Sekondari za Kata Mzigo Mpya kwa Wakuu wa Shule - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Breaking

Home Top Ad

Responsive Ads Here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Sekondari za Kata Mzigo Mpya kwa Wakuu wa Shule

 
Victus Kiwango, Mkuu wa Sekondari ya Tanya

Na Thehabari, Rombo

KUANZISHWA kwa Sekondari za Kata maeneo mbalimbali nchini kulikuwa na matumaini makubwa kwa wananchi. Maeneo mengi uitikio wa wananchi umekuwa mkubwa na shule hizo kujengwa kwa wingi hali ambayo imegeuka kuwa mzigo tena kwa Serikali kutokana na kuelemewa katika kuzihudumia baadhi ya shule hizi kwa baadhi ya maeneo.

Baadhi ya shule hizi zimekuwa zikikubwa na changamoto kadha wa kadha hivyo kuwa kikwazo kikubwa katika kufanya vizuri kitaaluma. Uchache wa vifaa vya muhimu vya kujifunzia na kufundishia, walimu stahili hasa wa sayansi na uduni wa miundombinu ya kutosha ya shule imebaki kuwa changamoto zaidi.

Kimsingi kwa tafsiri rahisi inaonekana wazi wazi kuwa Serikali imeelemewa na mzigo wa kuziendesha kihuduma shule hizi. Na sasa mzigo huo umeangukia kwa walimu wakuu wanaoziongoza shule hizo.

Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo yaliokuwa na muitikio mkubwa wa ujenzi wa shule hizi. Wilaya hii kwa sasa imefikisha jumla ya Shule za Sekondari 41 za Serikali, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na hapo nyuma kabla ya zoezi la uhamasishaji wa ujenzi wa shule hizo.

Mwandishi wa makala haya amezungukia baadhi ya shule hizi na kufanya mahojiano na walimu, wanafunzi, wazazi/walezi, wadau wa elimu pamoja na viongozi wa maeneo hayo kuangalia changamoto anuai zinazo zikabili shule hizi.
Baadhi ya wanafunzi wa moja ya Sekondari za kata, Rombo wakiwa darasani
Urauri Sekondari ni miongoni mwa shule za Kata zilizoanzishwa Tarafa ya Tarakea wilayani Rombo ikiwa ni mpango wa Serikali kuendelea kusogeza elimu ya sekondari kwa wananchi wake. Shule hii licha ya kukabiliwa na changamoto nyingine kadhaa, hadi sasa haina walimu wa masomo ya sayansi kama Baiolojia, Hisabati, Kemia pamoja na Fizikia.

Sim Silayo ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Urauri, anakiri kuwa kukosekana kwa walimu wa sayansi kuwafundisha wanafunzi muda wote kiutaratibu ni miongoni mwa vikwazo vya kufanya vizuri kitaaluma kwa shule yake. Hata hivyo anasema hali hiyo haimkatishi tamaa ya wanafunzi wake kufundishwa masomo ya sayansi shuleni hapo.

Anasema ili kuziba pengo la walimu wa sayansi shuleni hapo ametafuta walimu wa muda ambao ni vijana waliomaliza kidato cha sita na wanaendelea kumsaidia kufundisha masomo ya Fizikia, Baiolojia, Kemia pamoja na Hisabati. Anasema vijana hao wanalipwa ujira wao na shule kwa kutumia michango inayopatikana shuleni.

Anasema mwitikio wa ulipaji ada wa wazazi ni mdogo na fedha zinazotolewa na Serikali hazitoshi kuendesha shule, hivyo hulazimika kutumia mbinu kadhaa kuchangishana na wazazi kuhakikisha wanapata chochote kusaidia baadhi ya gharama za shule. "Shule hii ni mchapuo wa kilimo lakini watoto walikuwa hawasomi somo hilo kutokana na kutokuwa na mwalimu husika wa somo...juzi nimejitahidi kwa kushirikiana na wazazi tumechanga na kumpata mwalimu wa kilimo wa muda...hapa michango ya wazazi pamoja na fungu la taaluma limetuokoa," anasema Silayo.

Kama hiyo haitoshi mwalimu Silayo anasema shule yake haina vitabu vya kutosha, maktaba, maabara na changamoto ya mazingira ya kuvutia kimiundombinu kwa wanafunzi kusoma.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Rombo, Judethadeus Mboya
Hata hivyo kilio kama hicho cha ukosefu wa walimu wa sayansi kimeangukia tena katika Sekondari ya Holili, Wilayani Rombo. Benson Samizi ni Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, anasema shule hiyo haina kabisa walimu wa masomo ya sayansi na badala yake hutumia wanafunzi wa kidato cha sita kufundisha kwa muda na uongozi wa shule kuwalipa ujira wao.

"Shule yetu imebahatika kuwa na vitabu vya sayansi vya kutosha, lakini hatuna kabisa mwalimu wa masomo ya Fizikia na Hisabati...pamoja na hali hiyo ili mambo yasiwe mabaya zaidi tunakodi vijana ambao hutusaidia masomo haya kwa muda kuwafundisha wanafunzi wetu na kulipwa na shule chochote kinachopatikana," anasema mwalimu huyo.

Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Rombo, Erasmo Mwingira anasema shule nyingi za kata zina walimu wa masomo ya sanaa zaidi na hazina walimu wa Sayansi wa kutosha. Anaongeza kuwa licha ya Serikali kujua tatizo hilo bado imeendelea kuwapa mitihani ya masomo ya sayansi wanafunzi bila kujali kama wanafunzi hao wamefundishwa masomo hayo.

