PONDA AWEKA REKODI - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

PONDA AWEKA REKODI


Na Waandishi Wetu
ILE sinema ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Shehe Ponda Issa Ponda kudai kufyatuliwa risasi na polisi wa Morogoro, kulazwa chini ya ulinzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kusomewa mashitaka wodini na kupelekwa Segerea, Dar imeingia ‘part two’ huku shehe huyo akiweka rekodi ya matukio akiwa mshitakiwa, Risasi Mchanganyiko lina mchanyato wa habari............
BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI»


Sheikh Ponda akishuka kutoka kizimbani.
PART TWO ILIPOANZIA
Agosti 19, 2013 saa 2:12 (muda wa kazi ni saa2:30),  Shehe Ponda alifikishwa Mahakama ya Kisutu, Dar akitokea Gereza la Segerea ambapo alifutiwa mashitaka ya kuchochea vurugu nchini kati ya Juni 2 na Agosti 10, mwaka huu kwenye maeneo ya Zanzibar, Dar es Salaam na Morogoro.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hellen Riwa alimwachia huru mshitakiwa huyo, hivyo askari wa magereza wakawa hawana neno naye tena.

Ponda wakati akifikishwa mahakamani.
Saa 2:32, polisi walimkamata tena Shehe Ponda na kumwingiza ndani ya gari aina ya Land Cruiser lenye nembo ya utalii (tours), msafara wa gari hilo na mengine mawili ya aina hiyo yenye askari wa FFU ulianza.
Msafara ulitoka nje ya mahakama na kuelekea kulia ambapo mbele ya safari ilidaiwa kuwa, Ponda alifikishwa kwenye Viwanja vya Gymkhana, jijini Dar ambako alipandishwa kwenye helikopta ya Jeshi la Polisi Tanzania na kupelekwa Morogoro.

DAKIKA 26 ZA DAR MPAKA MORO

Wataalam wa safari za anga walisema kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro (kilometa 178), kwa usafiiri wa helikopta ni dakika 26, ikizidi 30 (kwa gari saa 2:35). Ponda anakadiriwa kuondoka Dar saa 3:30 na kutua Moro saa 3:56 asubuhi ya Agosti 19, 2013.
Uwanja ulitumika kutua helikopta hiyo ni wa Gymkhana mjini Moro. Pale palikuwa na gari maalum lililomchukua Ponda akiwa na askari wa kulinda ghasia hadi Mahakama ya Mkoa wa Morogoro ambapo alisomewa mashitaka matatu.

...Ponda akiwa kizimbani.
AAMBIWA MAKOSA YAKE
Shitaka la kwanza; Agosti 10, mwaka huu kwenye mhadhara uliofanyika Viwanja vya Shule ya Ndege, mjini Moro, Ponda alichochea kwa kusema:
‘’Ndugu Waislamu msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata ambao ni vibaraka wa serikali.”
Shitaka hilo liliunganishwa na mengine mawili anayodaiwa kuyafanya Shehe Ponda maeneo ya Dar na Zanzibar.
Baada ya kusomewa, mwendesha mashitaka alisema upelelezi umekamilikaa na dhamana imefungwa akarudishwa rumande mpaka Agosti 28, mwaka huu ambapo kesi hiyo itaanza kusikilizwa katika mahakama hiyo.

...Wananchi nje ya mahakama.
FILAMU YAENDELEA
Utata ulizuka baada ya Ponda kuondolewa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali na kurudishwa kwenye helikopta. Baadhi ya watu walisema kuwa mtuhumiwa huyo alirudishwa Segerea huku wengine wakisema alipelekwa Zanzibar ambako ana kesi nyingine ya uchochezi.
Hata hivyo, habari za baadaye zilisema Shehe Ponda alirudishwa Segerea, Dar es Salaam.

...Helkopta iliyomleta Sheikh Ponda.
KWA NINI AMEWEKA REKODI?
Shehe Ponda anakuwa mshitakiwa wa kwanza nchini kufutiwa mashitaka na mahakama akiwa ndani ya gari. Washitakiwa wengi hufutiwa mashitaka wakiwa vizimbani.
Hakimu aliyemfutia mashitaka Ponda alifika mahakamani hapo nje ya muda wa kazi kama alivyomsomea mashitaka Muhimbili watu wakidai ilikuwa nje ya muda wa kazi. Kufutiwa mahakama maana yake ni kutopatikana na kesi ya kujibu.
Mbali na kufutiwa mashitaka akiwa ndani ya gari, Ponda ameweka rekodi kwa kuwa mshitakiwa wa kwanza kufikishwa mahakama mbili zilizopo kwenye mikoa miwili isiyopakana kwa siku moja. Moro na Dar zinatenganishwa na Mkoa wa Pwani.

...Ulinzi ukiimarishwa wakati Sheikh Ponda akitolewa kwenye gari ili apande helkopta
FAMILIA YAPIGWA BUTWAA!
Habari kutoka ndani ya familia ya Ponda zinasema, habari za baba huyo wa familia kupelekwa Mahakama ya Kisutu na baadaye Morogoro walizipata juujuu.
“Sisi hizi habari tumezipata juujuu tu, kwanza hatukuamini, kwani tunavyojua ni kwamba baada ya kusomewa mashitaka pale Muhimbili walisema kesi ingeendelea Agosti 28, mwaka huu baada ya kupata nafuu.
“Tumeshangaa sana kusikia kaenda Kisutu, mara kapelekwa Morogoro. Kwa nini mzee wetu wanamtembeza namna hii wakati mgonjwa?” alihoji mwanafamilia mmoja ambaye aliomba jina lake liwekwe kapuni kwa kuwa si msemaji.
Alisema mtu wa zamu ya chakula alikuwa akijiandaa kwenda Segerea, lakini ghafla akaambiwa mzee yupo Moro, awali hakuamini mpaka aliposikia ‘breaking news’ kwenye redio.
Risasi Mchanganyiko lilifanya jitihada zote kumpata msemaji wa familia ya Ponda, Is’haka Rashid lakini bila mafanikio.

...Helkopta iliyombeba Sheikh Ponda ikimrudisha Dar.
URAIA WAKE WACHOKONOLEWA
Wakati Ponda akiendelea na filamu yake, baadhi ya watu wamekuwa na maoni tofauti juu ya uwezo wa kiongozi huyo kwa namna anavyoisumbua serikali.


“Tunasikia Ponda ni raia wa Burundi, wengine wanasema asili yake ni Kigoma, kama ni kweli wa Burundi kwa nini asirudishwe kwenye nchi yake ili serikali ya kule nayo ikahangaike naye.
“Sijaona sababu ya mtu mmoja kuihenyesha serikali kiasi hiki. Kutoka Dar hadi Moro na kutoka kule kuja Dar kwa helikopta ni gharama kubwa kwa mtu mmoja,” alisema mkazi mmoja wa jiji aliyejitambulisha kwa jina la Chisano.

AUNGWA MKONO

Mkazi mwingine wa jijini, Mbaruku Omar alimuunga mkono Ponda akisema  haoni kosa la msingi la mtu huyo lakini akasema kwa vile kesi iko mahakamani hawezi kuzungumzia kwa undani, sheria itachukua mkondo wake.

IMEANDIKWA: DUSTAN SHEKIDELE NA RICHARD BUKOS.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages