Pages

Uzazi pasipo mipango unavyowatesa wanawake Kishapu


Na Thehabari.com, Kishapu

WASUKUMA ni moja ya makabila nchini Tanzania ambayo awali yalishikilia desturi ya  familia kuwa na idadi kubwa ya watoto. Familia moja yaani baba na mama waliendelea kuzaa kadri walivyo jaaliwa kupata watoto bila kujali ukubwa wa familia. Mume pia hakuwa na kizuizi katika familia cha kuongeza mke  mwingine endapo atakuwa na ardhi (mashamba) na mifugo (hasa ng'ombe) ya  kutosha kuweza kuihudumia familia aliyonayo.

Wapo walioamini kwamba kuwa na ukubwa wa familia ni  kuongeza nguvu kazi katika uzalishaji kwa kutumia ukubwa wa familia.  Hata hivyo pia wapo walioamini uzazi ni mpangilio wa Mungu hivyo  haupaswi kupangiliwa na wazazi bali mola mwenyewe. Hivyo basi familia za imani hii ziliendelea kuza hadi pale uwezo wa kupata watoto ulipopotea  wenyewe au vizuizi vingine.

Hata hivyo sasa hivi mambo yamebadilika kiuchumi,  hali ni ngumu hivyo familia nyingi zinapangia idadi ya watoto.  Waliojisahau na kuendelea kuzaa idadi kubwa ya watoto pasipo na uwezo  kuwamudu wanajuta na kutamani wangelipata uelewa wa elimu hiyo awali.
Hali hii ya majuto ndiyo inayozikuta baadhi ya  familia katika vijiji anuai Kata ya Kishapu, mkoani Shinyanga, baada ya  kuzungumza na mwandishi wa makala haya. Familia hizi zimejikuta na idadi kubwa ya watoto kiasi cha baba na mama kushindwa kuwapatia mahitaji ya  msingi watoto wao hivyo familia kuendelea kuwa na maisha duni kiuchumi.

Bi. Rejina Moshwa (37) mkazi wa Kijiji cha Isoso ni  miongoni mwa familia zinazojutia uamuzi wa kuwa na idadi kubwa ya  watoto. Anasema familia yao ilikuwa na jumla ya watoto 10, lakini bahati mbaya wawili walifariki dunia hivyo kubakia na watoto nane ambao ni  mzigo mkubwa hivi sasa.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)