"...Katika Shule nyingi zina walimu wa sanaa, walimu wengi katika shule hizi ni wa sanaa lakini wanapokuja kumpima mtoto (mwanafunzi) anapimwa kwa masomo ya sanaa na sayansi bila kujali kama amefundishwa kwa njia gani masomo hayo

Mwingira anabainisha kuwa fedha zinazotolewa kuziendesha shule hizo 'capitation' hazitoshi na mara nyingine huwa hazifiki kwa kwa wakati shuleni hali ambayo huwalamimu walimu wakuu kubuni mbinu mbalimbali za uendeshaji wa shule zao, ikiwemo kuweka utitiri wa michango kwa wazazi ili kuhakikisha mambo yanaendelea.

"Sasa hivi shule hizi zinaendeshwa na mifuko ya walimu wakuu...'capitation' haifiki kabisa shuleni, fedha inayowafikia ni kidogo sana na haiwezi kuendesha zile shule, walimu wanatumia mbinu zao kuziendesha shule ndio maana unaona michango inakuwa mingi shuleni," anaeleza Mwingira akizungumza na mwandishi wa makala haya.

Anaongeza kuwa licha ya serikali kusisitiza kwamba ada ya sekondari ni shilingi 20,000 kwa sasa michango katika shule hizo ni mingi kiasi cha kufikia 120,000 jambo ambalo limewafanya baadhi ya wazazi kuzidiwa na mzigo wa michango na wengine kushindwa kabisa kuimudu. Mdau huyu wa elimu anasema vijana wa kidato cha sita ambao hutumiwa na shule nyingi kuokoa jahazi ya masomo ya sayansi wamekuwa wakiwakaririsha wanafunzi kujibu mitihani na sio kuwafundisha jambo ambalo ni hatari kwa elimu ya Tanzania hapo mbeleni.

"Kujua kusoma na kuandika si kigezo cha kumfundisha mtu...vijana hawa wa kidato cha sita hawana mbinu za ufundishaji wanachokifanya ni kuwakaririsha wanafunzi. Pamoja na hayo anaishauri serikali kutojitoa katika jukumu la kuziendesha shule za kata na kuwaachia wazazi kwani shule hizo ziko katika hali mbaya na zinahitaji kuongezewa fedha za uendeshaji.

Victus Kiwango ni Mkuu wa Sekondari ya Tanya, anaishauri Serikali kuongeza fungu la uendeshaji wa fedha shuleni kwani fedha za michango zinazotolewa na wazazi hazitoshi kuendesha shule. Anasema shule huwa zinakodi wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na kuwasaidia wanafunzi kwa muda masomo ya sayansi hivyo shule kuwa na gharama kubwa za uendeshaji.

"Sisi tumelazimika kuajiri kwa muda wanafunzi sita waliomaliza kidato cha sita kufundisha masomo ya sayansi kwa fedha za shule...tunajibanabana kwa michango pamoja na wazazi na kuhakikisha tunapata chochote kuwalipa walimu hawa wa muda bila hivyo mambo hayaendi," alisema Mkuu Msaidizi wa Sekondari ya Nduweni, Venance Mramba akizungumza na mwandishi wa habari hizi.

Pamoja na hali hiyo uchunguzi wa kina uliofanywa katika shule za Sekondari za Tanya, Nduweni, Urauri, Holili na Ngaleku na nyinginezo za wilayani Rombo, umebaini uwepo wa ongezeko la michango shuleni hali ambayo imelalamikiwa na baadhi ya wazazi na wadau wa elimu wilayani waliozungumza. Uchapaini shule ya Sekondari Tanya imefikisha jumla ya michango sh. 115,000; mgawanyiko wake ukiwa kama ifuatavyo; Ada sh 20,000, Madawati sh 15,000, Chakula sh 60,000, Tahadhari sh 5,000, Ulinzi 5,000, Taaluma sh 5,000 na Kitambulisho sh 5,000.

Aidha uchunguzi zaidi umebaini shule nyingi za sekondari za kata hazina walimu wa masomo ya sayansi jambo ambalo huwalazimisha walimu wakuu kutafuta walimu wa kukodi hasa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita kuja kuwafundisha wanafunzi masomo ya sanyansi kama Hisabati, Fizikia, Kemia, Baiolojia na mengineyo huku wakitumia mbinu anuai kukusanya michango kuwalipa walimu hao wa kukodi.

Judethadeus Mboya ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Rombo, katika mazungumzo na makala haya anakiri kuwepo na tatizo la upungufu wa walimu wa sayansi katika shule nyingi za wilaya yake, hivyo walimu kulazimika kuajiri kwa muda vijana wa kidato cha sita kusaidia wanafunzi huku jitihada zikiendelea kufanya kukabiliana na tatizo hilo.

"Walimu wa sayansi ni tatizo Rombo hawatoshi...mwaka huu tumejitahidi na kuajiri takribani walimu 134 wakiwemo wachache wa masomo ya sayansi lakini tatizo bado lipo," alisema Mboya kikilitolea ufafanuzi suala hilo ofisini kwake wilayani Rombo hivi karibuni. Hata hivyo kiongozi huyu mtendaji wa wilaya anasema licha ya changamoto zilizopo katika shule hizo bado zinanafasi ya kufanya vizuri kitaaluma endapo walimu wa kuu watajitoa kikamilifu katika kusimamia utendaji wa shughuli shuleni hapo.

"...Walimu wakuu ndio msingi wa kufanya vibaya kitaaluma katika shule, endapo mwalimu mkuu atatumia uwezo na ukakamavu katika kuongoza shule yake itafanikiwa...mwalimu huyu akitumia uwezo wake kuwaongoza vizuri walimu wengine lazima atafanikiwa na shule itafanya vizuri kitaaluma," anasema Mboya.

Imeandaliwa na www.thehabari.com

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here

Pages