BAADA YA KUPIGWA RISASI MOROGORO, HII NDIO SINEMA YA PONDA.........MWONGOZAJI WA FILAMU HAJULIKANI. - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

BAADA YA KUPIGWA RISASI MOROGORO, HII NDIO SINEMA YA PONDA.........MWONGOZAJI WA FILAMU HAJULIKANI.




Na Mwandishi Wetu

TUKIO la Katibu wa Jumuiya ya Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda kudaiwa kupigwa risasi na askari wa jeshi la polisi mjini Morogoro ni sakata linalotengeneza taswira mithili ya sinema yenye kisa kisichoeleweka.

Huku utata ukitawala, jeshi la polisi kupitia kwa Kamanda wa Mkoa (RPC), Faustine Shilogile likipinga kumpiga risasi Ponda, kwa upande wa Waislamu mkoani hapa wanathibitisha kwamba mwanaharakati huyo amepigwa risasi begani.................
BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI»

Sinema inaendelea; polisi wanahoji kama Ponda kapigwa risasi ni kwa nini asijitokeze apewe matibabu? Wafuasi wake wanasema hawawezi kumweka hadharani, wakihofia kiongozi huyo kufanyiwa kitu kibaya.

Wakati utata ukiendelea, picha inayomwonesha Ponda akiwa ameshajeruhiwa kwa risasi kwenye bega la kulia, imevuja mtandaoni (gazeti hili linayo picha hiyo).


Vilevile wakati RPC Shilogile anadai anamtafuta ndani ya Moro, tayari kiongozi huyo alikuwa ameshafikishwa Hospitali ya Taifa, Muhimbili, Dar es Salaam kwa matibabu.

POLISI NI WAZEMBE KIASI GANI?
Agosti 11 (Jumapili iliyopita), saa 5 asubuhi, RPC Shilogile aliitisha mkutano na waandishi wa habari, akadai kwamba jeshi lake halijampiga risasi Ponda na kwamba wanaendelea kumtafuta.


Taarifa za uhakika; Ponda alifikishwa Muhimbili siku hiyohiyo, saa 6 mchana, moja kwa moja akapokelewa kwenye Taasisi ya Mifupa na Ufahamu (Moi) kisha akaanza kutibiwa mara moja.


Ofisa Habari wa Moi, Almasi Jumaa, alilithibitishia gazeti hili Jumapili iliyopita, saa 10:30 alasiri kwamba Ponda anaendelea kutibiwa katika kitengo hicho cha tiba ya mifupa katika Hospitali ya Muhimbili.
“Ni kweli Ponda tunaye, leo hii tutampeleka chumba cha upasuaji kwa huduma zaidi,” alisema Almasi.


Tafsiri; mpaka Ponda anaondoka Morogoro hadi anafikishwa Muhimbili, polisi mkoa huo hawakuwa na taarifa zozote, vilevile hawakujua alilala wapi mkoani hapo.

PONDA KAPIGWA RISASI NA NANI?
 Kwa mujibu wa Almasi, Ponda alifikishwa Moi akiwa amefungwa bandeji kwenye bega la kulia kisha akajieleza kwamba amepigwa risasi.
RPC Shilogile alisema kuwa polisi wakati wanafanya jaribio la kumkamata Ponda Morogoro, walipiga mabomu ya machozi kisha wakafyatua risasi tatu za baridi hewani ili kuwatawanya wafuasi waliokuwa wanazuia kiongozi huyo kukamatwa.
Maelezo hayo ya RPC, yanaacha viulizo vingi kwenye vichwa vya watu, swali kuu likiwa pale begani Ponda kafanya nini? Kama siyo polisi, ni nani mwingine aliyempiga risasi?

KUNA ALIYETUMWA KUVURUGA AMANI?
Kwa mujibu wa RPC Shilogile, Ponda hakuonesha ukaidi wa aina yoyote pale polisi walipotaka kumkamata, isipokuwa wafuasi wake ndiyo walipinga kitendo hicho, hivyo kuanzisha vurugu.
 

Kwa tafsiri ya RPC, Ponda kama kweli kapigwa risasi, maana yake aliadhibiwa kwa makosa ya watu wengine.

Ukienda mbele zaidi, kauli hiyo ya RPC inaweka wazi shaka kwamba pengine ndani ya jeshi la polisi, kuna askari waliopo kwenye sura ya wakala mchochezi (agent provocateur) wenye lengo la kuvuruga amani ya nchi.
Mfano wa Ponda kupigwa risasi katika mazingira ambayo hajaonesha ubishi wowote, inalipeleka tukio kwenye kumbukumbu ya mwandishi wa habari wa Channel Ten, Iringa, David Mwangosi, aliyeuawa katikati ya askari polisi.
Kama ilivyokuwa kwa Mwangosi, kauli ya RPC Shilogile inaonesha namna ambavyo hakukuwa na sababu ya kumpiga risasi Ponda.

POLISI WELEDI MDOGO
Kwa mujibu wa uchunguzi wetu, Ponda alifika Morogoro mapema na alisali adhuhuri (sala ya saa 7 mchana), mkoani hapo lakini polisi hawakumkamata wakati nia ya kumtia nguvuni walikuwa nayo.
RPC Shilogile alisema kuwa walifikiria kumkamata wakati akifanya mkutano wa kidini katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege lakini walihofia amani kuvurugika kwani kulikuwa na idadi kubwa ya Waislamu wapatao 3,000.


Swali kuu linaloulizwa na wengi ni kwamba kwa nini polisi walazimishe kumkamata Ponda barabarani akitoka kwenye mkutano, huku wafuasi wake wakishuhudia, wakati tayari kulishakuwa na angalizo la kuvurugika kwa amani?

KWELI NI SINEMA
RPC Shilogile alisema kwamba mkutano wa kidini ambao Ponda alihudhuria, ulifanyika kwa baraka zote za jeshi la polisi mkoa.
Alisema, kabla ya kutoa kibali, walitoa masharti kwamba hakutatakiwa kufanyika uchochezi wa aina yoyote wala asitokee mzungumzaji yeyote atakayeitusi dini nyingine wala serikali.


“Kibali kilielekeza kwamba mkutano huo ufanyike kuanzia saa 9:00 alasiri mpaka saa 12:00 jioni. Muda ulifuatwa na kila kitu kilifanyika kama kibali kilivyoelekeza,” alisema Shilogile na kuongeza:


“Saa 11:55 jioni, Ponda alikaribishwa, akazungumza kidogo na kuahirisha mkutano. Hakuzidisha muda wala kuzungumza uchochezi.”
Shilogile aliongeza kwamba kwa vile Ponda alikuwa anatafutwa kwa kufanya uchochezi Zanzibar na Dar es Salaam, vilevile kwa kuwa bado anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja ambacho kinamtaka asitoke nje ya Dar, ilibidi kumkamata.


“Alipotoka pale uwanjani, alitangaza anakwenda kusali kwenye Msikiti wa Dini Moja Mungu Mmoja, polisi katika kutekeleza azma ya kumkamata, njiani walisimamisha gari alilokuwa amepanda ili kumkamata,” alisema Shilogile, akaongeza:


“Ponda baada ya kutajiwa sababu za kukamatwa, akawa anajieleza, walitokea wafuasi wake waliokuwa wanapinga kukamatwa kwake, wakaanza kurusha mawe ndipo vurugu zikatokea.
“Polisi walipiga hewani risasi za baridi na kupiga mabomu ya machozi. Na hivi sasa tumewakamata watu wawili ambao walizuia Ponda asikamatwe.”

PATASHIKA POLISI NA PONDA
Habari zinasema kuwa baada ya vurugu kutawala, utupaji wa mabomu ya machozi pamoja na risasi za baridi (kama alivyosema Shilogile) kushika kasi, wafuasi wa Ponda walimwona kiongozi wao akivuja damu.
Ustaadh Vurungwe ambaye alitambulishwa kama msemaji wa Waislamu katika sakata hilo, alisema kuwa baada ya kuona anavuja damu, wafuasi walimtorosha Ponda na kumpandisha Bajaj kumuwahisha Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.


“Baada ya kufika hospitali ya mkoa, kukatokea mvutano kati ya Waislamu kwa Waislamu, wengine wakisema pale siyo mahali salama kwani Sheikh Ponda anaweza kufanyiwa kitu kibaya, wengine wakitaka atibiwe palepale.
“Tukiwa katika mvutano, polisi walitokea, kwa hiyo vurugu nyingine zikatokea. Waislamu walimchukua Sheikh Ponda kumpeleka Hospitali ya Kiislamu Morogoro,” alisema Sheikh Vurungwe.


Gazeti hili lina picha zinazoonesha jinsi wodi namba mbili ya Hospitali ya Mkoa, ilivyoharibiwa hasa kwenye madirisha, wakati wa purukushani kati ya polisi na wafuasi wa Ponda.

HOSPITALI ALIKOPELEKWA
Mwandishi wetu, alifika Hospitali ya Kiislamu iliyopo Msamvu, Morogoro na kukuta milango imefungwa kwa kufuli lakini mtu mmoja aliyedai ni mhusika, alithibitisha kumpokea Ponda.


Hata hivyo, ilibainishwa kwamba Jumapili asubuhi, Ponda aliondolewa hospitalini hapo na kupelekwa Muhimbili ambako alipokelewa kitengo cha mifupa saa 6 mchana.CHANZO GLOBAL PUBLISHERS TZ

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages