ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto wanawezeshwa kuandaa bajeti kwa
mtanzamo wa kijinsia.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yanasaidia kujenga stadi na maarifa kwa viongozi na watendaji wakuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kuzingatia masuala ya jinsia kwenye bajeti ya Wizara hiyo.
Alisema ni mafunzo yanayounganisha utashi wa kisiasa kwa kuzingatia
masuala ya jinsia na usawa serikalini, ili kupunguza mapengo yaliyopo
inabidi kuwekeza fedha na rasilimali anuai.
alisema nadharia iliyopo kwenye sera inaweza kutekelezeka endapo
kutakuwa na uwezeshaji wa rasilimali na fedha ili kuhakikisha huduma za
kijamii zinatekelezwa kwa kuzingatia mahitaji ya makundi yote yaani
wanawake na wanaume.
Aidha aliongeza kuwa mara nyingi mahitaji ya kundi la wanawake
yamekuwa yakisahaulika jambo ambalo lina onesha kuna kila sababu ya
kuwawezesha watendaji wizara husika kiuchambuizi wa sera na bajeti kwa
mlengo wa kijinsia na kuainisha mapungufu kama hayo ili yaweze kufanyiwa
kazi.
Alisema kundi la wanawake bado limekuwa na changamoto hasa katika
huduma za afya, elimu na yinginezo ambazo zinaongeza mzigo kwa wanawake.
Ameitaka Serikali kuongeza uwekezaji katika kukabiliana na vitendo vya
ukatili wa kijinsia, na kuongeza idadi ya wanawake katika vyombo vya
uamuzi ili kuleta usawa wa kijinsia.
Alisema Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ndiyo wizara
yenye dhamana katika usimamizi wa masuala ya kijinsia nchini Tanzania na
usimamizi wa sera ya jinsia na uratibu wa vitengo vyote vya
jinsia…hivyo ni muhimu kwa watendaji wake kuwa na uelewa kwa kutosha,
uwezo wa kirasilimali na rasilimali watu ili watendaji hao waweza
kufanya ufuatiliaji wa kutosha katika utekelezaji wa masuala anuai
kwenye bajeti.
Alisema wakati TGNP ikijiandaa kuadhimisha miaka 20 ya utendaji wake
licha ya uwepo wa changamoto kadhaa, yapo mafanikio ambayo yanaonekana
katika juhudi za mapambano ya harakati za kijinsia kupitia taasisi hiyo.
“Mabadiliko yoyote ya kijamii ni mchakato na miaka 20 ni mingi,
tungetarajia tuwe tumepiga hatua kubwa zaidi, lakini kwanza ni vizuri
kutambua juhudi zilizofanywa zimeanza kuzaa matunda kwenye maeneo mengi,
miaka 20 iliyopita hata dhana ya jinsia haikuwepo kwenye mazungumzo
yetu hata dhana ya mfumo dume ilikuwa haipo lakini kwa sasa wanawake na
wanaume wanakaa pamoja na kuzungumzia masuala hayo,” alisema Bi. Mallya.
Naye Mkurugenzi wa Mashirika yasio ya Kiserikali toka wizara hiyo,
Marcel Katemba akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu alisema
serikali inajitahidi katika upangaji na utekelezaji wa bajeti maeneo
anuai ili kuhakikisha makundi yote yananufaika na rasilimali za taifa.
Akifafanua juu ya kuendelea kwa hali ya unyanyasaji wa kijinsia
katika baadhi ya maeneo licha ya juhudi za kupambana na vitendo hivyo
alisema serikali inaendelea na utoaji wa elimu ya uelewa juu ya masuala
ya haki, kwani jamii ikielewa vitendo kama hivyo vitakoma mara moja.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)