Askari saba wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliouawa katika jimbo la Darfur nchini Sudan, wanatarajiwa kuagwa leo kwenye viwanja vya makao makuu ya jeshi hilo.
Miili ya wanajeshi hao iliwasili nchini juzi kwa ndege maalumu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J. K Nyerere, Terminal One na kwenda kuhifadhiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Lugalo jijini Dar es Salaam.
Wanajeshi waliouawa ni Sajenti Shaibu Othuman, Koplo Oswald Chaula, Koplo Mohamed Juma, Koplo Mohamed Chikilizo, Rodney Ndunguru, Peter Werema na Fortunatus Msofe.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano, Makao Makuu ya JWTZ, ilieleza kuwa askari hao wataagwa leo na shughuli hiyo itahudhuriwa na familia, makamanda wa jeshi na viongozi wa Serikali.
“Shughuli ya kuaga kwa heshima za kijeshi itaanza saa tatu kamili asubuhi katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Upanga na itaendelea mpaka mchana kabla ya kusafirishwa,” ilisema taarifa hiyo.
Wanajeshi hao ambao ni miongoni mwa askari wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani katika Jimbo la Darfur nchini Sudan, waliuawa kutokana na mashambulizi ya kushtukiza yaliyofanywa na waasi wanaopigana na Serikali, hivyo kuwa ni mara ya kwanza kwa idadi kubwa ya wanajeshi wa Tanzania wanaolinda amani katika nchi mbalimbali kuuawa kwa wakati mmoja.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)