Waziri wa Mambo ya Nje wa
Marekani, Bw. John Kerry, akizungumza wakati wa mkutano wa Baraza Kuu
la Usalama la Umoja wa Mataifa, uliokuwa ukijadili hali katika eneo la
Maziwa Makuu na uungaji mkono Mpango Mpana wa Kisiasa wa Umoja wa
Mataifa wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Maendeleo katika Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo na Maziwa Makuu.
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akizungumza kwa niaba ya Serikali.
Taswira ya Ukumbi wa Baraza Kuu
la Umoja wa Mataifa ulivyokuwa siku ya Alhamisi wakati wa mkutano
uliojadili hali katika eneo la Maziwa Makuu, mkutano huo ulihudhuriwa
pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, Mwakilishi wake wa
Maziwa Makuu Mary Robinson, Mawaziri kutoka nchi za Maziwa Makuu, SADC
, Umoja wa Afrika, EU, na Mkuu wa Banki ya Dunia aliyeongea kwa njia
ya Video kutokea Makao Makuu ya Banki hiyo jijini Washington.
----
Imeandikwa na Mwandishi Maalum, Umoja wa Mataifa, NY — Wakati hali ya
usalama ikiendelea kuwa tete Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo, kufuatia kuibuka upya kwa mapigano hivi karibuni. Marekani
imetamka bayana mbele ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa,
kwamba, inakaribisha na kuunga mkono upelekaji wa Brigedi Maalum (
Force Intervention Brigade) pamoja na mamlaka iliyopewa kupitia Azimio
namba 2098 la 2013.
Brigedi hiyo Maalum inaundwa na wanajeshi kutoka Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi. Na imepewa mamlaka na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ya, pamoja na mambo mengine, kuyakabili na kuyadhibiti na ikibidi kutumia nguvu za ziada pamoja na kuyapokonya silaha makundi ya wanagambo wakiwamo M23 na FDRL.
Brigedi hiyo Maalum inaundwa na wanajeshi kutoka Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi. Na imepewa mamlaka na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ya, pamoja na mambo mengine, kuyakabili na kuyadhibiti na ikibidi kutumia nguvu za ziada pamoja na kuyapokonya silaha makundi ya wanagambo wakiwamo M23 na FDRL.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bw. John Kerry ameyasema hayo wakati alipokuwa akiongoza mkutano wa Baraza Kuu la Usalama katika ngazi ya Mawaziri ulioandaliwa na Marekani ambaye ndiyo RaisAjenda iliyoandaliwa na Marekani na kujadiliwa na Baraza hilo siku ya Alhamisi ilihusu hali katika Eneo la Maziwa Makuu na Uungaji mkono Mpango Mpana wa Kisiasa wa Umoja wa Mataifa wa Amani , Usalama na Ushirikiano wa Maendelea katika DRC na eneo la Maziwa Makuu (PSC Framework).
Anasema Bw. Kerry “ Marekani inakaribisha upelekaji wa Brigedi Maalum na inaunga mkono mamlaka iliyopewa ya kutangua makundi yote ya wanamgambo yenye silaha, na kuwalinda raia ili hatimaye Amani iweze kutawala”
Amesisitiza kwa kusema, Marekani inaunga mkono jitihada zote za kutafuta Amani katika DRC ikiwa ni pamoja na kuziunga mkono nchi 11 na wadhamini wanne (11+4) waliotia saini mpango mpana wa kisiasa na kwamba itashirikiana nao katika utekelezaji wa mpango huo.
Hata hivyo amesema, nchi yake inasikitishwa sana na taarifa mpya na za hivi karibuni zinazoonyesha kwamba bado makundi ya waasi ya M23 na FDRL yanaendelea kupewa misaada kutoka nje.
Na kwa sababu hiyo, amesisitiza kwa kuzitaka pande zote zinazohusika kuacha mara moja kuyasaidia makundi hayo na kwamba kila nchi ihakikishe wale wote wanaokiuka haki za binadamu wanachukuliwa hatua na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Kama hiyo haitoshi Bw. Kerry ametoa changamoto kwa nchi zote ambazo zimetia saini PSC Framework kuheshimu na kutoiingilia DRC katika mambo yake ya ndani ikiwamo mipaka yake.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, Mshauri wake Maalum katika Maziwa Makuu, Bi. Mary Robinson, Mawaziri kadhaa wakiwamo wa kutoka nchi za Maziwa Makuu, SADC, EU, na Umoja wa Afrika na Mkuu wa Bank ya Dunia aliyeongea kwa njia ya Video kutokea Washgton DC.
Waziri huyo wa Marekani pia amesema suala la eneo la Maziwa Makuu na DRC ni moja wapo ya vipaumbele vya serikali ya Rais Obama na kwamba kwa kuutambua umuhimu huo, Obama amemteua, Seneta mstaafu, Bw. Russ Feingold anayetajwa kuwa na uzoefu na utaalam mkubwa kuhusu masuala ya Afrika kuwa Mjumbe Maalum wa Marekani katika Maziwa Makuu.
Miongoni mwa nchi chache nje ya wajumbe wa Baraza Kuu zilizokaribishwa kuzungumza katika mkutao huo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Balozi Tuvako Manongi aliweka bayana msimamo wa Tanzania kuhusu suala zima la ushiriki wake katika mchako mzima wa utafutaji wa Amani ya kudumu katika DRC.
Katika mchango wake Balozi Manongi alianza kwa kulikumbusha Baraza Kuu la Usalama tamko la Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwamba, suluhu ya upatikaji wa Amani ya kudumu katika DRC haiwezi kuwa kwa njia za kijeshi bali ni kwa mchakato wa kisiasa na ambao nyuma yake kuna utekelezaji wa PSC Framework. Na kwamba suala la kuyahusisha makundi yote katika majadiliano bila ya kubaugua haliepukiki.
Na kwa sababu hiyo akasema ndiyo maana Tanzania inaunga mkono na kushiriki juhudi zote za kimataifa na kikanda zikiwamo za utekelezaji wa mpango mpana wa kisiasa, pamoja na utoaji wa wanajeshi wake kushiriki katika Brigedi Maalum kama sehemu ya MONUSCO kwa mamlaka iliyoainishwa katika Azimio namba 2098(2013) la Baraza Kuu la Usalama.
Akasema Brigedi hiyo Maalum inahitaji kuungwa mkono na watu wote na hasa kutoka Baraza Kuu la Usalama.
Akasisitiza kwamba Brigedi Maalum haipashwi kuvunjiwa heshima kwa tuhuma za uongo na zisizokuwa na ushahidi wowote.
Balozi Tuvako Manongi amesema katika siku za hivi karibuni kumeibuka tuhuma dhidi ya uongozi wa juu wa Brigedi Maalum na kwamba tuhuma hizo za kuwapaka matope wale wote ambao wamejitolea kwa nia njema kusaidia katika eneo la Mashariki ya Kongo, zinatia shaka.
Na kwa sababu hiyo Tanzania kupitia Mwakilishi wake huyo imelitaka Baraza Kuu la Usalama, lidai ushahidi dhidi ya tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwa Uongozi wa Juu wa Brigedi Maalum
Akalikumbusha Baraza Kuu kwamba hata Tanzania iliwahi kupata heshima ya kuwa mjumbe wa Baraza hilo, heshima ambayo iliibeba kwa dhamana kubwa , ikikatekeleza wajibu wake kwa uadilifu wa hali ya juu kwa sababu ilitambua iko ndani ya chombo hicho kuiwakilisha Afrika na Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla na kamwe si kwa maslahi binafsi au kuitumia vibaya nafasi hiyo.
Akasisitiza kwamba lazima Baraza Kuu la Usalama lichukue hatua madhubuti za kuwalinda wale ambao wamekabidhiwa jukumu hilo adhimu.
Aidha akasema Tanzania inalipongeza Baraza Kuu la Usalama kwa kuendelea kuunga mkono MONUSCO katika utekelezaji wa mamlaka iliyokabidhiwa licha ya mlolongo wa kampeni chafu kutoka kwa makundi ya waasi na waharibifu wengine.
Akasema Tanzania inaamini kwamba, kampeni hizo chafu na tuhuma zisizokuwa na ukweli dhidi ya Brigedi Maalum zinalenga kudhoofia utekelezaji wa mpango mpana wa kisiasa na kudhoofidha mamlaka ya MONUSCO.
“ Tunaamini jumuiya ya kimataifa itashinda, hakuna nguvu au propaganda chafu zitakazodhoofisha kiu ya kutafuta amani, usalama na ustawi katika eneo la Maziwa Makuu. Huu ndiyo Mpango wa Matumaini ambao Tanzania inaunga na itaendelea kuunga mkono.” Akasisitiza Balozi Manongi.
Baadhi ya nchi zilizozungumza zikiwamo Ufarasa na Uingereza zimeunga mkono mchakato wote wa upelekaji wa Brigedi Maalum huku Uingereza ikisema tuhuma za uongo na zisiokuwa na ushahidi dhidi ya Brigedi hiyo hazina maana yoyote na zinalenga kudhoofisha upatikanaji wa Amani. Na ikatakakuharakishwa upekelekaji wa teknolojia ya kisasa ya ndege ambazo haziendeshwi na binadamu ( UAVs)
Waziri kutoka Ufaransa yeye alikwenda mbali Zaidi kwa kuitaka FIB ianza kazi haraka iwezekanavyo.
Mwishoni mwa mkutano huo ilitolewa taarifa ya Rais wa Baraza Kuu, taarifa ambayo pamoja na mambo mengine ilielezea uungwaji mkono wa Brigedi Maalum, huku ikitaka makundi ya waasi wanaopigana kuacha mara moja mapingano.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)