Rais wa Zanzibar Dr Ali Shein Akisoma hotuba yake kwa wananchi na waumini wa Dini ya Kiislamu wakati Baraza la Iddi el Fitri lililofanyika katika ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Rais wa Zanzibar Dr Ali Shein Akisoma hotuba yake kwa wananchi na waumini wa Dini ya Kiislamu wakati Baraza la Iddi el Fitri lililofanyika katika ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,akitoa hotuba yake kwa wananchi na waumini wa Dini ya Kiislamu  wakati   Baraza la Iddi el Fitri  lililofanyika juzi katika ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja.Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.
--- 
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar  09/08/2013

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa Serikali itafanya kila iwezalo kuwakamata na kuwapeleka katika Vyombo vya sheria Watu waliohusika kuwamwagia Tindikali Raia wawili wa Uingereza hivi karibuni.

Amesema Vyombo vya Ulinzi na Usalama viko Imara na kwamba vitaendelea kulinda amani ya Nchi ikiwemo kuwabaini Wahalifu wote na kuwapeleka katika Vyombo husika.

Dkt Shein ameyasema hayo leo alipokuwa akiwahutubia Wananchi kupitia Baraza la Idd lililofanyika Ukumbi wa Salama Hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar.

Amesema kwa mara ya pili kila inapokaribia Sherehe za Sikukuu kumekuwa na mfululizo wa Matukio ya kihalifu na kuongeza kuwa kila aliyehusika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
“Vitendo hivi si uungwa ni Ukatili, hatutawatia hatiani Wasiohusika lakini kila aliyehusika hatutamsamehe” Alionya Dkt Shein.

Aidha Dkt. Shein amelaani kushamiri kwa Vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo ubakaji hasa kwa Watoto ambapo jumla ya Watoto wakike 480 Zanzibar wamebakwa katika kipindi cha mwezi Julai 2012 hadi Aprili mwaka huu.

Amesema hilo ni jambo la kushtua sana na kwamba wakati umefika kila mmoja kuchukua hatua zinazofaa kudhibiti hali hiyo.

Dkt Shein ametoa wito kwa Wananchi na Viongozi wote kuendelea kupendana bila kuchukiana na kulinda Amani, Umoja na Kuvumiliana kwa manufaa ya Zanzibar.

Amesema panapotokea tofauti za hoja kuhusu suala la Maendeleo ya Nchi jambo la busara ni kuzungumza na kujadili kwa kuzingatia sheria zilizopo kwa manufaa ya Zanzibar.

Dkt Shein ametoa Shukrani kwa Jeshi la Polisi kwa kudumisha hali ya amani katika kipindi chote cha Mwezi wa Ramadhani na kulitaka Jeshi hilo lizidishe juhudi zake kipindi cha Sherehe za Idd na siku za usoni.

Kabla ya Baraza la Idd Dkt Shein alitoa Mkono wa Idd kwa Wazee na Watu wasiojiweza katika hafla iliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar.

IMETOLEWA NA 
IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages