JOHN MNYIKA:KAULI YA WAZIRI WA FEDHA KUHUSU KODI YA LINE ZA SIMU NI KIELELEZO CHA UDHAIFU WA SERIKALI NA UZEMBE WA BUNGE; NIANDIKIE SASA KUHUSU HATUA ZA KUCHUKUA JUU YA SUALA HILI KUPUNGUZA MZIGO WA GHARAMA ZA MAISHA KWA WANANCHI - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

JOHN MNYIKA:KAULI YA WAZIRI WA FEDHA KUHUSU KODI YA LINE ZA SIMU NI KIELELEZO CHA UDHAIFU WA SERIKALI NA UZEMBE WA BUNGE; NIANDIKIE SASA KUHUSU HATUA ZA KUCHUKUA JUU YA SUALA HILI KUPUNGUZA MZIGO WA GHARAMA ZA MAISHA KWA WANANCHI

Mbunge wa Jimbo la Ubungo -Chadema John Mnyika
---
Katika kipindi cha Hot Mix cha EATV muda mfupi uliopita Waziri wa Fedha amesema kwamba mawazo ya kutoza elfu moja kwa mwezi kwenye kila laini ya simu ni ya wabunge. 

Kauli inayokaribiana na hiyo imewahi kuandikwa pia na Naibu Waziri wa Wizara yenye dhamana na sekta mawasiliano kwenye mitandao ya kijamii katika siku za karibuni. Baadaye alifuata Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na sasa waziri mwenyewe. Mwaka 2012 nilitahadharisha kuhusu udhaifu wa Rais (na Serikali) na uzembe wa Bunge katika masuala yanayohusu maandalizi ya bajeti, hususan kutozingatiwa kwa mpango wa taifa wa maendeleo na ongezeko la mara kwa mara la gharama za maisha kwa wananchi. Kwa kauli hizi za Serikali udhaifu na uzembe huo unaendelea kujihidhirisha.

Kauli hizi za Serikali ni za kujivua mzigo wa lawama baada ya malalamiko ya wananchi kuhusu kodi hii na nyinginezo kwa kuhamisha mzigo huo kwa wabunge.

Ni muhimu badala ya kutoa kauli za ujumla za kulaumu wabunge, Serikali ijitokeze itaje kwa majina na wabunge gani hasa walitoa mawazo hayo. Mimi sijawahi kutoa wazo hilo wala kuliridhia. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwenye Hotuba yake juu ya Muswada wa Sheria ya Fedha ilipinga pendekezo hilo lililokuwepo katika jedwali la marekebisho lililowasilishwa na Wizara ya Fedha. Katika kuhakikisha kwamba kifungu hicho hakipitishwi, niliwasilisha jedwali la marekebisho ya sheria kutaka kifungu hicho kiondolewe katika muswada wa sheria ya fedha na marekebisho yake yaliyowasilishwa na Serikali.

Hata kama ikiwa ni ukweli kwamba wazo hilo ni la baadhi ya Wabunge (ambao ni muhimu wakatajwa kwa majina), Serikali inayokwepa kutetea maamuzi ambayo Serikali yenyewe imeyaunga mkono inadhihirisha kwamba imechoka na imepoteza uhalali kwa kimaadili kwa kushindwa kukubalika mbele ya wananchi wake yenyewe (illegitimate government) . 

Mamlaka na madaraka ya Bunge kwa mujibu wa katiba ibara ya 63 ni kuishauri na kuisimamia Serikali. Katika kutekeleza mamlaka hayo, Bunge ni chombo cha uwakilishi wa wananchi na chenye mamlaka pia ya kutunga sheria na kupitisha bajeti ya nchi. Hata hivyo, ibara ya 99 ya Katiba imeweka mipaka kwa mamlaka hayo ya Bunge inapokuja suala la kutunga sheria ya fedha kama hii iliyoongeza mzigo wa kodi kwa wananchi. Mamlaka hayo yamewekwa kwa kiwango kikubwa mikononi mwa Rais kupitia Waziri wake mwenye dhamana.

Ninachofahamu mimi ni kwamba kodi hiyo ya simu iliingizwa kwa mara ya kwanza ndani ya ukumbi wa Bunge na Rais kupitia kwa Waziri wa Fedha aliposoma bajeti ya Serikali. Ilikuwepo kwenye Hotuba ya maandishi ya Waziri lakini wakati wa kusoma akaruka sehemu hiyo na kutangaza kwamba imefutwa.

Waziri wa Fedha aeleze katika hatua hiyo, wazo hilo lilitoka kwa nani mpaka likaingia katika kitabu cha hotuba yake na nini maamuzi ya Baraza la Mawaziri kwenye kikao kilichofanyika siku moja kabla ya yeye kusoma hotuba yake kilichojadili hatua za kikodi (tax measures).

Kifungu hiki kilirejeshwa kwa mara nyingine tena kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha kupitia jedwali la Marekebisho lililowasilishwa na Waziri wa Fedha mwenyewe. Hivyo, ajitokeze na kueleza katika hatua hiyo, ni wabunge gani waliotaka kodi hiyo iingizwe katika muswada huo na sababu za Wizara ya Fedha kukubaliana nao.

Uzembe wa Bunge usitumike kama kisingizio cha kuficha udhaifu wa Serikali katika suala hili na mengine. Ni wazi, kuna uzembe pia kwa upande wa Bunge kwa kuacha mapendekezo ya wabunge wachache yageuzwe kinyemela kuwa ni msimamo wa wabunge wote bila ya kuwa na azimio la Bunge kuhusu mapendekezo hayo.

Katika mchango wangu bungeni kuhusu muswada huo, nilifanya rejea ya inayoitwa Kamati Ndogo ya Spika ya kupanua wigo wa mapato iliyoundwa kabla ya kuundwa kwa Kamati ya Bajeti; zote mbili zikiongozwa na Mh. Andrew Chenge (Mb).

Kamati hii ambayo haijawahi kuwasilisha ripoti yake Bungeni bali kwa Spika mwenyewe na hatimaye sasa ripoti kuwekwa kwenye maktaba ya Bunge, bila ya ripoti hiyo kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni kama taarifa ya kamati au walau kuwekwa mezani kama hati rasmi ya Bunge; sasa inatumika kusukuma mzigo wa lawama kwa Bunge na wabunge.

Baada ya kamati hii, majadiliano kati ya Serikali na Kamati ya Bajeti yaliyofanyika kwa nyakati mbalimbali yanatumika kuhalalisha maamuzi ya Serikali yenye kuongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi katika hali yenye kudhihirisha uzembe wa Bunge wa kuachia mamlaka na madaraka yake kutumiwa visivyo.

Katika muktadha huu, kulaumiana kati ya Serikali na Wabunge au kulalamika kwa wananchi pekee hakutoshelezi kuwezesha uwajibikaji au mabadiliko yanayokusudiwa. Lawama ziendelee kwa kuwa zinasaidia kuendeleza mjadala na kufanya ukweli uoendelee kutolewa na pande zote. Malalamiko ya wananchi yaendelee kwa kuwa inawezesha Serikali na wabunge kutambua athari za maamuzi hayo kwa wananchi.

Tunapaswa kwenda mbele zaidi kwa wewe, mimi na mwingine kuchukua hatua? Wewe unapendekeza hatua gani zichukuliwe? Nitatoa msimamo wangu kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa baada ya kupata maoni yenu kwa kuniandikia kupitia mbungeubungo@gmail.com. Maslahi ya umma kwanza.
 
JOHN MNYIKA (MB)
11/07/2013

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages