Baadhi ya wanafunzi Sekondari ya Nduweni wakiwa darasani
Baadhi ya wanafunzi wa Sekondari ya Urauri, Wilaya ya Rombo
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Nduweni Sekondari, Venance Mramba
Sehemu ya maktaba ya Sekondari ya Tanya, ikionesha utitiri wa vitabu vya sayansi japokuwa haina walimu wa somo hilo
Na The Habari.com
KITENDO
cha upungufu wa walimu wa sayansi nchini hasa katika shule za sekondari
zinazomilikiwa na serikali kimezidi kuibua changamoto maeneo mbalimbali
nchi. Shule ambazo kwa sasa zinakabiliwa na changamoto hiyo kwa kiasi
kikubwa ni sekondari za kata ambazo uwingi wake umechochea zaidi
changamoto hiyo.
Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro ni miongoni mwa
maeneo ambayo yanakabiliwa na changamoto hiyo ya uhaba wa walimu wa
sayansi kama ilivyo kwa mikoa tofauti ya Tanzania. Hata hivyo walimu
wakuu wa shule zenye changamoto wamebuni mbinu mbadala kukabiliana na
hali hiyo.
Zoezi la uhamasishaji ujenzi wa shule za sekondari
za kata limekuwa na mafanikio kiasi kikubwa katika Halmashauri ya Wilaya
ya Rombo, kwani hadi sasa wilaya hiyo imefikisha jumla ya sekondari 41
zilizo chini ya serikali ikiwa ni jitihada za wananchi kwa kushirikiana
na viongozi wao.
Mwandishi wa makala haya amefanikiwa kutembelea
shule sita tofauti za sekondari za kata wilayani Rombo na kufanya
mazungumzo na walimu wakuu, walimu na wananfuzi ambao wanatoa picha
halisi ya uhaba wa walimu wa sayansi. Miongoni mwa shule zilizotembelewa
ni pamoja na Sekondari za Nduweni, Tanya, Urauri, Holili na Ngaleku.
Victus Kiwango ni Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Tanya
iliyopo wilayani Rombo. Mwalimu huyu anasema uhaba wa walimu wa masomo
ya sayansi ni moja ya tatizo zinaloikabili shule hiyo. Kiwango anasema
shule yake haina kabisa walimu wa masomo ya Kemia, Fizikia na Baiolojia
hivyo hulazimika kutumia walimu wa kukodi kwa vipindi tofauti.
Anasema shule hiyo hutegemea wanafunzi kadhaa
waliomaliza kidato cha sita ambao huwakodi na kufundisha masomo hayo
pale wanapopatikana ili wanafunzi waweze kupata chochote na hatimaye
baadaye kufanya mitihani ya sayansi. "...Hapa shuleni kwetu (Tanya
Sekondari) masomo ya sanyansi ndio tatizo, mfano hatuna kabisa walimu wa
masomo ya Kemia, Fizikia pamoja na Baiolojia hivyo huwa tunakodisha na
shule kuwalipa," anasema Kiwango.
Hata hivyo kero na kilio cha uhaba wa walimu
kinasikika tena katika sekondari ya duweni wilayani humo. Mwalimu Mkuu
Msaidizi wa sekondari hiyo, Venance Mramba anasema tatizo la uhaba wa
walimu wa masomo ya sayansi linaiathiri shule hiyo kitaaluma. Anasema
shule miaka yote shule hiyo imekua ikianzia ufaulu wa daraja la pili.
Anatolea mfano katika matokeo ya mwisho ya kidato
cha nne (juzi), ilifanikiwa kufaulisha mwanafunzi mmoja kwa daraja la
pili na wanne kwa daraja la tatu. Anaongeza kuwa katika matokeo hayo
wanafunzi 25 walipata daraja la nne na wanafunzi 70 wakiambulia sifuri,
kati ya idadi ya wanafunzi 102 waliofanya mtihani huo wa mwisho wa
taifa.
"Tatizo kubwa la kufaulu ni uhaba wa walimu wa
masomo ya sayansi ikiwemo hesabu na mengineyo, uhaba wa vifaa vya
ufundishaji na kujifunzia pamoja na upungufu wa vitatu vya masomo yote,"
anasema mwalimu Mramba katika mahojiano na mwandishi wa makala haya.
Anaongeza ili kukabiliana na upungufu wa walimu wa
sayansi shule hiyo huajiri kwa muda wanafunzi waliohitimu kidato cha
sita na kuwasaidia kuwafundisha wanafunzi masomo hayo. Hata hivyo
anasema bado kuna changamoto kubwa katika kuwatumia walimu hao wahitimu
wa kidato cha sita, kwani hawana mbinu za kufundishia jambo ambalo bado
ni kikwazo katika shule hiyo.
Benson Samizi ni Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Sekondari
ya Holili iliyopo katika Wilaya ya Rombo. Mwalimu huyu anasema japokuwa
hali ya kitaaluma shuleni hapo si mbaya sana lakini shule inakabiliwa na
upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi kama ilivyo katika shule
nyingine wilayani hapo.
Mwalimu Samizi anasema shule hiyo haina kabisa
walimu wa masomo ya Fizikia na Hesabu na hulazimika kukodi walimu wa
muda ili kuwaandaa wanafunzi. Shule hii haina maabara japokuwa ina
vitabu vya kutosha vya masomo ya sayansi. Akizungumzia ufaulu wa kidato
cha nne kwa mwaka 2011, anasema shule ilipata mwanafunzi mmoja aliyekuwa
na daraja la kwanza na wengine wawili waliopata daraja la pili, huku
wanafunzi watatu wakipata daraja la tatu.
Samizi anaendelea kubainisha kuwa katika matokeo
hayo jumla ya wanafunzi 55 walipata daraja la nne na 18 kuambulia patupu
(sifuri) kati ya watahiniwa 80 waliofanya mtihani wa mwisho wa taifa
kuhitimu kidato cha nne mwaka 2011.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya
Urauli, iliyopo Tarakea wilayani Rombo, Sim Silayo anasema mbali na
biashara zinazofanyika mpakani mwa Tanzania na Kenya eneo hilo kuathiri
taaluma kimaudhurio, upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi ni kero
nyingine shuleni hapo.
Mwalimu Silayo anaeleza kuwa shule hiyo haina kabisa
walimu wa masomo ya Fizikia, Kemia na Baiolojia; hivyo uongozi wa shule
kulazimika kukodi walimu wa muda wa masomo ya sayansi wakiwemo baadhi
ya wanafunzi waliohitimu kidato cha sita wanaosubiri kuendelea na masomo
yao ya juu. Aidha anaongeza kuwa shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007,
yenye jumla ya wanafunzi 464 haina maabara wala vitabu vya kutosha licha
ya kukabiliwa na changamoto zingine mbalimbali.
Yehova Mashalo ni mwanafunzi wa kidato cha nne Shule
ya Sekondari Tanya anasema wapo wanafunzi wengi ambao hukata tamaa
kuchukua masomo ya sayansi tangu wakiwa madarasa ya chini kutokana na
kukosekana kwa walimu wa masomo hayo. Kwa upande wake Joice Kimaro
mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya Sekondari Tanya anaongeza kuwa
kutojitosheleza kwa walimu wa sayansi shule za sekondari hasa za kata
inakatisha tamaa wanafunzi kupenda masomo hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Rombo, Judethadeus
Mboya anasema halmashauri yake inajitahidi kuongeza idadi ya walimu kila
mwaka ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa walimu. Anasema kwa
uwiano wa kawaida Wilaya ya Rombo haina upungufu mkubwa wa walimu,
lakini una upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi.
Anasema kwa sasa wilaya ina jumla ya walimu 800,
huku kwa mwaka huu pekee ikiwa imeajiri walimu 134 wakiwemo wa masomo ya
sayansi. "...Kwa suala la upungufu wa walimu Wilaya ya Rombo ni tofauti
na maeneo mengine, hapa kuna upungufu wa walimu wa masomo; kama Hesabu,
Fizikia, Kemia na Baiolojia nitatizo," anasema Mkurugenzi Mboya.
Hata hivyo anakiri kutokana na suala la uhaba wa
walimu wa masomo ya sayansi zipo shule ambazo zimelazimika kutumia
walimu wa kukodi na kutumia wanafunzi waliomaliza kidato cha sita ili
shule iweze kwenda mbele. Anasema kuwa lengo kubwa la halmashauri hiyo
ni kuhakikisha inatatua changamoto hiyo kila inapotokea nafasi.
Kwa upande wake Katibu wa CWT Wilaya ya Rombo,
Erasmo Mwingira anasema vijana wa kidato cha sita ambao hutumiwa na
baadhi ya shule kuokoa jahazi la masomo ya sayansi wamekuwa hawafundishi
zaidi ya kuwakaririsha wanafunzi kujibu mitihani jambo ambalo
anatahadharisha huenda likawa na madhara makubwa kwa elimu yetu
Tanzania.
"Kujua kusoma na kuandika si kigezo cha kumfundisha
mtu...vijana hawa wa kidato cha sita hawana mbinu za ufundishaji,
wanachokifanya ni kuwakaririsha wanafunzi," anasema Mwingira. Pamoja na
hayo mdau huyu wa elimu anaishauri serikali kutojitoa katika jukumu la
kuendesha shule za kata kwa kuwaachia wazazi kwani shule hizo ziko
katika hali mbaya na zinahitaji kuongezewa fedha za uendeshaji.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)