Na Onesmo Ngowi, Rais wa IBF/Africa
Katikati ya
miaka ya 90, nchi ya Tanzania ilipata bahati ya kuwa na bingwa wa ngumi wa
dunia ambaye alitambuliwa na Umoja wa Ngumi wa Dunia (WBU). Rashid Matumla
aliweza kuonyesha dunia kwamba Tanzania pia inaweza kushindana na kushinda
katika medani ya ngumi za kulipwa hivyo aliweza kujizolea sifa kemkem yeye
binafsi pamoja na nchi yetu ya Tanzania.
Ilikuwa ni miaka ya msisimko kwenye ngumi za kulipwa na wadau pamoja na
mabondia wengi walisisimka na uwezekano wa nchi yetu kuweza kushinda mataji
mengi zaidi ya Afrika, Mabara pamoja na dunia.
Wakati Rashidi
akiwa bingwa wa dunia, mdogo wake Mbwana naye alikuwa bingwa wa mabara alietambuliwa
na WBU pia. Hiyo iliongeza chachu na hamasa kwa wadau wa ngumi za kulipwa hivyo
nchi ilikuwa kwenye shamrashamra za aina ya pekee.
Mkuzaji (Promota)
aliyefanya mambo yote hayo si mwingine bali ni Kampuni ya DJB Boxing Promotions
iliyokuwa inamilikiwa na kuendeshwa kwa umahiri na ndugu wawili Dionis Malinzi
na Jamal Malinzi. Ndugu hawa wazalendo kweli waliweza kuwekeza kiasi kikubwa
sana katika kuwaendeleza kina Matumla
pamoja na mabondia wengine wengi hapa Tanzania. Ni Watanzania wachache alioweza kushiriki au
kuwekeza katika michezo kama kina Malinzi na hiyo iliweza kuitangaza nchi yetu
kwa kiasi kikubwa.
Kina Malinzi
hawakuwaandalia tu mapambano kina Matumla bali walienda mbali na kuwapeleka
nchini Afrika ya Kusini ili waweze kufanya mazoezi kwenye gyms zilizokwa na
vifaa vya kisasa pamoja na wataalamu mahiri waliowafanyia mazoezi na kubadili
kabisa uwezo wao wa kupigana kuwa wa hali ya juu kama mabondia wezngie katika
nchi zilizoendelea.
Tanzania imepita
katika kipindi kirefu na kigumu bika kuweza kuwa na msisimko kama ule ambao kina
Matumla chini ya kina Malinzi waliuleta nchini. Pamoja na kwamba Magoma Shabani
kutoka Tanga alikuja pia kuwa bingwa wa dunia aliyetabuliwa pia na WBU lakini
ule msisimko waliouleta kina Matumla na kima Malinzi ulishafifia.
Ujio wa
bondia Francis Cheka na wengine wa jika lake umeanza tena kufufua matumaini na
msisimko wa ngumi za kulipwa hapa Tanzania. Cheka bondia kutokaMorogoro ameweza
kuwa kivutio pekee wa ngumi za kulipwa kwa sasa hapa Tanzania na Afrika ya Mashariki
kwa ujumla.
Francis
Cheka ni bondia pekee katika bara la Afrika ambaye ameweza kushinda na kutetea
taji la IBF kwa kipindi kirefu.
Nikiwa kama
Rais wa IBF katika bara la Afrika,Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati, ninaona
faraja kubwa sana kuwa karibu na bondia Francis Cheka. Kwa kweli umahiri wake
sio tu kwenye ulingo bali ni namna Cheka anavyojichanganya na watu wengine
katika jamii.
Francis
Cheka anatambuliwa kuwa bondia namba 4 katika viwango vya mabara vya IBF na ni
bondia pekee katika bara la Afrika aliye na kiwango cha juu kama hicho katika
orodha ya mabondia wa kiafrika katika uzito wake wa Super Middle.
Tanzania imeona
na kushughudia malumbano mengi katika ngumi za kulipwa ambayo yanaletwa na
sababu ambazo hazina msingi. Tumefikia
mahali tumalize tifauti zetu na kukaa meza moja ili tuweze kuuendeleza mchezo
wa ngumi za kulipwa hapa nchini kwa faida ya taifa letu ili kuwapata kima Matumla
na kina Cheka wengi zaidi. Pia
ushirikiano wetu utawapa moyo kina Malinzi wengi zaidi kuweza kushirikiana
katika kuuendeleza mchezo wa ngumi.
Nataka itambulike
rasmi kuwa bondia ana HAKI ya kuchagua ni taji lipi au chama kipi anataka
kupigania. Chaguo lake lisilete mzozo au vivu kati ya wanaosimamia mchezo wa
ngumi badala yake ulete ushirikiano utakaoweza kumsaidia bondia mwenyewe ili
aweze kushinda na kuitangaza nchi yetu vizuri.
Ndiyo maana
naona faraja sana kwa bondia Francis Cheka kupata nafasi ya kupigana pambano la
dunia. Kwangu mimi Francis Cheka ni bingwa wangu wa Afrika (IBF) mpaka
atakapopanda ulingoni siku ya tarehe 30 Augusti katika ukumbi ya Diamond
Jubilee. Mimi itakuwa
mmoja wa maelfu ya Watanzania watakaokwenda katika ukumbi ule kumshangilia
Francis Cheka akiipeperusha bendera ya Tanzania.
Kwa kawaida
bingwa wa shirikisho moja akishaamua kuwania mkanda wa shirikisho lingine anapoteza
ubingwa wa shirikisho alilokuwa analishikilia. Lakini nimechukua pia jukumu la
kuhakikisha kuwa kwa bahati mbaya kama Cheka akishindwa kuupata ubingwa wa
dunia hatapoteza ubingwa wake wa IBF Afrika. Pia hatapoteza viwangio vyake alivyonavyo
katika IBF. Hii itamsadia kuweza kung’ara zaidi.
Mimi nadhani
imefikia wakati sasa sisi watanzania wenye nia nzuri ya maendeleo kushirikiana
na kuhakikisha kuwa nchi hii inapiga hatua kwenye medani ya ngumi.
Hongera Sana
Francis Cheka pamoja na waandaaji wa mpambano huo muruwa.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)