Mahakama Yaelekeza Mazishi ya Mandela, Yaamuru Miili ya Wanawe Ifukuliwe Ikazikwe Atakapozikwa - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Mahakama Yaelekeza Mazishi ya Mandela, Yaamuru Miili ya Wanawe Ifukuliwe Ikazikwe Atakapozikwa

Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela

HATIMAYE vita iliyokuwa ikipiganwa ndani ya familia ya Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, kuhusu mahali panapostahili kuwa eneo la kuzikia miili ya wanafamilia hiyo imefikia mwisho, baada ya Mahakama Kuu ya Mthatha iliyoko Jimbo la Eastern Cape, kutoa hukumu inayoelekeza yawe katika makazi ya Mandela yaliyoko kijijini Qunu.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Jaji Lusindiso Pakade wa Mahakama Kuu ya Eastern Cape, aliyekuwa akisikiliza shauri lililofunguliwa mahakamani hapo na mtoto mkubwa wa kike wa Mandela, Makaziwe, aliyekuwa akipinga hatua ya Mandla ambaye alichukua uamuzi wa kufukua miili ya watoto watatu wa Mandela akiwamo baba yake mzazi, kutoka katika makaburi ya familia yaliyoko Qunu na kwenda kuizika katika makazi yake ya kichifu yaliyoko Mzove.
\
Jaji Pakade katika hukumu yake ya juzi, alikiita kitendo cha Mandla kufukua miili hiyo kutoka kaburini na kwenda kuizika upya bila ridhaa ya wanafamilia, kuwa hakikubaliki hivyo miili hiyo ifukuliwe na kurudishwa ilipozikwa awali.

Katika kile kilichoonekana kuwa ni vita ya kugombania uhalali wa kutwaa madaraka ya kusimamia mazishi ya Mandela baada ya kifo chake, Mandla alitangaza kutokubaliana na hukumu hiyo na haraka haraka mwanasheria wake alikata rufaa ya kuipinga. Hata hivyo, rufaa hiyo ilitupiliwa mbali na hivyo kutoa mwanya wa kufukuliwa kwa mabaki ya miili hiyo kwa ajili ya kurejeshwa kijijini Qunu.

Baada ya sekeseke hilo kwisha mahakamani hapo, Makaziwe aliyekuwa akiongoza kundi la wanafamilia 16 kudai miili ya Makgatho, Thembekile na Makaziwe, aliyodai iliibwa na Mandla usiku na kwenda kuizika katika himaya yake, alisema atasimamia irejeshwe katika eneo la makaburi la Mandela.

Makaziwe alikaririwa akieleza kuwa, kama baba yake (Mzee Mandela) angezikwa nje ya eneo la Qunu ambalo kama alivyoelekeza mwenyewe, mifupa yake ingetikisika kutoka kaburini.
Makaziwe, mtoto wa mke mkubwa wa Mandela, marehemu Evelyne, akiwa sambamba na mama zake wa kufikia, Winnie na Graca Machel, pamoja na ndugu zake wengine, aliwaongoza kwenda kuhifadhi mabaki ya miili ya ndugu zake katika chumba cha kuhifadhia maiti ambako itafanyiwa uchunguzi kabla ya kwenda kuzikwa upya katika makaburi ya Qunu.

Kurejeshwa kwa mabaki ya miili hiyo kijijini Qunu, kumetafsiriwa kuwa ni hatua muhimu ya kuondoa utata uliokuwa umejitokeza kuhusu eneo ambalo Mandela atazikwa baada ya kufa.
Pamoja na mvutano huu, Mandela mwenyewe alikwishaeleza kuwa, siku akifariki, azikwe nyumbani kwake Qunu sambamba na yalipo makaburi ya watoto wake.

Aidha, uwepo wa Winnie na Graca mahakamani wakiwa sambamba na Makaziwe katika mapambano ya kuhakikisha sauti ya Mandela inasikilizwa na kufuatwa, kumetafasiriwa kuwa ni uamuzi wa busara waliochukua ili kulinda heshima ya familia katika kipindi hiki kigumu ambacho rais huyo mstaafu yuko mahututi hospitalini.

Wakati hayo yakijiri, makundi tofauti tofauti ya wakazi wa vitongoji mbalimbali vya Soweto, jana yalikuwa yakiendesha ibada za nyimbo za shukurani kwa Mungu kwa kuinusuru familia ya Mandela na ugomvi wa eneo la kuzika miili ya marehemu wa familia hiyo.

Nyimbo hizo zilikuwa zikiimbwa kwa lugha za Kizulu, Kixhosa na Kiswana, huku baadhi ya vikundi vikiwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe wa kutoa shukurani kwa Mungu kwa kusimamia pamoja na wanafamilia ya Mandela iweweze kumaliza ugomvi wao uliokuwa ukitishia heshima ya familia na taifa.

Ikiwa ni siku ya 28 leo tangu Mandela alipolazwa katika Hospitali ya Medi Clinic, mjini Pretoria akisumbuliwa na ugonjwa wa mapafu, hali yake bado ni mbaya kwa kuwa bado anaendelea kupumua kwa msaada wa mashine.
CHANZO: www.mtanzania.co.tz

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages